Mei 3 kila mwaka Duniani kote tunaadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, Tangu umoja wa mataifa ilipoidhinisha siku hiyo mwaka 1993, Hapa nchini kama wadau na wanahabari tumeendeleza utaratibu huu wa kusherekea maadhimisho haya ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni “Habari kwa manufaa ya Umma”.
Lengo la maadhimisho haya ni kukuza uelewa wa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na kukumbusha serikali na jamii umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki ya uhuru wa Habari kama inavyolindwa katika Ibara ya 19 ya tamko la ulimwengu la haki za binadamu.
Tunapoelekea kilele cha maadhimisho haya, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Taasisi zaidi ya 20 za kihabari za kitaifa na kimataifa nchini chini ya Shirika la umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), Tunaungana na jamii na ulimwengu kuadhimisha siku hii adhimu ambayo sherehe za kilele zitafanyika Jijini Arusha siku ya tarehe 3 mwezi wa 5 2021.
TAMWA kwa niaba ya waandaaji wa maadhimisho haya tunapenda kutoa salamu za pole kwa serikali ya jamuhuli ya muungano wa Tanzania na kwa wananchi wote kwakuondokewa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dk.John Joseph Pombe Magufuli, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina.
“Tusimame dakika moja kumuombea Hayati Rais wa awamu ya tano Dk. John Joseph Pombe Magufuli”.
Katika siku hii TAMWA tunawiwa kuikumbusha serikali umuhimu wa kulinda uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla pia kupongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania MHE. Samia Suluhu Hassan kwakuona umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru na kujali uzalendo wa nchi bila kuvunja sheria.
Rais Samia mapema aliposhika nyazfa ya urais, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu alimwagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa na kuagiza wahusika kutotumia ubabe kuvidhibiti.
Pia alishauri Vyombo vya habari visifungiwe kibabe na kuongeza kuwa namnukuu “Watakapofanya makosa adhabu zitolewe kulingana na sheria inavyoelekeza, viacheni vifanye kazi yao isionekane wanazuiwa kuongea,”.
TAMWA kikiwa ni chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania na kufanya shughuli zake nyingi kwa kutumia vyombo vya habari kimefarijika sana kusikia na kuona namna kiongozi wa nchi kulipa uzito suala hili mara tu aliposhika nyazfa hiyo.
Katika Jamii yetu vitendo vya kupokwa kwa uhuru wa habari kwa wanahabari pamoja na Tasnia yote kwa ujumla vimekuwa vikitendwa mara kwa mara na baadhi ya viongozi katika Nyanja mbalimbali za Serikali bila kujali kuwa ni uvunjifu wa haki kwa tasnia ya habari na kwa jamii kwa ujumla.
Ukamataji wa wanahabari kinyume na sheria: Ukamataji wa waandishi wa habari kinyume na sheria mwanzoni mwa mwaka huu tuliona kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Mhe. Lusubilo Mwakabibi, alituhumiwa kuwaweka chini ya ulinzi kwa saa 3 Wanahabari wawili kutokana na kuhudhuria Mkutano wake na Wafanyabiashara wa soko la Mbagala Rangi Tatu pasipo kupewa mwaliko, Wanahabari hao ni Christopher James kutoka ITV & Radio One pamoja na Dickson Billikwija wa Island TV.
Haki ya Uhuru wa Vyombo vya Habari na wanahabari ni moja ya haki ya msingi ya kiraia ambayo huwapa jamii haki yao ya kupata habari na kusambaza taarifa, haki ya uhuru wa kujieleza pamoja na haki ya uhuru wa maoni ambazo ni haki za msingi katika mataifa yanayojiendesha kwa misingi ya demokrasia.
Uwepo wa sheria kandamizi: Katika hili tumeona sheria kandamizi zimeendelea kuwa kikwazo katika utekelezaji na uhabarishaji na uhuru wa kujieleza nchini Tanzania, kama sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015, Sheria ya upatikanaji wa habari 2016 na kanuni ya maudhui ya kimtandao, Sheria hizi zina vifungu amabvyo havijakidhi viwango vya kimataifa vya uhuru wa kujieleza.
Ukatili wa kijinsia katika vyombo vya habari: Tafiti ndogo iliyofanywa na Shirika la umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), tathimini ya muundo na utendaji ndani ya vyombo vya habari dhidi ya uhamasishaji wa usawa wa kijinsia na kupinga udhalilishaji kwa wanahabari wanawake , inaonyesha kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyumba vya habari.
Ndugu Wadau wa habari: TAMWA tunasihi wadau wa habari kuungana kwa pamoja kwa lengo la kuwaimarisha wanahabari kwa kuwapa mafunzo, maarifa na kuwajengea uwezo juu ya masuala ya jinsia, ambayo itapelekea kuwezesha wanahabari kujitambua, kujiamini na kusaidia kuwepo kwa usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili ndani ya vyumba vya habari.
Sera: TAMWA inasihi kuwepo na sera na mfumo rasmi wa kutoa taarifa za masuala ya ukatili wa kijinsia na usalama binafsi ambao hautatoa mwanya wowote wa unyanyasaji wa kingono, na taratibu thabiti za kuripoti unyanyasaji huo.
TAMWA inaomba ushirikiano zaidi kutoka kwa wadau wa habari wakiwemo, Asasi za kiraia, Wizara ya Habari na Michezo, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee Watoto na Wizara ya sheria na katiba kwa jamii kwa kuhakikisha uhuru wa habari unaeshimika na kupelekea wanahabari kutoa habari kwakufuata sheria na taratibu na kufikia jamii yote kama kaulimbio yetu inavyo sema “Habari kwa manufaa ya umma”
Pia kutoa elimu kwa wanahabari na kwa jamii kuhusiana na ukatili wa kijinsia, Kwani vitendo hivyo ni moja ya sababu ya kupotea kwa uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari katika kutekeleza majukumu yao.
Ndugu Wanahabari na vyombo vya habari: TAMWA tunasihi vyombo vya habari kuwa mastari wa mbale kuahabariasha na kutoa taarifa na kuburudisha kwa kuzingatia maadili yanayoongoza tasnia ya habari pamoja na kufuata sheria za nchi.
Maadhimisho ya Mwaka 2021 yana mafanikio mengi katika tasnia ya habari, Kufuatia na ongezeko la vyombo vya Habari kulingana na takwimu alizozisema Hayati Rais wa awamu ya tano Dk.John Joseph Pombe Magufuli, wakati alivyokuwa Akizindua studio za vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayati Rais Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano serikali yake imeruhusu vyombo vingi zaidi vya habari kuliko wakati mwingine wowote tangu taifa hilo lipate uhuru.
Alisema mwaka 2015, Tanzania ilikuwa na vituo vya radio 106 na televisheni 25 lakini hadi kufikia mwezi februari 2021 kuna jumla ya vituo vya redio 193, televisheni 46, magazeti 247,televisheni za mtandao 443 na redio za mtandao 23.
%%%%%%%% “Habari kwa manufaa ya umma” %%%%%%%%%
Imetolewa Mei 27,2021 na:
Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji.