Press Release

HONGERA MHESHIMIWA RAIS SAMIA SULUHU

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Dar Es Salaam, Machi, 19, 2021. Bodi ya wanachama, wanachama na Sekretariati ya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa Makamu wa Rais, ameapishwa leo, Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Hayati Rais John Magufuli ikiwa ni utekelezaji wa hatua za kikatiba na kisheria inayoeleza kuwa, Makamu wa Rais ataapishwa kuwa Rais, endapo Rais aliyeko madarakani atafariki dunia. 
 
TAMWA tunampongeza Rais huyu wa awamu ya sita, tukiamini kuwa ni kiongozi amestahili, makini na  anayekwenda kusimamia maadili, kusimamia katiba na kuzisimamia haki za wanawake na watoto. 
 
Tunaamini Rais wetu mpya ni muumini wa usawa wa kijinsia na hivyo atakwenda kuwa mstari wa mbele kusimamia sheria na haki zinazolinda watu wote, ikiwa ni pamoja na mwanamke hakika hatuna shaka na utendaji wake, TAMWA inaamini   ‘Wanawake Wanaweza  na sio kwa kuwezeshwa pekee bali waliaminika tangu enzi kwa kupewa madaraka ya kuwa  wasimamizi wakuu wa familia, kuanzia ngazi ya malezi,  jambo ambalo linawafanya kuwa imara, wanyenyekevu, wavumilivu na makini  zaidi hata katika nafasi za kisiasa na uongozi katika maeneo mengine.
 
Tangu akiwa Makamu wa Rais, amekuwa chachu kwa watoto wa kike na wanawake wa Tanzania katika kuwaza makubwa kwenye kuleta mabadiliko katika jamii ya kijinsia.
 
Hatuna  shaka na  utendaji kazi wa Rais wetu mpya na  historia yake ya kufanya kazi katika taasisi zisizo za kiserikali, kwa zaidi ya miaka kumi ambapo alijikita zaidi katika harakati za usawa kijinsia. 
Hivyo basi tunaamini kuwa atakwenda kusimamia ajenda hizo akiwa anaelewa kwa kina umuhimu wa usawa wa kijinsia na umuhimu wa kumaliza ukatili wa kijinsia,
 
Rais Samia Suluhu Hassan ameweka historia Afrika Mashariki  kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais, jambo ambalo  litaacha alama kwa vizazi vijavyo na kisha kuulinda  na kuuheshimisha mfumo wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi. 
Wakati tukiendelea kuomboleza msiba wa Hayati Rais John Magufuli, TAMWA ina imani kuwa, Rais Mama Samia Suluhu ataendelea kusimamia kauli yake  ile ya kuitaka jamii  kupinga na kupambana na vitendo vya ukatili katika maeneno yao.
 
Hongera Rais Samia Suluhu Hassan! Hongera Tanzania!
 
Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji,
TAMWA.

Search