News/Stories

TAMWA YALAANI UKATILI NA MAUAJI YANAYOFANYWA NA WAALIMU KWA WANAFUNZI

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Chama cha Wanahabari Wanawake nchini – TAMWA kimesikitishwa na kulaani vitendo na matukio ya ukatili uliopindukia unaofanywa na baadhi ya walimu kuwapiga wanafunzi bila kufuata sheria zinavyoelekeza na kupelekea baadhi yao kuathirika kisaikolojia na hata kupoteza maisha kutokana na vipigo hivyo.

Miongoni mwa matukio ya kusikitisha ni lile la tarehe 27 Agost ambapo MWANAFUNZI wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta, Bukoba mkoani Kagera, Sperius Eradius (13) alifariki dunia baada ya kupigwa na mwalimu wake kwa kutuhumiwa kuiba pochi ya mwalimu.

Tukio jingine ni lile la mwaka 2016 lililotokea kwa msichana wa kidato cha Nne (17) aliyekuwa akisoma katika shule moja ya Sekondari ya Kata mkoani Mbeya ambaye alivuliwa nguo zake za ndani na kucharazwa bakora zisizo na idadi kwa sababu za utoro shuleni, adhabu iliyotolewa na walimu wanne wa shule hiyo akiwemo Mkuu wa shule hiyo.

Tukio hilo ambalo limeripotiwa katika kituo kidogo cha  Polisi Mbalizi wilaya ya Mbeya kwenye jalada la uchunguzi namba MBI/IR/967/2016 na kuwekwa kwenye taarifa yenye namba MBI/RB/2653/2016.

Aidha katika tukio jingine mwanafunzi wa shule moja ya Sekondari ya Kutwa mkoani Mbeya, walimu walimkamata mikono mwanafunzi na kumwangusha chini kisha kumpiga kwa makofi, ngumi, mateke na fimbo huku mmoja wao akionekana kumpiga kichwani mithili ya mtu anayeua nyoka kwa fimbo. Mwanafunzi huyo inadaiwa alipewa adhabu hiyo baada ya kufanya kosa la kuonesha kiburi alipotakiwa kupiga magoti ikiwa ni adhabu ya kutofanya zoezi la Kiingereza alilopewa na mwalimu wake.

SherIa juu ya viboko mashuleni katika Kifungu cha 61(1)(v) Cha Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002, kinampa mamlaka waziri wa Elimu kutunga kanuni za masuala mbalimbali zitakayokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo. 

Mojawapo ya kanuni zilizotungwa ni The Education (Corporal Punishmemt ) Regulation G.N.294 ya mwaka 2002.Kanuni hizi zinatoa mwongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani Kanuni ya 3(1) inasema athabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhabu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule amabalo litailetea/ litaishushia shule heshima.

Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itolewe kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko 4 kwa tukio lolote. Nani Ana mamlaka ya kumchapa mwafunzi.
Sheria inamtaka mwalimu mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo. Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.

TAMWA inalaani kwa nguvu ukatili wa aina hii na ni matarajio yetu kuwa vipigo na mauaji mashuleni havitatokea tena. Aidha tunamshukuru na kumuunga mkono Waziri wa Elimu, Sayansi, Technologia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako kwa kukemea vitendo hivi kwa wanafunzi pamoja na viongozi wenye mamlaka kuchukua hatua katika matukio haya ambayo yanarudisha nyuma na kukatisha ndoto za wanafunzi, familia zao na hata kudhalilisha Taifa letu.

 Edda Sanga,

Mkurugenzi Mtendaji

Latest News and Stories

Search