Press Release

TAARIFA YA KUKANUSHA HABARI ILIYOANDIKWA NA GAZETI LA JAMHURI JULAI 20, 2021.

User Rating: 3 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar InactiveStar Inactive
 
Dar Es Salaam, Julai 20, 2021.
Leo Julai 20, gazeti la Jamhuri, linalotolewa kila wiki, katika ukurasa wake wa kwanza na kuendelea ukurasa wa tatu limeandika habari yenye kichwa  kinachosema: Mambo ya Nje haijamchukulia hatua Balozi".
Katika habari hiyo, inayomtuhumu Balozi wa Libya nchini Tanzania, Bwana Kamal Ramadan Krista kuhusika katika usafirishaji haramu wa wasichana na unyanyasaji wa kingono, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dk Rose Reuben amenukuliwa akisema kuwa: Sina maoni yoyote kwa sababu habari hii haikufanyiwa uchunguzi wa kutosha
Taarifa hiyo ikaeleza zaidi kuwa Dk Rose“Alipoelezwa kuwa suala hilo ni la kukiukwa kwa haki za watoto wa kike na kusafirishwa nje ya nchi kinyume na sheria huku TAMWA ikijipambanua kuwa watetezi wa haki za wanawake, alishauri watafutwe Polisi wa Kimataifa(Interpol) na Idara ya Uhamiaji. 
Aya ya mwisho ya habari hiyo imesema: Mkurugenzi huyo ameonyesha kutofurahishwa na gazeti la Jamhuri kuandika tuhuma dhidi ya mwanadiplomasia huyo.
Mkurugenzi wa TAMWA anakiri kupigiwa simu na kutembelewa na mwandishi wa Habari wa gazeti hilo Bwana Alex Kizenga tarehe 16 Julai mwaka huu majira ya mchana ambako alihitaji maoni dhidi ya Habari iliyochapishwa katika gazeti hilo wiki tatu nyuma iliyomtuhumu Balozi Krista kusafirisha wasichana wa kitanzania kwenda kufanya biashara ya ngono nchini mwake.   
Mbali na kukataa kutoa maoni kuhusu Habari hiyo kwa msimamo kuwa haikuwa na taarifa kutoka vyanzo vya msingi ama vilelezo. Mkurugenzi wa TAMWA hakukubali kutoa maoni wala kuzungumza maneno kama ilivyonukuliwa na gazeti hilo na  badala yake mhariri na mwandishi  wa Jamhuri Media ambao walidhamiria kumuandika katika taarifa hiyo wamemlisha maneno Mkurugenzi wa TAMWA Dk Rose Reuben.
Ifahamike kuwa chama hiki ni cha kihabari na hivyo kinafahamu misingi yote ya taaluma ya habari na mawasiliano na hivyo tunasikitishwa na mmonyonyoko huu wa maadili uliofanywa  na gazeti la Jamhuri.
Kwa unyenyekevu tunawataka waombe radhi katika gazeti hilo. 
Kadhalika, TAMWA inafanya kazi na wanahabari kila siku na imekuwa ikiruhusu mahojiano na Mkurugenzi Dk Rose Reuben bila kuweka vikwazo, lakini endapo chama hakijatoa ruhusa ya kunukuliwa, basi maombi hayo yaheshimiwe kama maadili ya kihabari yanavyofundisha. 
Kwa kuwa TAMWA ni sehemu ya wanahabari, tunapenda kutoa wito kwa wanahabari wote kufuata misingi na maadili ya habari pindi wanapotimiza majukumu yao. 
Dkt. Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji ~ TAMWA.

Search