Press Release

TAMWA yalaani matukio ya ubakaji wa watoto yanayoendelea nchini

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Dar es Salaam, Novemba 12, 2020. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinalaani vikali, matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea hapa nchini katika kipindi cha miezi miwili.

Hivi karibuni, vyombo vya habari vimeripoti matukio kadhaa ya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji wa watoto yanayoashiria kuwa bado vitendo hivi vinaendelea licha ya kuwepo sheria, matamko na sera zinazopinga vikali matukio hayo.

Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na lile la Novemba 11, mwaka huu, ambapo  Mwenyekiti wa Kijiji cha Ijinga, Wilaya ya Magu, Badri  Masengo (40) anayedaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita,Shule ya Msingi Ijinga mwenye umri wa miaka 15 .

 

Tukio jingine ni lile la mtoto wa miaka 6, wa shule ya msingi Themi, jijini Arusha, aliyebakwa hadi kufa, mnamo Julai mwaka huu.

Wakati huo huo, mtoto wa miaka 12, wilayani Serengeti, alibakwa na kujeruhiwa vibaya mnamo Januari 12, 2020.

Kadhalika tukio jingine kama hilo ni lile la kubakwa kwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Monfort, (10) aliyebakwa na mwalimu wake, (27) Anderson Eneza, mnamo Novemba 11, 2020.

Tukio jingine ni lile la Medadi Chitezi(60) mkazi wa kijiji cha Ulumi, Rukwa, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 10. Chitezi alifanya kosa hilo Agosti, 12, 2020.

Huko visiwani Zanzibar, limeripotiwa tukio la Mzee wa miaka 60, Haroub Abdallah Hamad, anayedaiwa kumbaka mtoto wa miaka mitano. Tukio hilo limetokea Oktoba 10, 2020, wilayani Wete, Pemba.

Kwa matukio haya na mengine ambayo hayajaripotiwa, ni dhahiri kuwa bado matukio haya yanaendelea hapa nchini, licha ya sheria zinazopinga na kutoa adhabu kali katika matukio hayo.

Hivyo basi, TAMWA ambayo miongoni mwa malengo yake makuu ni kuzuia na kupunguza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, inalaani vikali kuendelea kwa matukio hayo katika jamii.

“Watoto wana haki ya kulindwa na kuishi kwa furaha, kama binadamu wengine na kibaya zaidi ni kuwa watoto wanabakwa wengine wanapoteza maisha kutokana na kufanyiwa ukatili, kujeruhiwa na kuathirika kisaikolojia hata kuharibiwa mustakabali wa maisha yao,” Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben.

Ripoti ya Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) 2017, imeeleza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2016, ziliripotiwa kesi, 10, 551 za uhalifu dhidi ya watoto, huku kesi za ubakaji zikiripotiwa kuwa nyingi zaidi 4423.

Kwa mujibu wa kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 Mtoto ni mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 18. Sheria hii ya mtoto inakataza ubaguzi na ukatili wa aina yeyote dhidi ya watoto.

TAMWA tunaiomba serikali kuendelea na vita hii dhidi ya ubakaji hasa wa watoto, kwani hiki ni kizazi kijacho chenye manufaa tarajiwa katika ujenzi wa nchi yetu.

“Vita hii si ya serikali peke yake, bali na hata wadau wengine wote wa masuala ya ukatili wa jinsia na wa watoto, nia ikiwa ni kupunguza na kuzuia kabisa vitendo vya ukatili kwa watoto,” Reuben, TAMWA.

Hata hivyo tunaipongeza serikali na mahakama kwa kusimamia kesi za ubakaji kwa umahiri, kwa mfano zipo kesi za ubakaji wa watoto ambazo zimefanyiwa kazi kwa kipindi kifupi na kutolewa hukumu.

Kadhalika, zipo kesi za ubakaji ambazo zimefikishwa mahakamani na zinafanyiwa kazi kwa bidii na maofisa usalama.

Pia tunaona dhahiri kuwa, TAMWA na wadau wengine wa masuala ya ukatili tukiwa tumefanikiwa kwa kuwezesha matukio haya kuripotiwa kwa uwazi badala ya kufanywa siri au kumalizwa kifamilia kama ilivyokuwa zamani.

“TAMWA tunaendelea kusisitiza uwazi na uwajibikaji katika kuripoti masuala ya ubakaji wa watoto. Kila mmoja atimize wajibu wake, familia, jamii, na watoto wenyewe wafundishwe kuvunja ukimya na wadau watumie nafasi walizonazo katika kuhakikisha ubakaji huu unamalizwa, serikali nayo itemize wajibu wake kisheria na katika usimamizi wa kesi za ubakaji kwa wakati” Reuben, TAMWA.

TAMWA tunasema:  “Tujitolee, tuuzuie, tuwajibike na tuukatae ukatili wa aina hii.”

Rose Reuben.

Mkurugenzi Mtendaji,

TAMWA.

Search