News/Stories

MTANDAO WA WADAU KUTOKA ASASI ZA KIRAIA UNAOTETEA MAREKEBISHO YA SHERIA NA SERA IHUSUYO USALAMA BARABARANI TANZANIA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Mtandao wa wadau kutoka Asasi za kiraia  unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzaniatunapenda kumpongeza  na kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr John Pombe Magufuli kwa kuguswa na kutoa maagizo kunapo kuwa na matukio ya ajali za barabarani yanayotokea nchini ambayo yamekuwa na athari nyingi  kiuchumi na kijamii.

 

Vilevile matukio haya ya ajali za barabarani yamekuwa yakiwasababishia wananchi madhara makubwa yakiwemo kupoteza maisha, majeraha makubwa, ulemavu wa kudumu, mali kuharibika ikiwa ni pamoja na kuacha familia nyingi zikiwa tegemezi baada ya kuondokewa na watu wanaowategemea.

Kwa pamoja tunaunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa hivi karibuni ambapo alitoa maagizo kwa vyombo vya usalama barabarani kufanya uchunguzi wa kina wa ajali iliyotokea katika kijiji cha Makomero, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora tarehe 04 Aprili, 2018.  Ajali hiyo ilitokea saa 2:00 usiku na kusababisha vifo vya watu 12 baada ya basi la kampuni ya City Boy lililokuwa limebeba abiria kutoka Karagwe kuelekea Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Singida.

Aidha, nalitaka Jeshi la Polisi, Kamati za ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Mamlaka zote zinazohusika na usalama Barabarani kujitathimini, na kutafuta majawabu ya kwa nini ajali za barabarani zinaendelea kutokea kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za barabarani”. Ilibainisha Sehemu ya tarifa hiyo ya ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa hivi karibuni ambapo alitoa maagizo ya Rais.

Pamoja na agizo la Mheshimiwa Rais, la kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama barabarani na mamlaka yake kutafuta majawabu kwa nini ajali zinaenaendelea kutokea nchini, sisi kama Taasisi za Kiraia kwa muda sasa tumekuwa pia tukijiuliza swali kwa nini ajali za barabarani  zimeendelea kutokea nchini?. Baada ya tathimini na tafiti mbalimbali tulipata jawabu kwamba, kuna haja ya kufanyia tena mapitio na kuboresha Sheria yetu ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973.

Kwa ujumla sheria hii ni imejitahidi kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto za  usalama barabarani isipokuwa utafiti uliofanyika unaonesha kuna mapungufu kadha wa kadha ambayo yanahitaji kufanyiwa maboresho ili yaendane na hali ya sasa na pia iweze kukabiliana kikamilifu na changamoto za ajali za barabarani pamoja na madhara yatokanayo na ajali hizo.

Maeneo ndani ya sheria ambayo tumependekeza yafanyiwe kazi ni pamoja na; mwendokasi, matumizi ya mikanda, kofia ngumu, matumizi ya vilevi na vizuizi vya watoto.

 

a)      Mwendo kasi (Speeding): Mwendokasi ndio unatajwa kuwa ndio chanzo kikuu cha ajali- “the faster the speed the greater impact in the crush”. 
 Kifungu cha 51(8)  cha Sheria yetu ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 inatamka mwendokasi maeneo ya makazi ni 50km/h, kwa maeneo mengine utadhibitiwa na alama za barabarani, na magari makubwa zaidi ya tani 3500 hayatazidisha 80km/h.

 

Mapungufu ya sheria ni kwamba inatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi. 

Tunapendekeza kuwa sheria itamke maeneo yote na si yale ya mjini tu/makazi, itamke wazi kuhusu maeneo ya shule, nyumba za ibada, maeneo ya michezo na mbuga za wanyama.

 

b)      Matumizi ya mikanda; Sheria ya sasa ya Usalama Barabarani inasema ni kosa kisheria kwa dereva na abiria anayekaa kiti cha mbele kutokufunga mkanda wakati wa safari lakini sheria hiyo hiyo haisemi chochote kwa abiria wanaokaa kiti cha nyuma.

 

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unasema kuwa iwapo ajali ikitokea madhara/athari kwa abiria wa kiti cha mbele itapungua kwa 50% na kwa abiria wa nyuma madhara yatapungua kwa 70%. Kanuni zilizotungwa na SUMATRA zinataka abiria wote wafunge mkanda ila kwa vile sheria mama (Road Traffic Act of 1973) ipo kimya katika eneo hili la utekelezaji wa kanuni unakuwa mgumu.

 

Hivyo basi ni pendekezo letu sheria hiyo ibadilishwe na kuwataka abiria wote wanaokuwa katika chombo cha usafiri wa kibiashara au binafsi kufunga mkanda wakati wote wa safari.

 

 

c)      Matumizi sahihi ya kofia ngumu; Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa ni kosa kwa muendesha pikipiki kutokuvaa kofia ngumu wakati wa kuendesha chombo hicho. Lakini sheria hiyohiyo haisemii chochote kwa abiria anayepanda katika chombo hicho.

Vilevile pamoja na kuanishisha kosa kwa dereva wa pikipiki kutovaa kofia ngumu lakini pia sheria haielezi ni jinsi gani kofia inatakiwa kuvaliwa na aina maalum ya kofia inayotakiwa kuvaliwa.

 

Kwa mujibu wa Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO)  unaonyesha kuwa iwapo ajali itatokea madhara yanayotokea kwa kutovaa kofia maalum na kwa usahihi ni makubwa sana ukilinganisha na kofia hiyo ikivaliwa kwa usahihi. Hivyo basi kwa kukizingatia kuwa sasa hivi usafiri wa pikipiki umekuwa unatumika kwa kiasi kikubwa (public transport), hivyo ni pendekezo letu sheria hiyo ifanyiwe maboresho na kuwekwa kuwa ni sheria kwa mtu yoyote anayepanda pikipiki kuvaa kofia ngumu na kwa usahihi.

 

 

d)     Matumizi ya vilevi na uendeshaji vyombo vya usafiri: Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa itakuwa kosa kwa mtu yoyote kuendesha chombo cha moto akiwa na kiwango cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08% katika mfumo wa mwili.

 

Kiwango hiki ni kikubwa sana kikilinganishwa na tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kupendekeza kiwango cha asilimia 0.05% kwa dereva aliyebobea (experienced driver) na asilimia 0.02% kwa dereva  mchanga (young driver). Hivyo basi ni pendekezo letu kuwa sheria ifanyiwe marekebisho ili iendane na kiwango cha sasa cha kimataifa kilichofanyiwa utafiti.

 

Tunatoa wito kwa  serikali na watunga sera kutaka kujishughulisha zaidi na wadau katika kuuelimisha umma zaidi katika eneo la uhusiano wa adhabu zitokanazo na makosa ya usalama barabarani na ongezeko la ajali. Pia sheria kufanyiwa maboresho na kuangalia upya kwa mianya iliyopo.

 

Hata hivyo Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani wanakiri kwamba sheria  madhubuti zinahitajika katika kupunguza idadi ya watu wanaofariki katika barabara zetu, na Tanzania lazima tuwe na sheria kali za usalama barabarani kukomesha hali hii .

 

Lakini pia kwa muda wa miaka minne iliyopita, karibia nchi 17 zinazowakilisha wananchi milioni 409 zimetunga na kufanyia maboresho ya sheria angalau kwa kiashiria kimoja au zaidi ambavyo vimekuwa ndio vyanzo vikubwa vya ajali na nchi hizo zimekuwa zikifanya vizuri katika kudhibiti ajali, ila Tanzania haipo miongoni mwa nchi hizo. Ni mda mwafaka sasa kwa Tanzania kuchua hatua kwa vitendo.  #AJALISASABASI

 

TAMKO HILI LIMETOLEWA LEO NA MTANDAO WA WADAU KUTOKA ASASI ZA KIRAIA:

1.       TAWLA

2.       TAMWA

3.       WLAC

4.       TCRF

5.       TLS

6.       TMF

7.       RSA

8.       AMEND TANZANIA

9.       SHIVYAWATA

10.    TABOA &

11.    SAFE SPEED FOUNDATION

Latest News and Stories

Search