Press Release

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
 
WAJIBIKA KULINDA UTU WA MWANAMKE UPATE KURA YAKE
01/09/2020
Wanamtandao wa Katiba, Uchaguzi na Uongozi ambao ni watetezi wa haki za wanawake na wasichana, yakiwemo masuala ya kukuza ushiriki wao katika uongozi wa kisiasa,    na pia tukiwa ni  wadau wakuu wa uchaguzi kama wapiga kura na wagombea katika nafasi mbalimbali za uchaguzi. Tumekuwa  tukifuatilia  kwa ukaribu mkubwa sana mchakato mzima wa uchaguzi tangu ulipoanza na matukio mbalimbali ambayo tayari yameshajitokeza ikiwemo utumiaji wa lugha za matusi na kauli mbaya za udhalilishaji dhidi ya wanawake wanaogombea na wafuasi wa vyama kwa ujumla. Kwa mfano, kumekuwepo na lugha za kutukana Wanawake wagombea wakiitwa “Malaya”, n.k 
 
Ni vema tutambue kwamba kasumba hii mbali na kwamba ni kinyume na haki za binadamu na ni kosa kisheria, inarudisha nyuma jitihada za serikali katika kufikia usawa wa kijinsia na kurudisha nyuma ari ya wanawake wengi kugombea nafasi za uongozi kwa sababu ya kuogopa kudhalilishwa. Halikadhalika,  inanyamazisha sauti za wanawake ambao ni zaidi ya nusu ya watanzania wote ambao ni wapiga kura wakuu na ambao wanahaki ya ushirki salama katika masuala ya kisiasa, suala ambalo halina tija kwa taifa letu. Kutokana na hali hii, tunaona umuhimu wa vyombo na mamlaka zinavyohusika kuwawajibisha kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi kwa wote wanaotumia matusi na lugha za kudhalilisha wanawake.
 
 Sisi, Wanamtandao watetezi wa haki za wanawake nchini, tunachukulia matukio haya kama kuvunjwa kwa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), inayokataza ubaguzi wa aina yoyote, na  tunaikumbusha jamii  kwamba Kanuni ya Makosa ya Adhabu, Sura ya 16, kifungu cha 89 kinataja kutumia lugha chafu dhidi ya mtu mwingine kuwa ni kosa la jinai. 
 
Tunaomba Umma wa Watanzania na Vyombo mbalimbali vinavyosimamia uchaguzi wa taifa hili utambua kwamba, ushiriki wa wanawake katika michakato ya uchaguzi ni haki yao ya kikatiba, na zimebainishwa katika sheria mbalimbali za nchi. 
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi huweka  wazi Kanuni mbalimbali za uchaguzi na Maadili ya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kwa  lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa Watanzania wote, wakike na wakiume, kushiriki katika mchakato huu wa uchaguzi na kutoa mchango wao, kwa uhuru, uwazi na amani. Vile vile, Sheria ya Vyama vya Siasa, iliyorekebishwa mwaka 2018, katika kifungu chake cha 9, inakataza viongozi na wanachama wake kutamka au kutumia lugha za matusi, maneno ya kudhalilisha, uchochezi, au alama ambazo zinaweza kusababisha au kuhatarisha amani na ukosefu wa umoja wa kitaifa.
 
 Vilevile  Kanuni za  maadili ya Uchaguzi zilizotolewa katika Gazeti la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania la tarehe 5/06/2020 zimebainisha mambo yaliyokatazwa kufanywa na vyama vya siasa kifungu ca 2.2 (b)  kinakataza kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjfu wa amani au kuashiria ubaguzi wa jinsia, ulemavu, rangi au maumbile kwenye mikutano na kwenye shughuli zote za kampeni.
 
Kwa kuzingatia hili katazo, na kwa kuzingatia haki zetu za kikatiba na sheria za nchi, Sisi kama watetezi wa  haki za wanawake na usawa wa kijinsia hapa nchini, tunataka yafuatayo yazingatiwe ili kutokomeza udhalilishaji wa wanawake hasa kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu: 
Tunazitaka mamlaka zinazohusika (Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama Vya Siasa, na Taasisi nyingine husika kuwachukulia hatua kali kwa wagombea, pamoja na wapambe wao, wanaotoa lugha za kudhallisha na kutukana wanawake kwenye kampeni au mahali popote wakati huu wa uchaguzi m
Tunawataka viongozi wa taasisi mbalimbali zikiwemo za dini, na hasa vyama vya siasa, Asasi za Kiaraia, na Jamii yote kwa ujumla ya Tanzania kukemea vikali tabia hizi za kudhalilisha wanawake hasa kipindi hiki cha uchaguzi.
 
Vyama vya Siasa vitambue kwamba vina wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha haki na usawa wa Wanawake ndani ya vyama vyao na katika jamii kwa ujumla, kwa kuwa Wanawake ndiyo kundi kubwa la wapiga kura Tanzania. Kwahiyo lazima viheshimu UTU wa mwanamke  na kutoa fursa na kuweka mazingira yaliyo ya wazi na wezeshi ili wanawake wengi washiriki kikamilifu katika kutimiza haki yao ya kikatiba kama wagombea  na wapiga kura.
 
Mwisho na siyo kwa daraja, sisi wanawake wote kwa ujumla wetu, bila kujali Imani za kiitikadi, tukemee, tukatae na kuwajibisha wale wote wenye kutudhalilisha kwa njia yoyote ile, ikiwa ni pamoja na kututukana  
 
Tunawataka wanahabari na vyombo vya Habari kutumia taaluma yao vizuri kutetea UTU, HAKI ya mwanamke na hususani kipindi hiki cha uchaguzi. Vyombo vya Habari visishiriki katika kusambaza taarifa zenye lugha za matusi na udahlili zilizodhamiria katika kumdalilisha mwanamke wa Taifa hili.
 
 
Tamko hili la kukemea lugha za matusi dhidi ya wanawake ni mwendelezo wa matamko ambayo Wanamtandao tumeshayatoa tangu uchaguzi huu uanze. TUNALAANI NA KUKEMEA KWA NGUVU ZOTE MATUMIZI YA LUGHA ZA MATUSI, LUGHA ZA KEJELI, UDHALILISHAJI,  KATIKA KIPINDI CHOTE CHA UCHAGUZI
 
 
Imetolewa leo Septemba 1, 2020
Mtandao wa Wanawake Katiba Uchaguzi na Uongozi.

Search