News/Stories

SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Machi 18, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
 
TAMWA inaungana na watanzania wote kuomboleza kifo cha kiongozi  huyo mahiri, Rais John Pombe Magufuli. 
Kwa niaba ya wanachama wa TAMWA, bodi ya TAMWA, Wanahabari, Wanawake, na wapigania haki za jinsia, tunatoa pole kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu,  familia ya Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli viongozi wa serikali na watanzania wote kwa kumpoteza kiongozi wa nchi. 
 
TAMWA inaomboleza msiba huu kwa kukumbuka mafanikio yaliyofanywa na Rais Magufuli katika kipindi cha uongozi wake tangu mwaka 2015. 
 
Rais Magufuli alikuwa na juhudi katika kujenga miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa ilisaidia kumkomboa mwanamke kuanzia ngazi za chini. 
Miundombinu aliyojenga kuanzia ya maji, barabara na mingineyo, ilikuwa inalenga kumkomboa mwanamke, kumtua mama ndoo kichwani na kumsaidia mjasiriamalia mwanamke kufanya shughuli zake kwa umakini na ufasaha, 
Aliwahi kusema kuwa, katika wizara inayomnyima raha  ni wizara ya maji, na hivyo akaamua kuimairisha eneo hilo ili kuhakikisha adha ya maji inatoweka. Kwa kufanya hivyo alimsaidia sana mwanamke wa kijijini na mjini, mwanamke na mtoto wa kike, kwa sababu ukosefu wa maji ulichangia kwa kiasi kikubwa ukatili wa kijinsia, ukosefu wa masomo na ufinyu wa kipato. 
 
Rais Magufuli alikuwa akijipambanua kuwa rais wa wanyonge na kweli alijitahidi kuimarisha miundombinu ya maji, umeme na kuwatazama wajane waliodhulumiwa kwa namna moja au nyingine, kuondoa riba kwa mikopo ya wanawake ya Halmashauri. 
 
TAMWA tulitamani Rais Magufuli, akamilishe kipindi chake  cha uongozi ili Watanzania tupate hasa kile alichodhamiria kukamilisha, kwa sababu alikuwa na maono makubwa.
TAMWA itamkumbuka Rais Magufuli kwa kuwa rais wa kwanza kumteua mwanamke kuwa Makamu wa Rais. 
Kwa hili aliweka historia nchini, ya kuwepo Makamu wa kwanza wa Rais mwanamke, hata kama hatujaifikia ile asilimia 50 kwa 50 ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, 
 
Rais Magufuli atakumbukwa kama kiongozi aliyekuwa anatamani kuwakomboa wananachi kwa ujumla na sio kuwepo kwa mafanikio ya mtu mmoja mmoja. 
 
Mungu ailaze roho ya Hayati John Pombe Magufuli Mahali pema Amina!
 
Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji 
TAMWA.

Latest News and Stories

Search