Juni 16, 2019. Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), kinaungana na taasisi za umma na zisizo za umma zinazotetea haki za watoto duniani katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16 kila mwaka.
Kauli mbiu ya mbiu ya mwaka huu ni Mtoto ni msingi wa taifa endelevu tumtunze tumlinde na kumuendeleza.
Pamoja na changamoto zinazomkabili mtoto wa kiafrika, lakini takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa ubakaji umeendelea kuwa ni janga la Taifa.
Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na LHRC zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka 2018 watoto 2365 walibakwa, idadi ambayo ni sawa na watoto 394 kwa siku.
Kadhalika ripoti ya hali ya uhalifu kwa mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) inaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2017, matukio ya uhalifu dhidi ya watoto yalikuwa 13,457. Kwa mwaka 2016 matukio hayo yalikuwa 10,551. Kati ya hayo, matukio ya ubakaji yalikuwa 2984.
Kutokana na uzito wa takwimu hizi, TAMWA inaiomba serikali na wadau wengine wa masuala ya haki za watoto waendelee kupaza sauti zao ili kuhakikisha ukatili huu unapungua na ikiwezekana unamalizika kabisa.
Mtoto ni taifa la kesho, endapo atafanyiwa ukatili leo, je kesho taifa hili litaongozwa na nani? TAMWA tunasisitiza hatua kali za kisheria na mabadiliko mengine ya kisera ili kumlinda mtoto dhidi ya ukatili, Rose Reuben, Mkurugenzi wa TAMWA. Kadhalika TAMWA inawasihi wazazi, walezi kulipa uzito mkubwa suala la ulinzi kwa mtoto ili kuepusha ubakaji kwani, ripoti ya UNICEF inaonyesha kuwa wabakaji wengi ni ndugu wa karibu ambao tunaishi nao nyumbani.
Kupinga unyanyasaji, ubakaji na ulawiti wa watoto ni jukumu la jamii nzima na wakati umefika sasa kila mmoja kwenye nafasi yake awalinde watoto kwa kuripoti vitendo vya unyanyasaji vilivyofichika kwenye jamii yetu.
Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA