News/Stories

TAMWA YAUNGANA NA WA MASHIRIKA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Chama cha Wanahabari Wanawake –TAMWA, kinaungana na mashirika mengine yanayopinga ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu kote nchini kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa tarehe 16 Juni kila mwaka.

Maadhimisho hayo ambayo yatafanyika wilayani Ilala Kata ya kivule leo tarehe 14 Juni, 2018 kuanzia saa tatu Asubuhi hadi saa tano katika viwanja vya stendi ya Mbondole, Mgeni rasmi ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Sophia Mjema ambapo kauli mbiu mwaka huu ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Tusimwache Mtoto Nyuma’’ inamlenga kila mzazi, mlezi, ndugu, jamaa, jirani na rafiki kumpenda mtoto kwa namna yoyote ile, kuhakikisha anatunzwa vizuri na haki zake zinalindwa ipasavyo ili atimize ndoto zake. 

 

Takwimu za Shirika la Hali ya Afya na Uzazi  (TDHS) mwaka 2015 -16 zinaonyesha idadi ya wasichana wanaopata watoto katika umri wa miaka 15-19 imeongezeka mpaka kufikia asilimia 27 mwaka 2015 kutoka asilimia 23 mwaka 2010, hali ambayo inaonyesha watoto hawa wanaopaswa kuwa shule badala yake wamepata watoto wakiwa na umri mdogo wakakatisha masomo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na UNICEF mwaka 2015, Tanzania ina asilimia 3.5 ya watoto wenye umri wa miaka 7-17 walio nje ya shule, hii inajumuisha watoto takriban milioni 2 waliotakiwa kuwa shule za msingi na watoto takriban milioni 1.5 waliotakiwa kuwa shule za sekondari.

Takwimu za Jeshi la polisi nchini kupitia kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Boaz mwakajana 2017 zinaonyesha makosa ya ubakaji  na kunajisi yameongezeka kutoka 6,985 yaliyoripotiwa mwaka 2016 mpaka makosa 7,460 mwakajana 2017.

Takwimu pia zinaonyesha makosa hayo ni ongezeko la makosa 478 sawa na asilimia 6.8 wakati makosa ya kunajisi mwaka 2016 yalikuwa 16 ikilinganishwa na makosa 25 mwaka jana 2017 kufanya ongezeko la makosa 9 sawa na asilimia 56.3. Takwimu hizi ni kwa yale makosa ambayo yameripotiwa tu. Ina maana yako mengi pia ambayo hayaripotiwi.

Utandawazi umekuwa ni changamoto kubwa kwa watoto kwani wazazi wameacha majukumu yao ya kuwalinda na kuwalea ipasavyo na badala yake wanakimbizana na maisha wakiwaacha watoto wajilee au kulelewa na majirani. Huu ni utelekezaji wa majukumu yetu katika kuandaa taifa la kesho.

Mbali na hilo hata walezi, ndugu wa karibu na walimu wa shule ambao wamekuwa wakitegemewa na wazazi kwa kuwa ndiyo wanakuwa na watoto muda mwingi wamekuwa ni changamoto kubwa kwa  vile nao badala ya kuwa viongozi na walinzi wamekiuka haki za watoto kwa kuwapa mimba, kuwapiga na kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji, udhalilishaji hata mauaji.

Hali hii inakiuka haki za mtoto ambapo inatutaka kwa pamoja tumlinde mtoto, na tuweke mikakati ya kuzuia na kutokomeza ukatili kwa watoto.  Serikali kwa kushirikiana na wadau ilizindua Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto mwishoni mwa mwaka 2016 ambao umelenga kupunguza ukatili wa watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/22

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa tarehe 16/06 kila mwaka. Siku hii ilirasimishwa na OAU (organization of Africa Unit), tangu mwaka 1991 ili kuwapa heshima watoto wale ambao walishiriki maandamano ya Soweto mwaka 1976.

Katika maandamano hayo, zaidi ya watoto 10,000 walioshirikiki waliuwawa na wengine walijeruhiwa. Haya yaliwakuta wakiwa katika harakati za kutetea haki zao, miongoni mwa hayo ni elimu bora na yenye kukidhi mahitaji na matakwa yao.

Edda Sanga,

 

Mkurugenzi Mtendaji.

Latest News and Stories

Search