Press Release

TAMWA yaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Oktoba 11, 2020, Dar Es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kinaungana na watanzania, pamoja na watu wote ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. 
Kauli mbiu kitaifa kwa mwaka huu, inasema; Tumuwezeshe mtoto wa kike, kujenga taifa lenye usawa na kimataifa, kauli mbiu inasema: Sauti yangu, ni mustakabali wetu wa usawa.’ 
 
Kila mwaka ifikapo Oktoba 11, dunia huadhimisha siku hii ili kukumbushana madhila wanayopitia watoto wa kike na kuikumbusha jamii nguvu iliyomo kwa watoto hao.
Kwa mfano ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto(UNICEF) inaeleza kuwa watoto wa kike milioni 12 huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 kila mwaka?
 
Watoto wa kike takribani milioni 6 hadi 17 duniani kote hawajapata nafasi ya kwenda shule na inaelezwa kuwa watoto wa kike milioni 15 duniani, wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19 wameathirika kisaikolojia kutokana na manyanyaso ya ukatili wa kijinsia, ikiwamo kubakwa, vipigo na udhalilishaji wa kingono.  
Takwimu zinazojitokeza zinaonyesha kuwa tangu kuzuka kwa COVID-19, unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana (VAWG), na hasa unyanyasaji wa nyumbani, umeongezeka kwa kasi.
 
TAMWA ni shirika lisilo la kiserikali, lilioanzishwa mwaka 1987  kwa lengo la kutetea haki na ustawi wa wanawake na watoto, kupitia vyombo vya habari hivyo basi, wakati tunaadhimisha siku hii, tunaiasa jamii kuacha mifumo yote inayomkandamiza mtoto wa kike na badala yake tunahimiza taifa lenye amani,  linalozingatia ulinzi kwa watoto wa jinsia zote. 
 
Kupitia miradi mbalimbali tuliyofanya, TAMWA imebaini kuwepo kwa mifumo kandamizi kwa watoto wa kike, mifumo hiyo imepelekea baadhi ya jamii kukumbatia vitendo vya   ubakaji, ulawiti, ndoa za utotoni, manyanyaso kutoka ndani ya familia, kunyimwa haki ya kupata elimu na kugubikwa na mzigo wa majukumu ya kazi za nyumbani. 
 
Changamoto hizi na nyingine nyingi, zimechangia mtoto wa kike kukosa fursa ya elimu, kuathirika na maradhi, kuathirika kisaikolojia na kukosa nafasi yake ya kufurahia utoto wao kutokana na mimba za utotoni na ndoa za utotoni. 
 
Taifa lenye amani ni lile linalothamini haki za watoto, ikiwamo haki ya kuishi kwa furaha, kupata huduma za msingi ikiwemo huduma ya afya, elimu na amani. 
 
Kwa mujibu wa takwimu za madawati ya jinsia ya hapa nchini imebainika kuwa mimba za utotoni ziliongezeka kwa kasi wakati wa likizo ya miezi mitatu  mwaka huu iliyosababishwa na mlipuko wa virusi vya corona. 
Hivyo basi, TAMWA inaiomba serikali kuandaa utaratibu wa ulinzi, utoaji taarifa na ufuatiliaji kwa watoto hasa wakati wa dharura za milipuko ya magonjwa au majanga kama Covid-19 ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika.
 
Wakati huo huo takwimu za uhalifu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2016 jumla ya kesi 10,551 za uhalifu dhidi ya watoto ziliripotiwa katika vituo vya polisi, ukilinganisha na kesi 9,541 kuanzia Januari hadi Desemba 2015. Uhalifu huo ni pamoja na ubakaji, utelekezaji wa watoto, wizi wa watoto, ukeketaji na mashambulio ya kudhuru mwili.
 
“TAMWA tunaomba wazazi, walezi na watoto wa kike,wanaofanyiwa ukatili, wavunje ukimya, kwani zipo asasi, taasisi na vyombo vya serikali ambavyo wanaweza kuvitumia kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia 
Ndiyo  maana kauli mbiu ya kimataifa ya mwaka huu inasema, sauti yako, ni mustakabali wetu wenye usawa. 
Tunasisitiza serikali ijenge mifumo imara ya utoaji taarifa ili tujue kwa kina sababu na kiwango cha ukatili huu. Kwa kufanya hivi tutapata mifumo bora ya kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto nchini .
 
Tukumbuke kuwa, watoto hawa, wakiwamo wa kike ni taifa la kesho, hivyo basi wanapoharibiwa misingi bora ya maisha, tunakwenda kuharibu mustakabali wa taifa, Joyce Shebe, Mwenyekiti wa TAMWA.
 
Hatutaweza kupata wafanyabishara, wakulima, mawaziri, wabunge, wakurugenzi na viongozi bora wanawake, iwapo watoto wa kike wa sasa  watabakwa, watapata mimba, wataozwa katika umri mdogo, watashambuliwa na kunyanyaswa. 
 
Tuna taarifa kuwa ukatili kwa watoto unafanywa na watu wa karibu sana, wapo wazazi, walezi wanaochochea au kuchangia kwa namna moja ama nyingine ukatili kwa watoto wa kike, ikiwamo kuwaozesha, kuwabaka, kuwaumiza miili yao na kuwazuia kupata elimu, tunakemea haya na tunataka serikali iendelee kuwachukulia  hatua kali wazazi/walezi wa aina hii, Shebe.
 
TAMWA Bado tunakumbusha umuhimu wa mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 tukiamini kuwa, mtoto wa kike mwenye umri chini ya miaka 18, bado hajapevuka vya kutosha kumudu majukumu ya ndoa na kubeba ujauzito. 
 Tunahimiza zaidi elimu kwa mtoto wa kike, fursa ya kusikilizwa, haki ya kupata huduma za afya na zaidi hasa mtoto wa kike na nafasi sawa na mtoto wa kiume, Shebe.
 
 Tunaipongeza serikali, chini ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa jitihada za ulinzi na afya kwa watoto wa kike Tanzania. 
TAMWA bado tunaishikilia kauli yetu isemayo: Mtoto wa mwenzio, ni wako, mlinde na nirudie kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema Sauti yangu, ni mustakabali wetu wa usawa.
 
Watoto pazeni sauti zenu mara tu mnapoona dalili za kufanyiwa ukatili.
 
Joyce Shebe
Mwenyekiti, TAMWA

Search