Septemba 3, 2021.
Dar Es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinampongeza Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe kwa kusimamia kidete masuala ya ukatili wa kijinsia yanayotokea wilayani humo.
Mchembe akitimiza majukumu yake ya kazi wilayani humo, ameweza kuibua ukatili unaofanywa na baadhi ya askari polisi wilayani humo, wanaodaiwa kuwashika sehemu za siri wasichana, kuwabaka, kuwapiga na kuwalazimisha kuwa na mahusiano ya kimapenzi.
Mchembe ambaye pia kisheria ndiyo mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya, amenukuliwa akisema wazi katika mkutano huo kuwa; Mimi kama Mkuu wa wilaya, unyanyasaji wa kijinsia Handeni, Hapana.
Mkuu huyo wa Wilaya alichukua hatua za kuitisha mkutano baada ya kuwepo kwa madai ya askari kuwapiga na kuwajeruhi wasichana wawili katika ukumbi wa starehe wilayani humo kwa kile kinachodaiwa walikataa kuwa na mahusiano na askari hao.
Katika mkutano huo walikuwepo wasichana ambao walitoa ushahidi wa wazi kuwa wanalazimishwa kuwa na mahusiano na askari na endapo wanawakataa basi wanawekwa mahabusu bila sababu ya msingi.
Mashahidi wengine katika mkutano huo wamesema kuwa baadhi ya askari polisi huingia kwenye kumbi za starehe na kuwapiga wasichana bila sababu anuwai yenye mashiko.
Kadhalika, DC Mchembe alisimamia kidete tukio la mwezi Agosti mwaka huu, la mtoto wa miaka 10 kubakwa mara kadhaa na kijana wa miaka 20 wilayani humo.
TAMWA tunaamini kwamba utendaji kazi wa namna hii unaofanywa na Mheshimiwa Mchembe, utasaidia kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia ambao umekuwa ukisababisha madhara makubwa ya kimwili na kiakili kwa watoto wa kike na wanawake.
Kadhalika, tunakemea vikali vitendo vya askari polisi kutumia madaraka yao vibaya na kufanya ukatili wa kijinsi kama huu.
Hakuna aliye juu ya sheria, na ndiyo maana askari wana dhamana ya kusimamia sheria hizi, lakini cha ajabu baadhi wamekuwa wa kwanza kuzivunja, Dkt Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA.
Dkt Reuben amesema ukatili wa namna hii sio tu unavunja haki za binadamu lakini pia ndicho chanzo cha madhara mengi ikiwamo mimba zisizotarajiwa, mimba za mapema, magonjwa ya kuambukiza na wakati mwingine madhara ya kimwili kama majeraha.
Polisi wasimamie maadili yao ya kulinda raia na mali zao, wasiwe washika bendera wa kuendeleza ukatili wa kijinsia, hakuna aliye juu ya sheria, amesema Dkt Reuben.
TAMWA tunaomba askari watakaobainika kufanya ukatili huo wachukuliwe hatua huku tukiendelea kumtia moyo Mheshimiwa Mchembe kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto wilayani humo.
Dkt Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA