News/Stories

TAMWA YALAANI MAUAJI YANAYOENDELEA KWENYE NDOA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

 Chama cha Wanahabari Wanawake nchini – TAMWA kimefadhaishwa na kinalaani vikali vitendo vya mauaji vinavyoendelea kutekelezwa na baadhi ya wanandoa kwa makusudi na kuwanyima haki ya kuishi wenza wao kwa kuwaua  kinyama kwa sababu ya wivu wa mapenzi. 

 

 Matukio hayo ya mauaji hivi karibuni yamewahusu kwa Mhadhiri wa chuo kikuu cha Dodoma (Udom) Rose Malfred (31), mkazi wa Swaswa aliyeuwawa kikatili na mumewe ambaye inadaiwa kuwa ni Mchungaji wa kanisa la TAG John Mwaisango, kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali za mwili hadi kufa.

 Tukio jingine ni lile la kuuawa kinyama kwa Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Rosemary Mgombela, kisha mwili wake kufukiwa pembeni mwa nyumba, tukio ambalo Shangazi wa marehemu Veronica Mapunda alisimulia akimshuku mume wa marehemu huyo kuhusika kutokana na malalamiko aliyokuwa anayapata kutoka kwa marehemu kuwa hawaelewani.

 Aidha tukio jingine ni lile la mfanyabiashara wa samaki mkazi wa mtaa wa Mahakama wilayani Ilemela, Nicholas Light (25) ambaye alimuua mpenzi wake, Victoria Swai (26) kwa kumnyonga na kumkaba shingo kwa wivu wa mapenzi

 Matukio haya ya mauaji ni miongoni mwa matukio mengi ya mwaka huu 2018 ambayo baadhi ya wanandoa wameamua kujichukulia sheria mikononi na kukatisha maisha ya wenza wao  kisha kukimbia na kuacha sintofahamu kwa familia na jamii kwa ujumla

TAMWA inalaani vikali visa na mikasa hii na kuomba jeshi la polisi kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha waliohusika wanatiwa hatiani na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inaeleza bayana haki ya kuishi kwa kila raia Ibara ya 14 ya Katiba hiyo imeeleza kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kupata  kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.Vilevile katika Ibara ya 15  Ibara ndogo ya kwanza ya Katiba hiyo imetamka kwamba, kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.

 Suala la uhuru wa Kuishi, si la Katiba peke yake bali hata Sheria nyingine hasa ile sheria ya Kanuni ya adhabu sura namba 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, imeweka adhabu kali kwa kila mtu ambaye atakatisha maisha ya mtu mwingine/kuua kwa makusudi/ Kukusudia

 Kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu (Sura namba 16 kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kimetamka kuwa itakuwa ni kosa kwa mtu kukatisha maisha ya mtu/ kwa makusudi wakati kifungu cha 197 cha sheria hiyo hiyo kimeweka adhabu ya kunyongwa hadi kufa mtu atakayepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia

 Aidha, TAMWA inadai sheria ichukue mkondo wake tena kwa haraka ili liwe fundisho kwa wanaoendelea kufanya ukatili wa kinyama na kukatisha maisha ya wenza ambao ndiyo wazalishaji na walezi wakuu wa familia.

 Takwimu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kupitia Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa kwa gazeti la Habari Leo mwaka jana 2017, kwa, mwaka 2016 kulikuwa na mauaji 151 baina ya wanandoa.

 Mwaka jana 2017 mauaji hayo yaliongezeka na kufikia 163 ambayo ni nyongeza ya mauaji 12 sawa na asilimia 7.9.

 Mikoa mingine iliyofuata kwa wingi wa matukio ya wanandoa kuua wenza wao na idadi kwenye mabano ni Geita (25), Mwanza (21), Kagera (20) Mbeya 19 na Shinyanga (18).

 

Edda Sanga

Mkurugenzi Mtendaji.

Latest News and Stories

Search