Press Release

TAMWA: Ubakaji wa watoto ni janga la kitaifa

User Rating: 2 / 5

Star ActiveStar ActiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Novemba 25, 2021, Dar es Salaam. Leo Dunia inanza madhimisho ya  Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. 
 
Maadhimisho haya  yanayobebwa na kauli mbiu isemayo; Ewe Mwananchi, Pinga ukatili wa kijinsia Sasa yanakuja wakati ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kukithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, ikiwamo ubakaji hapa nchini.
 
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinasikitishwa na ongezeko la ukatili huu hasa kwa watoto na wanawake ambao ndio tegemeo katika mustakabali wa kimaendeleo nchini. 
 
Akiwa bungeni, Naibu Waziri wa Afya, Mwanaidi Ali Khamis alinukuliwa akisema, kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu, watoto 6168 walifanyiwa ukatili wa kijinsia na kati yao, 3524 walibakwa. Wakati huo Naibu Waziri alisema, wanafunzi 1887 walipata ujauzito katika kipindi hicho hicho. 
 
Takwimu hizi zinaamanisha nini? Zinamaanisha kwamba, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa basi katika kipindi cha mwaka mmoja, zaidi ya watoto 7000 watakuwa wamebakwa au watoto zaidi ya 12,000 watakuwa wamefanyiwa ukatili.
 
Takwimu hizi mpya zinaogofya na kutufanya TAMWA tuone pengine wadau, ikiwamo serikali, wazazi na walezi, tukubaliane na kutamka kuwa; Ubakaji sasa ni janga.
 
TAMWA tunaona ni wakati sahihi sasa, kwa wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia, kukaa pamoja na kupanga mikakati mipya na madhubuti zaidi ya kumaliza au kupunguza matukio haya kwani sheria na sera nzuri zipo lakini ukatili huo bado unaendelea katika jamii yetu. 
 
Hata hivyo tunaipongeza mahakama kwa kutoa hukumu na kufuatilia kwa ukaribu kesi hizi za ubakaji, kwani ipo mifano ya waliohukumiwa kwa kufanya matukio haya. Tunayapongeza madawati ya jinsia kwa kusimamia upelelezi na kutoa ushauri kuhusu matukio au kesi hizi za ubakaji na ukatili mwingine.  Hata hivyo bado matukio haya yanaendelea kuongezeka kila kukicha. Je tatizo lipo wapi? 
 
Ni muhimu kwa taifa, sasa kuendelea kubuni njia mbadala na mpya za kukabiliana na janga hili. Tunaliita janga kwa sababu, watoto 3524 kubakwa si lelemama, bali ni tatizo kubwa katika jamii yetu ambalo linaharibu kabisa mustakabali wa maisha ya kizazi kijacho.
 
Wakati huo huo, bado kinamama wanaendelea kupokea vipigo, kubakwa, kupewa lugha dhalilishi katika jamii yao hali inayowafanya kuwa kundi linaloomboleza na wakati mwingine kuichukia jinsia yao. 
 
"Ukatili huu, una madhara ya muda mfupi, muda mrefu, kiuchumi, kimwili na kisaikolojia kwa wanawake na wasichana na watoto wote kwa ujumla, kwani inawazuia kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika jamii yao," Dk Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA. 
 
"Hakuna namna nyepesi ya kuelezea madhara haya ya ukatili wa kijinsia, tumewahi kuona, pengine tumesikia lakini bado jamii nzima haijajua madhara yake kwa kina labda kwa sababu, matukio haya hayatokei kwa wingi mara moja. Lakini tungewapata waathirika hawa na kuwakusanya pamoja, basi Tanzania ingelia," Dkt Reuben.
 
"Ubakaji huu wa watoto ni janga. Serikali itambue kuwa hili ni janga kwa sababu madhara yake yanaweza yasionekana kwa sasa lakini yataonekana baadaye wakati ambapo kizazi hiki cha sasa kitakapokuwa kimeshika usukani" Dkt Reuben.
 
TAMWA inaamini kuwa taifa salama ni lile linalojenga kizazi salama, ambacho waliopo wanawalinda watoto na kumlinda mwanamke. Hivyo basi, ili kuwa na jamii hiyo hatuna budi kuchagizana kwani; waswahili walisema; Kichango ni kuchagizana Kila mmoja ashiriki kwa namna yake kumaliza ukatili huu.
 
Kidunia hali ni kama hii, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wanawake(UN-Women)zinaonyesha kuwa ukatili wa wanawake aghalabu hufanywa na mwenza, mume wa zamani au wa sasa. Inaelezwa kuwa wanawake zaidi ya milioni 640 wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea waliwahi kufanyiwa ukatili na wenza.
 
Ukatili huu unatajwa kusababisha msongo wa mawazo, kihoro, mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa ikiwamo UKIMWI na wakati mwingine waathirika kujiua. 
 
Takwimu hizo kadhalika zinaeleza kuwa, zaidi ya wanawake 87,000 duniani waliuawa na nusu yao, (50,000) waliuawa na mwenza au mwanafamilia. Zaidi ya thuluthi, waliuawa kwa makusudi na mwenza/mume wa sasa au wa zamani. 
 
TAMWA imeona zaidi kuwa unyanyasaji huu kwa hapa Tanzania umeendelea kujikita pia katika mashindano ya ulimbwende, vyuo vikuu, vyombo vya habari ikiwemo  mitandaonii pamoja na mahala pa kazi. Haya yote yasipofanyiwa kazi, basi tutakuwa na dunia isiyo salama kwa kundi hili.
 
"Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha wazi kuwa anasimamia vyema haki za wanawake na watoto, tumemuona na kumsikia akipinga lugha dhalilishi kwa wanawake na udunishwaji wa kundi hilo katika nafasi za siasa na uongozi. Kongole Rais wetu,"Dkt Rose Reuben
 
TAMWA hatutaacha kusimamia haki za wanawake, watoto na wanahabari, tutaendelea kupaza sauti hadi tutakapoona amani imetawala tukiendelea kusema "Ewe Mwananchi, Pinga ukatili wa kijinsia Sasa”.
 
Kazi iendelee. 
 
Dk. Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA
 

Search