Press Release

TAMWA kufanya tathmini ya rushwa ya ngono ndani ya vyombo vya habari

User Rating: 3 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar InactiveStar Inactive
 

Dar Es Salaam , Oktoba 2, 2020.

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) tunachukua fursa hii, kuutambulisha kwenu mradi wa “Rushwa ya ngono miongoni wanahabari wanawake katika vyombo vya habari” unaofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania - Women Fund Tanzania (WFT).

TAMWA ilianzishwa 1987, na wanahabari wanawake, kwa lengo la utetezi wa ustawi wa haki za wanawake na watoto kupitia taaluma yao na vyombo vya habari.

“Kwa kuwa TAMWA kiini chake ni wanahabari,  hivyo basi jukumu la utekelezaji wa mradi huu, unaowalenga wanahabari litakwenda kutekelezwa kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na nyinyi wanahabari na vyombo vya habari,” Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA.

TAMWA tunakwenda kuutekeleza mradi huu tukifahamu kabisa kuwa zipo tafiti mbalimbali zinazoonyesha kuwa bado kuna rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari.

“Wakati huo huo, wanahabari wameonekana kuwa kimya kuhusu matukio hayo, aidha kwa kuogopa kupoteza ajira zao au pengine wakichelea kuaibika zaidi pindi watakapoweka wazi masahibu yao,” Reuben

Kimsingi, rushwa ya ngono haikubaliki na ni tabia isiyopendeza inayoshusha utu na kuwafanya waathirika kudhalilika, kupata msongo wa mawazo na kukosa kujiamini mahala pa kazi, lakini baya zaidi ni kuwa matukio mengi hayaripotiwi.

Baadhi ya watafiti, kama Barton A na Storm, (2014) walibaini kuwa asilimia 48 ya wanahabari wanawake waliohojiwa walikiri kuwa wamewahi kukumbana na  rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari kwa namna moja au nyingine na asilimia 83 kati ya hao, walisema hawakuripoti matukio hayo.

“Ombwe hili ni kubwa na huenda likawaathiri hata wanahabari wachanga walio vyuoni, ambao huenda wakakataa tamaa ya kuingia katika tasnia hii na hivyo kuizorotesha tasnia lakini baya zaidi, kukosa wanahabari wanawake katika nafasi za juu za uongozi na wenye mafanikio katika tasnia hiyo,”Reuben

Kadhalika, imebainika kuwa vyombo vyingi vya habari nchini havina sera madhubuti zilizowekwa kuwaongoza wanahabari katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinapowakumba ikiwamo masuala ya rushwa ya ngono katika mazingira ya kazi   na  hivyo kuchangia kuongezeka kwa visa vya rushwa ya ngono.

“Hivyo basi, kukiwa na ombwe kama hilo, TAMWA katika utekelezaji wa mradi huu, itafanya tathmini kwa kupitia maswali, ili kujua yanayowasibu wanahabari” Reuben

Kadhalika, TAMWA itawajengea uwezo wanahabari, wakiwamo wahariri na wanawake wanahabari walio katika vyombo vya habari.

Kisha, TAMWA itashirikiana na vyombo vya habari kufanya uchechemuzi, kufanya mazungumzo  na wamiliki wa vyombo vya habari ili kuwashirikisha matokeo ya tathmini na kuelimisha jamii kuhusu rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya Habari na kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Katika mradi huo TAMWA itashirikisha wadau mbalimbali  wa habari wakiwamo, MISA, TEF, MCT, TCRA na OSHA.

Mradi huo utatekelezwa jijini Dar es salaam ambapo ni kitovu cha vyombo vyingi vya habari nchini zikiwamo Redio, Runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.

TAMWA inaamini kuwa kwa kufanya tathimini ya rushwa ya ngono katika vyombo vya habari na kuwajengea kuwajengea uwezo wanahabari, itawawezesha pia kufichua na kuandika vyema habari zinazohusu rushwa hii ambayo kwa mujibu wa mila na desturi za watanzania walio wengi imekuwa ikizungumzwa kwa kwa kificho au kutokuzungumzwa kabisa.

TAMWA inatambua kuwa uwepowa Sheria ya Rushwa ya ngono ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)

Lakini zaidi hasa, tunataka wanahabari wapaze sauti zao, tuvunje ukimya, wayazungumze yanayowasibu, na kuondoa kabisa ukatili wa kijinsia wa aina hii ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya tasnia ya habari ikiwa ni pamoja na kuua vipaji.

Pasipo kuvunja ukimya uliotanda dhidi ya suala la rushwa ya ngono, waathirika kujengewa uwezo wa kukusanya vidhibiti visivyokuwa na mashaka yoyote taasisi yenye mamlaka ya kushughulikia makosa haya haziwezi kufanya kazi yake kwa ufasaha na kuleta mabadiliko katika jamii yetu.

Kadhalika serikali, taasisi za habari na za jinsia, zinatakiwa kushirikiana kumaliza tatizo hili ambalo halijazungumzwa kwa kina ili tuvunje ukimya huu.

Mkurugenzi Mtendaji

Rose Reuben

TAMWA

Search