Press Release

Nafasi ya mwanamke kuelekea Uchaguzi Mkuu Octoba 28, 2020 katika mustakabali wa haki, heshima, amani, utulivu na kuchagua viongozi bora

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Zanzibar, Septemba 16th, 2020. Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Waheshimiwa viongozi wa dini, wakiwamo maaskofu, masheikh, wachungaji.
Waheshimiwa viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa serikali, wakuu wa vyombo vya usalama na wanahabari. 
Itifaki imezingatiwa!
“Dini mbalimbali, Amani na Upendo, Amani na upendo, Dini mbalimbali!
Kwanza napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha katika kusanyiko hili na kutupa afya njema. 
 Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinayo furaha kubwa na kinatoa shukrani za dhati kwa viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa serikali, wanahabari, vyombo vya usalama na taasisi nyingine zisizo za kiserikali kwa kukubali kujumuika nasi katika warsha hii muhimu. 
 
Ndugu Mgeni Rasmi,
Bila shaka wengi wetu tunafahamu fika kuwa Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba 28 mwaka huu. 
Kutokana na tukio hilo kubwa la kihistoria, TAMWA imeona ni vyema kuhimiza na kukumbusha suala la nafasi ya mwanamke katika uchaguzi na kuishirikisha kamati ya Amani ya Viongozi wa dini nchini ambayo inaundwa na viongozi wa dini mbalimbali. 
Uwepo wako mahali hapa, ndugu mgeni rasmi, viongozi hawa wa dini na wadau wengine wa masuala ya Amani, umeonyesha dhahiri kuwa jambo hili ni zito na linaonyesha  mmeipa uzito ajenda hii na mnathamini nafasi ya mwanamke katika uchaguzi mkuu ujao.  
 
Ndugu mgeni Rasmi,
Ushiriki wa Wanawake katika siasa na katika ngazi za maamuzi, ni eneo lililo na changamoto lukuki na hivyo linahitaji kuhimizwa na viongozi wa ngazi za juu, asasi za kiraia, wanawake wenyewe na viongozi wa dini. 
Makundi niliyoyataja hapo juu yakitimiza wajibu wake katika kuhimiza na kuelimisha juu ya umuhimu wa wanawake katika uongozi, basi ni dhahiri kuwa, tutafikia ule usawa wa 50 kwa 50 ambao tumekuwa tukiupigia kelele kwa muda mrefu. 
Kwa sasa takwimu zinaonyesha kuwa bado ni asilimi 37 tu ya wanawake ndio walioko katika ngazi za maamuzi bungeni, hata hivyo bado tunaona kuna mapengo katika ushiriki wao ambayo hayana budi kuzibwa.
 
 Ndugu mgeni rasmi,
 Mapengo hayo ni pamoja na lugha dhalilishi wakati wa uchaguzi zinazowakatisha tamaa wanawake kuwania nafasi za uongozi, uteuzi usiozingatia jinsia ndani ya vyama vya siasa, hofu na kutojiamini kwa baadhi ya wanawake wenye nia ya kugombea na ilani za vyama zisizozingatia jinsia. 
Mapengo mengine yaliyobainika ni pamoja na rushwa ya ngono inayotajwa kutumika wakati wa uchaguzi, rushwa ya kifedha, uchumi duni kwa wanawake wanaotaka kugombea na hivyo kupelekea kushindwa kufanya kampeni. 
Mapengo mengine ni mila na desturi kandamizi, zinazowazuia kabisa wanawake wasishiriki katika siasa.
 
Ndugu mgeni rasmi,
Ipo pia mitazamo hasi katika jamii kuwa mwanamke anapoingia katika siasa basi amejishushia heshima na hadhi yake kwani hakuumbwa kuwa kiongozi, hayo yote yanachangia kupunguza idadi ya wanawake viongozi. 
Mapengo mengine ni chama kuwa na mapendekezo na utaratibu binafsi kwa kumthamini mwanaume zaidi hususan katika majimbo ambayo chama kina matarajio makubwa ya ushindi.
 
Ndugu mgeni rasmi na viongozi wa dini, 
TAMWA inawasihi kuendelea kuhimiza umuhimu wa wanawake kushiriki siasa na katika ngazi za maamuzi kwani nyinyi mnaaminika katika jamii kutokana na wajibu wenu mkuu. 
Viongozi wa dini, mna nafasi kubwa katika kuhimiza jamii, kuondoa mila na mitazamo potofu inayochochea ushiriki duni wa wanawake katika siasa na katika ngazi za maamuzi. 
 
 Ndugu mgeni rasmi,
Viongozi wa dini wanategemewa kuhubiri Amani na mshikamano katika kipindi cha uchaguzi na amani hiyo itapatikana iwapo makundi yote maalum wakiwamo watu wenye ulemavu na wanawake, watashiriki kikamilifu katika uchaguzi. 
Ndugu mgeni rasmi.
 Kwa kuwa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa na mikataba mbalimbali ya amani,  hivyo basi, tunaomba yafuatayo yazingatiwe ili kuondoa vikwazo vyote vinazouia ushiriki wa wanawake katika siasa. 
 
1. Taasisi za dini kutoa elimu kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na kuondoa mitazamo yote potofu inayokwamisha ushiriki wao  na kutoa mafundisho katika Quran na Biblia yanayomuonyesha mwanamke kama shupavu na mleta mabadiliko ili kuwajengea wanawake kujiamini. 
 
2. Serikali  na viongozi wa dini kukemea na kuwachukulia hatua  wanaotoa lugha dhalilishi  kwa wagombea wanawake wakati wa uchaguzi.
 
3. Vyama vya Siasa vitambue kwamba vina wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha haki na usawa wa Wanawake ndani ya vyama vyao na katika jamii kwa ujumla, kwa kuwa Wanawake ndiyo kundi kubwa la wapiga kura Tanzania. 
 
4. Vyama vya siasa vizingatie mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa kuzingatia mrengo wa jinsia, kama Sheria Mpya ya Uchaguzi inavyoainisha.
 
5. Tunawaomba wanahabari kutumia kalamu zao kimaadili kwa kuepuka kuchochea lugha dhalilishi na kuidunisha taswira ya mwanamke katika jamii. 
 
6. Vyombo vya vya habari na wanahabari wanapaswa kupaza sauti zao kuhimiza ushiriki wa wanawake katika siasa na kulinda utu wake ili kuleta Amani na ushiriki kamilifu katika uchaguzi.
 
7. Wanawake waondoe dhana chonganishi zinazoenezwa kuwa hawapendani na hawawezi bali waendelee kusimama imara na kujitokeza kwa wingi katika chaguzi zijazo.
 
TAMWA tunaliombea Taifa likatawaliwe na upendo, Amani na mshikamano katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 28.
 Mungu ibariki Tanzania!
 
Rose Reuben.
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA.

Search