News/Stories

TAMWA YAPONGEZA WABUNGE WANAWAKE KUCHANGISHA FEDHA KUJENGA VYOO VYA WATOTO WA KIKE NCHINI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Chama cha Wanahabari Wanawake - TAMWA kimefurahishwa na kinazidi kuupongeza Umoja wa Wabunge Wanawake nchini kwa juhudi ambazo unaendelea kuonyesha kutafuta kiasi cha Sh.3.2bilioni za kujenga vyoo vya mfano kwa wanafunzi wasichana na wenye mahitaji maalumu katika majimbo 264 ya uchaguzi nchini.

 

Wabunge wanawake hao wamefanikiwa kuchangisha Sh. 800milioni ambazo zimepatikana katika hafla iliyoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa vyoo hivyo vya mfano iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam  Agosti 31, 2018, mpaka sasa fedha zilizopatikana ni Sh. 2.3bilioni na zinazohitajika ni Sh. 3.2bilioni.

Dhamira hii njema ya Wabunge Wanawake imetokana na changamoto zinazoendelea kuwakabili wanafunzi kukosa vyoo bora na maji salama na safi shuleni. Tatizo hili linawaathiri watoto wa kike zaidi  kwani wanashindwa kujistiri hasa wanapokuwa katika siku zao za hedhi katika mazingira ya shuleni.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya hafla hiyo Mhe. Anna Tibaijuka, amesema wapo Wabunge waliotoa fedha taslimu na wengine wametoa vifaa mbalimbali vya ujenzi huku mbunge wa Chalinze (CCM) Ridhiwan Kikwete akijitolea kujenga vyoo hivyo katika jimbo la Bagamoyo na Chalinze.

Aidha Mwenyekiti wa Umoja huo wa wanawake, Magreth Sitta amewaomba wananchi pia kuongeza ushirikiano na kuchangia ili kuweza kujenga vyoo hivyo vya mfano katika majimbo 264 ya Tanzania, pia amebainisha kuwa gharama za ujenzi wa choo kimoja ni Shilingi milioni moja.

Katika hafla ya uchangishaji wa fedha hizo vitu mbalimbali viliuzwa zikiwemo picha za waasisi wa Taifa na za kupamba majumbani.  Aidha kiingilio katika ukumbi wa hafla hiyo  kilikuwa ni shilling 100,000/- ambacho kilikuwa ni njia mojawapo ya ukusanyaji mapato kwa lengo hilo.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria katika hafla hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama; Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako; Spika wa Bunge, Job Ndugai; Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai na Spika mstaafu Anne Makinda ambaye alikuwa mgeni rasmi, akimuwakilisha Rais John Magufuli.

TAMWA inaamini kuwa kiasi cha fedha zilizopatikana ni chachu katika kuhakikisha mtoto wa kike anawekewa mzingira rafiki anapokuwa shuleni ili aweze kuhudhuria masomo yake kwa ukamilifu kama ilivyokuwa kwa mtoto wa kiume kwani “Ukimkomboa mtoto wa kike umekomboa Taifa zima”.

Tafiti zinaonesha kuwa mtoto wa kike anakosa masomo siku 4 hadi 5 kila mwezi kutokana na ukosefu wa huduma ya vyoo bora na maji salama na safi shuleni ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Miongoni mwa malengo hayo ni lile lengo namba 4: linalohamasisha kuhusu Elimu Bora, Lengo la 5: linalo hamasisha juu ya Usawa wa Kijinsi na lengo namba 6: kuhusu Maji Safi na Salama.

Edda Sanga

Mkurugenzi Mtendaji

Latest News and Stories

Search