SIKU YA MTOTO WA AFRICA 16/6/2017

16 June 2017
Published in NEWS
Siku ya mtoto wa Afrika huazimishwa tarehe 16/06 kila mwaka. Siku hii ilianzishwa na OAU (organization of Africa Unit) na imeanza kuazimishwa toka mwaka 1991 ili kuwapa heshima watoto wale ambao walishiriki maandamano ya Soweto mwaka 1976. Katika maandamano haya ya Soweto, zaidi ya watoto 10,000 walioshirikiki maandamano kati yao waliuwawa na wengine walijeruhiwa. Haya yaliwakuta wakiwa katika harakati za kutetea haki zao, miongoni mwa hayo ni elimu bora na yenye kukidhi matakwa yao. Siku hii ya mtoto wa Africa ambayo kauli mbiu yake kitaifa ni “Maendeleo endelevu 2030: Imarisha ulinzi na Fursa sawa kwa watoto” ambayo inalenga jamii kuwajibika ipasavyo kwa watoto, kwetu TAMWA na wadau wengine washiriki, inatukutanisha na ninyi waandishi wa habari kujadili changamoto zinazowakabili watoto wa Taifa letu la Kitanzania sasa na siku za usoni. Miongoni mwa changamoto hizo ni ukatili wa kijinsia katika ngazi ya  familia. Tukumbuke kwamba familia ni taasisi inayojitegemea na yenye utaratibu, kanuni na uongozi kamili. Malezi na makuzi ndiyo dira, maono na dhamira yetu kwa watoto wetu. Katika malezi tunatazamia matendo yote yafanywe na wazazi/walezi na jamii, kwa lengo la kumlea, kumkuza kumlinda, na kumwendeleza mtoto kimwili, kikakili, kihisia na kimaadili ili aweze  kukua vizuri na kukabiliana na changamoto za kijamii. Ni dhahiri kwamba misingi hii bora ya malezi na makuzi kwa watoto wetu imeporomoka kabisa. Hali hii imepelekea watoto katika jamii zetu kufanyiwa ukatili wa kiwango cha juu kabisa.  Familia zetu siyo salama tena.  Tumepoteza utu na misingi mizuri ya imani ya dini, mila na desturi nzuri za mtanzania. Kiwango cha ukatili wa watoto majumbani kimepanda hadi kufikia asilimia 49 mwaka 2017.  Kiwango hiki ni cha juu zaidi ya kile cha asilimia 15% cha watoto kufanyiwa ukatili shuleni na asilimia 23% cha watoto kufanyiwa ukatili sehemu nyingine. Kwa uhalisia huu, ukatili wa majumbani hauwezi kutuacha salama kama hatutachukua hatua kama wazazi/walezi ndugu na jamaa. Ukatili  wa kijinsia kwa watoto wa kike na kiume umeenea sana kwenye jamii nyingi Tanzania. Tafiti zinaonyesha kuwa watendaji wa ukatili huu ni watu wa karibu sana na wengine huwa ni waathirika wa vitendo hivyo wakiwemo wazazi, welezi, ndugu jamaa, na majirani au waajiri. Sababu kubwa za ukatili huu ni pamoja na mitazamo ya kijamii kuhusu ukatili na unyanyasaji, uwezo wa mifumo ya ulinzi na ustawi wa jamii.   Tukumbuke ukatili wa jinsia utaligharimu Taifa na jamii kwa kiwango cha  juu kwa sasa na baadae. Ukatili dhidi ya watoto una madhara makubwa kwa afya ya mtoto kihisia, kitabia na kimwili. Pia huathiri maendeleo ya mtoto kijamii katika maisha yake yote. Watoto wanaotendewa ukatili, unyanyasaji na unyonyaji hukabiliwa na hatari ya kufanya vibaya katika masomo yao. Aidha vitendo vya kikatili ndio sababu kubwa ya watoto kukimbia nyumbani na kwenda kuishi mitaani. Hii huongeza uwezekano wa watoto kuishi katika mazingira ya umaskini. Pia upo mwanya kwa watoto kuendeleza vitendo vya ukatili kwa watoto/wenzao na si hivyo tu pia wanapokuwa watu wazima huuendeleza ukatili huo kwa watoto wao na kujihusisha na tabia nyingine zisizokubalika kijamii na ambazo huigharimu jamii. Watoto waliowahi kufanyiwa ukatili wapo katika uwezekano mkubwa wa kujiingiza katika tabia hatarishi ambazo huweza kuwasababishia hata maambukizo ya VVU/UKIMWI,  matumizi ya dawa za kuleya, wizi, ujambazi na hata ugaidi. Utafiti wa ukatili mwaka 2015/16 kwa watoto umegundua kuwa watoto wa kike na wakiume wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia kwa sasa , wana uwezekano mkubwa zaidi wa kufanya ngono na wapenzi wengi kuliko wale ambao hawafanyiwi ukatili. Hali hii inaibuwa wasiwasi wa  ongezeko la maambukizi ya VVU kwa kundi hili. Kundi hili lipo katika hatari ya kufanya biashara ya ngono ili kupata fedha au vitu vingine. Viwango vya ukatili unaohusisha ngono vinaongezeka kulingana na umri, kuanzia asilimia 8 kwa wanawake wenye umri wa miaka 15-19 hadi asilimia 18 kwa wanawake wenye umri wa miaka 40 – 49. Aidha wanawake 4 kati ya 10 wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15 nchini Tanzania, kama ambavyo vimebainishwa na Utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto na Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Tanzania mwaka 2015 /16. Katika hali isiyoweza kuelezeka hivi karibuni Wanafunzi 101 wamepewa ujauzito katika kipindi cha miezi sita kwa mwaka huu 2017, matukio hayo yametokea Mkoani mwanza wilayani ukerewe. Kwa masikitiko makubwa inasemekana vitendo hivyo vimefanywa na viongozi ngazi ya kata na vijiji. Na imethibitika kuwa wazazi na serekali za vijiji ndiyo kichocheo kikubwa kwa watoto  kupata ujauzito(Tanzania Daima 12/6/2017) Je ni watoto wangapi walifanyiwa ukatili huo na hawakupata mimba?Je ni wavulana wangapi walifanyiwa ukatili huo? Tanzania ipo katika hatari kubwa sana ya kuwa nchi yenye watoto na vijana (Waliopo katika kundi hatarishi (Key Population) ifikapo 2030 endapo jitihada za lazima juu ya ulinzi, malezi na makuzi bora, ya watoto wetu hayatazingatiwa. Ukatili dhidi ya watoto wetu unaosababishwa/kufanywa na wazazi na walezi majumbani ni mkubwa katika jamii zetu ambapo wakati mwingine mama amediriki kumchoma mtoto wake kwa kosa la kuiba kiasi cha shilling 7000 (Mtanzania 12/6/2017). Ndoto za watoto wetu zimezimwa ghafula. Ukatili dhidi ya  watoto  wetu kamwe hautatuacha salama. Kwa mfano mkoani Katavi mtoto wa kike alibakwa hadi kupoteza maisha(Majira 12/6/2017).Huu ni Unyama usiokuwa na mfano. Veronika Lucas(13) ndoto zake zakuwa rubani zimezikwa. Siku moja kabla ya mauti alimjulisha mama yake ndoto zake za kuwa rubani wa Tanzania,lakini ukatili wa kinyama ulizika matumaini yake. Tunakusihi ewe Yarabi umpekee veronica lucas kama ulivyompokea Yabili Wazazi tumekosa utu. Sisi ndiyo wachochezi na watekelezaji wa ukatili dhidi ya watoto. Malezi yetu na makuzi yamekuwa na ukatili usio kifani. Tumeyasahau majukumu na wajibu wetu kama wazazi/ walezi. Malezi na makuzi siyo salama kwa watoto wetu, makundi rika na mitandao isiyokuwa na maadili imechukua sehemu yetu wazazi. Kizazi kijacho hakina matumaini,kimetelekezwa. Kupitia kwenu waandishi wa habari, tunatoa wito kwa umma wa watazania wazazi na walezi, kuwa milango yetu TAMWA ipo wazi kukusaidia wewe mzazi/ mlezi kulea vyema. Ni imani yetu kuwa UKIMPENDA MTOTO UTAMLINDA   Malengo Mahsusi Kutoa mwongozo kwa waaandishi wa habari wawezeshaji wengine wa jamii katika ngazi ya jamii kuhusu stadi za malezi kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto Kuongeza uelewa na kuhamasisha uzingatiaji wa stadi zisizo katili katika malezi na makuzi ya watoto miongoni mwa wazazi na walezi wengine. Kuogeza uwezo wa wazazi na walezi, kuzungumza kwa uwazi kuhusu ukatili unaondelea katika jamii; na hivyo kutoa jukwaa la majadiliano kuhusu ukatili dhidi ya watoto kama fursa kwa jamii kukiri na kutambua yale yasiyokubalika na kujadiliana utaratibu wa kuyazuia.

OUR YOUTUBE VIDEOS

Events - Calendar

November 2017
Mon Tue Wed Thu Fri Sat Sun
1
2
3
4
5
6
7
8
9
10
11
12
13
14
15
16
17
18
19
20
21
22
23
24
25
26
27
28
29
30

FOLLOW US ON FACEBOOK

JoomShaper