NEWS

NEWS (98)

TAMWA KUTEMBELEA VYOMBO VYA HABARI

11 October 2016 Written by
Published in NEWS
Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani ambayo huadhimishwa tarehe 11 Oktoba ya kila mwaka, wafanyakazi wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) wamevitembelea  baadhi ya vyombo vya habari nchini. Lengo kubwa likiwa ni kuwapongeza wanahabari kwa namna  wanavyoibua na kuandika habari za ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto pamoja na  kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za watoto, jambo  ambalo limewafungua wananchi kuona ni hatua zipi za kuchukua pindi wanapoona vitendo hivyo katika jamii au familia vinatokea. Mbali na pongezi, TAMWA wanavipongeza vyombo vya habari vyote nchini kutokana na kuweza kutoa nafasi kubwa kuchapisha habari za ukatili wa kijisia kwa wingi na hata kuzipa uzito wa kuzichapisha  katika kurasa  za mbele tofauti na miaka ya nyuma.
Chama cha wanahabari wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na waandishi kutoka mkoa wa Kilimanjaro walikutana kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa ushirikiano ulio thabiti katika mradi endelevu wa majaribio kwa wasaidizi wa kisheria na serikali za mitaa kulinda haki za wanawake kuepukana na unyanyasaji wa kijinsia. Mkutana huo uliofanyika tarehe 20 September, 2016 ulikutanisha wadau mbalimbali pamoja na wanahabari. Ambapo pia wanahabari wamewezeshwa kutoa taarifa ya kazi wanazofanya wasaidizi wa kisheria hususani katika kuelimisha jamii ili kupinga vita ukatili wa kijinsia kwa kupitia vyombo vya habari vya kitaifa na kijamii. Mmoja wa wanahabari wa Boma Hai FM, Omary Mlekwa pamoja na wanahabari wenzake walieleza na kutoa mifano ya kazi nzuri ambazo wasaidizi wa kisheria wanazifanya na zinaleta usawa katika jamii. Hii imejidhihirisha wazi kutokana na jinsi jamii sasa ilivyoelimika kwani aina yeyote ya ukatili imekuwa ikitolewa taarifa mapema. Hivyo basi, kupitia wao sifa nyingi zimesikika kwani wamekuwa ni watu wa karibu sana kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure. Mradi huo unaoendeshwa na TAMWA kwa ushirikiano na Kilimanjaro Women Information Exchange and Consultancy Organisation (KWIECO) kwa ufadhiliwa wa Legal Service Facility (LSF) ambao TAMWA waliweza kukutana na wasaidizi wa kisheria mnao tarehe 23/9/2016 kutoka kata tano (5) za Ivaeny, Graragua, Sanya Juu, Biriri na Nasai. Kwa madhumuni ya kujadili changamoto kwa kutumia   mpango mkakati wa kihabari ulioandaliwa na wasaidizi wa kisheria. Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Amani Centre uliopo wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro na kufunguliwa na Afisa   mradi huo Bi Suzana Charles Mwaitenda . Sehemu kubwa ya mkutano ilikuwa ni ufuatiliaji wa mradi na kuhakikisha utekelezaji wa mradi shirikishi wa wasaidizi wa kisheria na serikali za mitaa katika   kulinda haki za wanawake unakuwa ni wa mafanikio.
Wanachama na wafanyakazi wa kituo cha usuluhishi ( CRC ) wamekutana pamoja leo tarehe 15.09.2106 katika ukumbi wa TAMWA uliopo Sinza mori Dar es salaam kujadili mpango kazi wa miaka 5 ambao unatarajia kuanza mwaka 2017-2021,CRC ni kutuo cha usuluhishi cha TAMWA ambacho kilianzishwa kwa lengo la kutoa huduma ya ushauri unasihi na msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia . Kituo kimefanikiwa kutoa huduma kwa wahanga takribani 70 kwa mwezi na kimeweza kujengea uwezo wasaidizi wa sheria 60 katika kata za Ruangwa mjini,Nachingwea( Ruangwa ),Luchingu ( Newala ), Makumbusho (Kinondoni),Nchinga ( Lindi Vijijini ). Aidha kimefanikiwa kutoa huduma kwa njia ya simu na mtandao kwa wahanga kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani.
TGNP kwa kushirikiana na Action Aid Tanzania (AATz),pamoja na mashirika yanayotetea haki za wanawake na watoto ambayo ni TAMWA, WiLDAF na TAWLA wameshiriki katika kufanikisha maadhimisho ya Tamasha la Jinsia la Wilaya pamoja na kusanyiko dogo la Kilimanjaro Initiative ambayo kwa pamoja yamefanyika kuanzia tarehe 8 hadi 10 Septemba 2016. Maadhimisho haya yamefanyika katika Mkoa wa Morogoro wilaya ya Morogoro katika kata ya Mkambarani kwenye viwanja vya Moseka. Tamasha hili ni sehemu ya maandalizi ya kusanyiko kubwa la wanawake wa Afrika la haki ya umiliki ardhi, linalotarajiwa kufanyika mwezi Octoba mwaka huu. Dhima kuu ya maadhimisho haya ni “Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Huduma bora za Jamii ni Haki Kwa maendeleo endelevu”. 2016 ukiwa ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa (FYDP) vyote vikiwa vimelenga kutokomeza umasikini na kupunguza mwanya kati ya walio nacho na wasio nacho, ni muda muafaka kwa mihimili yote ya serikali, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi kuhakikisha rasilimali za nchi hasa ardhi na huduma bora za jamii zinafikika kirahisi na kwa usawa kwa makundi yote hususan wanawake ambao ni wazalishaji wakubwa wa chakula nchini. Malengo ya maadhimisho haya ni: kuimarisha, uwezo wa kuchambua, kutafiti na kutathimini masuala yahusuyo umiliki na usimamizi wa ardhi kwa wanawake, huduma za jamii; kupanua na kuimarisha ushirikiano katika vuguvugu la kuwakomboa wanawake na kuchangia katika mjadala wa utengenezaji wa tamko la kitaifa la madai ya wanawake ya ardhi ambayo yatakuwa ni sehemu ya tamko la kikanda la wanawake kuhusiana na masuala ya ardhi (Kilimanjaro Initiative). Maadhimisho yaliendeshwa pamoja na warsha na mijadala mbalimbali pamoja na tukio la upandaji wa mlima Uluguru kwa baadhi ya Wanawake ili kupaza sauti za wanawake juu ya madai ya haki ya umiliki na usimamizi wa ardhi kwa wanawake nchini Tanzania.  

GEWE KUTOKOMEZA KABISA UKATILI WA KIJNSIA

13 September 2016 Written by
Published in NEWS
Ukatili wa kijinsia ndani ya Wilaya ya Mvomero umepungua na unazidi kupungua siku hadi siku. Hayo yamebanishwa na wanakamati wa GEWE walipotembelewa na maofisa kutoka TAMWA. “Kwa kweli tunasema tena kwa kujiamini kuwa ukatili hapa kwetu mtibwa umepungua tena kwa kiasi kikubwa ukilingalisha na siku za nyuma, ila wanaofanya ukatili kwa sasa, wanafanya kwa kujificha chinichini maana wanaogopa kuwa tutawatumbua na kuwachukulia hatua”. Ni maneno ya mwanakamati Asha Shabani wakati akieleza mafanikio ya mradi wa GEWE. Mafanikio haya ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa kina mama, watoto na hata kwa wanaume yamekuja baada ya TAMWA kufanya mafunzo mapema mwezi Aprili mwaka huu (2016), Mafunzo yaliyolenga kujenga, kuimarisha usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto nchini (GEWE II) kwa kamati zake na waandishi wa habari kuachilia mbali ambayo yalifanyika miaka ya nyuma. Matokeo ya mradi wa GEWE yamezidi kuonekana na kuthibitika kwa wanakamati wa GEWE, wahanga wa ukatili na wananchi kwa ujumla kwani wamepata uwezo wa kuzungumza na vyombo vya habari bila kuwa na wasiwasi na kueleza matatizo na mafanikio wanayoyapata katika kutoa huduma kwa jamii na kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari. Willy Mtembela, mmoja wa wajumbe wa kamati ya GEWE kata ya Mtibwa anasema kuwa, wao kama kamati wanajivunia kwa utendaji wao kwani wameweza kutoa elimu ya ukatili sehemu mbalimbali ikiwemo mashuleni ambapo walienda wakiwa wameambatana na waandishi wa habari na kutoa elimu ya jinsia na ukatili kwa watoto mashuleni ambapo waligundua mengi yanayowasibu watoto wakiwa katika mazingira ya shuleni, njiani na hata nyumbani. GEWE II ni mradi unaotekelezwa na TAMWA na ulianzishwa kwa lengo la kujenga, kuimarisha usawa wa kijinsia, na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini katika wilaya 10 za Tanzania bara na visiwani Jumla ya watoa habari 120, wasaidizi wa sheria 120 na waragibishi 120, polisi, viongozi wa dini, afya walipewa mafunzo jinsi ya kushughulikia ukatili wa kijinsia na wanaendelea na zoezi la kuratibu shughuli hizo katika ngazi za Vijiji hadi Kata.

OUR YOUTUBE VIDEOS

Events - Calendar

November 2017
Mon Tue Wed Thu Fri Sat Sun
1
2
3
4
5
6
7
8
9
10
11
12
13
14
15
16
17
18
19
20
21
22
23
24
25
26
27
28
29
30

FOLLOW US ON FACEBOOK

JoomShaper