Gallery

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Mhe. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa;

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Iddi Hassan Kimata;

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Mhe.Eng. Kundo Andrea Mathew;

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Peter Mutuku Mathuki;

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Anders Sjoberg;

Mwakilishi Mkazi wa Unesco nchini Tanzania, Mhe. Titso Dos Santos;

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Legal Service Facility, Lulu Ng’wanakilala;

Wawakilishi wa Jumuiya ya Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT);

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-Tan), Salome Kitomari;

Mwenyekiti wa Mtandao wa Radio za kijamii Tanzania (TADIO) Prosper Kwigize;

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben;

Wawakilishi wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF)

Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT);

Wawakiliishi wa Umoja wa Club za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)

Mwenyekiti wa Arusha Press Club, Claud Gwandu;

Wahariri na Waandishi wa habari;

Mabibi na Mabwana,

Mheshimiwa mgeni Rasmi, kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai, na ni kwa neema zake kuwa leo tuko hapa kufanya shughuli hii muhimu ya kukumbushana utendaji wa vyombo vyabari nchini na duniani, ambapo hatimaye tutaimarisha ushirikiano kati ya dola, jamii na vyombo vya habari kwa masilahi mapana ya maendeleo ya taifa letu.

Nakushukuru kwa kukubali mwaliko wetu, kwani kwa kufanya hivi Mhe. Waziri unadhihirisha kwa matendo kauli ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akiwaapisha makatibu wakuu kwamba serikali chini ya uongozi wake itaendelea kuenzi uhuru wa habari.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Ndugu Wanahabari,

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia uzima, afya njema na kuniwezesha kukutana nanyi ili niweze kuongea na watoto, wazazi/walezi na jamii kupitia kwenu wanahabari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2020.

Ndugu Wanahabari,

Tarehe 16 Juni, ya kila mwaka, Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ikiwemo Tanzania huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika. Chimbuko la maadhimisho haya ni mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa na Utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto, nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni, 1976. Mauaji hayo yalitokea wakati wa maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakipinga mfumo wa elimu ya kibaguzi nchini humo. Mwaka 1991 viongozi wa Umoja wa Nchi za Afrika walifanya uamuzi wa kuienzi siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto hao. Maadhimisho haya yanatumiwa na wadau wote katika nchi za Afrika kutathmini ya hali ya upatikanaji wa haki na ulinzi kwa watoto kwa lengo la kuboresha ustawi na Maendeleo ya watoto.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Dar Es Salaam, Oktoba 29, 2021.
 
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinalaani  tukio la Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, kudaiwa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike chuoni hapo.
 
Taarifa iliyotolewa na Chuo hicho baada ya kusambaa kwa jumbe za uwepo wa tukio hilo chuoni hapo katika mitandao ya jamii,  imeeleza kuwa Mhadhiri huyo, Petrol Mswahili, amefanya vitendo hivyo kwa wanafunzi wa kike, jambo linalodhihirisha uwepo wa rushwa ya ngono. 
 
TAMWA ikiwa ni taasisi inayopinga unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake ikiwamo rushwa ya ngono, tunalaani  tukio hilo linalovunja maadili ya utumishi wa umma na zaidi hasa kudhalilisha watoto wa kike katika taasisi hii ya elimu ya juu.
 
Kadhalika, TAMWA tunasikitishwa na  vitendo hivyo ambavyo sio tu vimekuwa chanzo cha kuharibu mustakabali wa kitaaluma wa watoto wa kike, lakini pia ndicho chanzo cha magonjwa ya kuambukiza, sonona na kurudisha nyuma kundi hilo. 
 
Mwaka 2019 TAMWA ilifanya tathmini ya kuangazia ukubwa wa rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari, maeneo ya kazini na taasisi za elimu ya juu, na kubaini kuwa tatizo hilo lipo kwa ukubwa wake.
 
Kadhalika TAMWA ilibaini kuwa ukimya umetawala kwa wale waathirika wa rushwa ya ngono kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo woga wa kukosa vibarua, kufukuzwa shule au kufeli mitihani yao. 
 
Hivyo tunalaani vikali vitendo hivi huku tukiupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuchukua hatua za haraka dhidi ya mhadhiri huyo lakini pia tunaushauri uongozi wa chuo hicho kuweka mikakati itakayokomesha vitendo hivyo.
 
TAMWA inaomba pindi uchunguzi utakapokamilika basi sheria ichukue mkondo wake ili iwe funzo kwa wahadhiri wengine wanaoharibu watoto wa kike. Pia tunaiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) iendelee kushirikiana na wadau kutoa elimu kuhusu rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine wa kijinsia. 
 
"Digrii bila rushwa ya ngono, ni digrii yenye tija"
 
Imetolewa na;
 
Mkurugenzi Mtendaji waTAMWA,
 
Dk Rose Reuben.
 

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Mheshimiwa, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani Dk. Willow Williamson, Mwakilishi kutoka Dawati la jinsia Mkoa wa Kinondoni Mathias Mulumba, Mwakilishi kutoka Muungano wa ‘Men engage Tanzania’ Marcela Lungu na Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali nchini, Habari za asubuhi.
UKATILI WA JINSIA: “MABADILIKO YANAANZA NA MIMI”
Wakati dunia ikiadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na CRC kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani Tanzania, (UsEmbassyTz) tunawasisitiza wanajamii kuibua na kufichua matukio yote ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea kuanzia katika ngazi ya familia na katika taasisi kama vile mashuleni, vyuoni na sehemu kazi.

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
Mei 3 kila mwaka Duniani kote tunaadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, Tangu umoja wa mataifa ilipoidhinisha siku hiyo mwaka 1993, Hapa nchini kama wadau na wanahabari tumeendeleza utaratibu huu wa kusherekea maadhimisho haya ambapo kwa mwaka huu  kauli mbiu yake ni “Habari kwa manufaa ya Umma”. 
Lengo la maadhimisho haya ni kukuza uelewa wa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na kukumbusha serikali na jamii umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki ya uhuru wa Habari kama inavyolindwa katika Ibara ya 19 ya tamko la ulimwengu la haki za binadamu. 
Tunapoelekea  kilele cha maadhimisho haya, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Taasisi zaidi ya 20  za kihabari za kitaifa na kimataifa nchini chini ya Shirika la umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), Tunaungana na jamii na  ulimwengu  kuadhimisha siku hii adhimu ambayo sherehe za kilele zitafanyika Jijini Arusha siku ya tarehe 3 mwezi wa 5 2021.
TAMWA kwa niaba ya waandaaji wa maadhimisho haya  tunapenda kutoa salamu za pole kwa serikali ya jamuhuli ya muungano wa Tanzania na kwa wananchi wote kwakuondokewa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dk.John Joseph Pombe Magufuli, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina.
“Tusimame dakika moja kumuombea Hayati Rais wa awamu ya tano Dk. John Joseph Pombe Magufuli”.
Katika siku hii TAMWA tunawiwa kuikumbusha serikali umuhimu wa kulinda uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla pia kupongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania MHE. Samia Suluhu Hassan kwakuona umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa  uhuru na kujali uzalendo wa nchi  bila kuvunja sheria.
Rais Samia mapema aliposhika nyazfa ya urais, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu  alimwagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa na kuagiza wahusika kutotumia ubabe kuvidhibiti. 
Pia alishauri Vyombo vya habari visifungiwe kibabe na kuongeza kuwa namnukuu “Watakapofanya makosa adhabu zitolewe kulingana na sheria inavyoelekeza, viacheni vifanye kazi yao isionekane wanazuiwa kuongea,”.
TAMWA kikiwa ni chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania na kufanya shughuli zake nyingi kwa kutumia vyombo vya habari kimefarijika sana kusikia na kuona namna kiongozi wa nchi kulipa uzito suala hili mara tu aliposhika nyazfa hiyo.
Katika Jamii yetu vitendo vya kupokwa kwa uhuru wa habari kwa wanahabari pamoja na Tasnia yote kwa ujumla vimekuwa vikitendwa mara kwa mara na baadhi ya viongozi katika Nyanja mbalimbali za Serikali bila kujali kuwa ni uvunjifu wa haki kwa tasnia ya habari na kwa jamii kwa ujumla.
Ukamataji wa wanahabari kinyume na sheria: Ukamataji wa waandishi wa habari kinyume na sheria mwanzoni mwa mwaka huu tuliona kwa aliyekuwa  Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Mhe. Lusubilo Mwakabibi, alituhumiwa kuwaweka chini ya ulinzi kwa saa 3 Wanahabari wawili kutokana na kuhudhuria Mkutano wake na Wafanyabiashara wa soko la Mbagala Rangi Tatu pasipo kupewa mwaliko, Wanahabari hao ni Christopher James kutoka ITV & Radio One pamoja na Dickson Billikwija wa Island TV. 
Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari na wanahabari ni moja ya haki ya msingi ya kiraia ambayo huwapa jamii haki yao ya kupata habari na kusambaza taarifa, haki ya uhuru wa kujieleza pamoja na haki ya uhuru wa maoni ambazo ni haki za msingi katika mataifa yanayojiendesha kwa misingi ya demokrasia.
Uwepo wa sheria kandamizi: Katika hili tumeona sheria kandamizi zimeendelea kuwa kikwazo katika utekelezaji na uhabarishaji na uhuru wa kujieleza nchini Tanzania, kama sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015, Sheria ya upatikanaji wa habari 2016 na kanuni ya maudhui ya kimtandao, Sheria hizi zina vifungu amabvyo havijakidhi viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza.
 Ukatili wa kijinsia katika vyombo vya habari: Tafiti ndogo iliyofanywa na Shirika la umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), tathimini ya muundo na utendaji ndani ya vyombo vya habari dhidi ya uhamasishaji wa usawa wa kijinsia na kupinga udhalilishaji kwa wanahabari wanawake , inaonyesha kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyumba vya habari. 
Ndugu Wadau wa habari: TAMWA tunasihi wadau wa habari kuungana kwa pamoja kwa lengo la kuwaimarisha wanahabari kwa kuwapa mafunzo, maarifa na kuwajengea uwezo juu ya masuala ya jinsia, ambayo itapelekea kuwezesha wanahabari kujitambua, kujiamini na kusaidia kuwepo kwa usawa wa kijinsia  na kutokomeza ukatili ndani ya vyumba vya habari.
Sera: TAMWA inasihi kuwepo na sera na mfumo rasmi wa kutoa taarifa za masuala ya ukatili wa kijinsia na usalama binafsi ambao hautatoa mwanya wowote wa unyanyasaji wa kingono, na taratibu thabiti za kuripoti unyanyasaji huo.
TAMWA inaomba ushirikiano zaidi kutoka kwa wadau wa habari wakiwemo, Asasi za kiraia,  Wizara ya Habari na Michezo, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee Watoto na Wizara ya sheria na katiba  kwa jamii kwa kuhakikisha uhuru wa habari unaeshimika na kupelekea wanahabari kutoa habari kwakufuata sheria na taratibu na kufikia jamii yote kama kaulimbio yetu inavyo sema “Habari kwa manufaa ya umma” 
Pia kutoa  elimu kwa wanahabari na kwa jamii kuhusiana na ukatili wa kijinsia, Kwani vitendo hivyo ni moja ya sababu ya kupotea kwa uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari katika kutekeleza majukumu yao.
Ndugu Wanahabari na vyombo vya habari: TAMWA tunasihi vyombo vya habari kuwa mastari wa mbale kuahabariasha na kutoa taarifa na kuburudisha kwa kuzingatia maadili yanayoongoza tasnia ya habari pamoja na kufuata sheria za nchi.   
Maadhimisho ya Mwaka 2021 yana mafanikio mengi katika tasnia ya habari, Kufuatia na ongezeko la vyombo vya Habari kulingana na takwimu alizozisema  Hayati Rais wa awamu ya tano Dk.John Joseph Pombe Magufuli, wakati  alivyokuwa Akizindua studio za vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayati Rais Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano serikali yake imeruhusu vyombo vingi zaidi vya habari kuliko wakati mwingine wowote tangu taifa hilo lipate uhuru.
Alisema  mwaka 2015, Tanzania ilikuwa na vituo vya radio 106 na televisheni 25 lakini hadi kufikia mwezi februari 2021 kuna jumla ya vituo vya redio 193, televisheni 46, magazeti 247,televisheni za mtandao 443 na redio za mtandao 23.
 
%%%%%%%%  “Habari kwa manufaa ya umma”  %%%%%%%%%
 
Imetolewa  Mei 27,2021 na:
Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji.

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
Dar Es Salaam, October 11, 2021. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinawakumbusha, wazazi, walezi, wadau, serikali na waandishi wa habari kuchukua hatua ili kuondoa aina mpya ya ukatili kwa njia ya mitandao ya kijamii.
 
Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Oktoba 11, ambapo kwa mwaka huu, kauli mbiu ya kitaifa na kimataifa ni: Kizazi cha Kidijitali, Kizazi Chetu!.
 
Kauli mbiu hii inalenga kuikumbusha jamii kutoa haki sawa kwa watoto wote kwenye teknolojia ya kidijitali ili waitumie  kwa Maendeleo na kwa usahihi.  
 
Zipo faida lukuki za matumizi ya mitandao ya kijamii, kama vile elimu kwa njia ya mitandao, taarifa muhimu za kitaifa na kimataifa lakini  bado watoto wa kike wameonekana kuachwa nyuma katika ulimwengu wa kidijitali kwa kukosa  fursa sawa hasa katika matumzi ya intanenti, kumiliki simu janja, na uhuru wa  kutumia mitandao ya kijamii kama ilivyo kwa watoto wa kiume. 
 
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya wanawake, (UN-Women) Julai mwaka huu, ilionyesha kuwa kuna ongezeko la ukatili wa kijinsia kupitia mitandao ya kijamii. 
 
Ripoti hiyo imeeleza: Upatikanaji  wa intaneti kwa watoto wa kike na wanawake, umesababisha kundi hilo kukumbana na udhalilishaji wa kingono zaidi, ukilinganisha na wanaume,
 
Kadhalika ripoti hiyo imeonyesha zaidi kuwa, watoto wa kike wamekuwa wakitishiwa kimwili, kutumiwa picha za ngono, na kupewa lugha dhalili katika mitandao ya kijamii.
 
Kwa hapa Tanzania, matukio kadhaa ya udhalilishaji wa kingono kwa njia ya mtandao yamewahi kuripotiwa ikiwamo kusambazwa kwa video za ngono zikiwaonyesha watoto wa kike, huku mwanaume akifichwa uso.
 
Aina nyingine ya ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao ni kashfa na matamshi ya chuki, jina la akaunti kuibwa na  na kisha kutumiwa na watu kwa njia za utapeli au kurushwa kwa video za ngono. Hili limewakuta zaidi watoto wa kike wenye majina makubwa au maarufu katika jamii. 
 
Lakini pia, imekuwa ni tamaduni kwa watoto wa kike kurushiwa lugha dhalilishi kwa njia ya mtandao, ikiwamo zile zinazohusisha baadhi ya maungo yao ya mwili.
 
Picha za watoto wa kike zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii na kugeuzwa mjadala jambo ambalo limeonekana kuchangia kuongezeka kwa lugha dhalili dhidi yao.
 
Kutokana na kuongezeka kwa matukio haya yanayoendana na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii, hatuna budi kupunguza udhalilishaji huu na kuendelea kuhimiza matumizi sahihi, salama na yenye faida, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben.
 
Reuben ameomba  wazazi, walezi, serikali, asasi za kijinsia, asasi za kiraia, wapatanishi na wanahabari, kusimamia usalama wa watoto kike mitandaoni. 
 
Inawezekana tabia hizi zinaonekana kuwa ni za kawaida au kugeuzwa utamaduni lakini zimeleta madhara kwa watoto wa kike ikiwamo kukatisha masomo, kujiua, kutengwa na jamii na baadhi kuathirika kisaikolojia, Dkt, Reuben
 
TAMWA inaamini katika usawa wa kijinsia, haki za watoto na wanawake, hivyo katika kuadhimisha siku hii, tunaikumbusha serikali kutunga sheria zinazoendana na kasi ya teknolojia ili kuwabana wale watakaofanya ukatili wa kingono kwa njia ya mtandao.
 
Sheria isifumbe macho katika masuala haya, lakini si hayo tu, bado tunasisitiza hata ile sheria ya ndoa  ibadilishwe ili kumpa mtoto wa kike haki ya kusoma na kuolewa katika umri wa utu uzima Dkt. Reuben
 
TAMWA inapenda kutoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa matumizi ya dijitali katika jamii yetu ili kuendana na uhalisia wa dunia, pia  kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kutoa na kuwezesha watoto wote kupata elimu ya masuala ya dijitali pia kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya kidijitali  kwa kuzingatia jinsi zote bila ubaguzi.
 
TAMWA inaamini kuwa, maadhimisho ya mwaka huu, yataangazia  changamoto na fursa za kidijitali  kwa mtoto wa kike lakini bila kusahau, kuwa kumbe; malezi bora, elimu kwa mtoto wa kike ndicho chanzo cha leo kuwa na Rais wa kwanza mwanamke, ambaye ni Mama Samia Suluhu.
 
Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni siku ya kimataifa iliyotangazwa na Umoja wa Mataifa; pia inaitwa Siku ya Wasichana na Siku ya Kimataifa ya Wasichana. Siku hii huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 11.
 
Umoja wa Mataifa ulianza kuadhimisha siku hii baada ya kuonekana kuna changamoto nyingi zinazomuandama mtoto wa kike ikiwamo kunyimwa fursa ya kupata elimu, ubakaji, ulawiti,  ndoa za mapema, mimba za mapema na kukosa haki nyingine ikiwamo ya kucheza na kushauri katika ngazi ya familia. 
 
Maadhimisho hayo pia yanaangalia  mafanikio ya watoto kike kidunia, ikiwamo Tanzania kama vile  kuongezeka kwa idadi ya watoto wa kike wanaopata elimu ya juu, watoto wa kike kuendelea kupata elimu ya afya ya uzazi na kufikiwa na taasisi mbalimbali zinazogusa maisha ya mtoto wa kike.
 
Kizazi cha Kidijitali, Kizazi Chetu!
 
Dkt Rose Reuben.
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA

Search