Press Release

TAMWA YASIKITISHWA NA KIFO CHA MWANAHABARI BLANDINA SEMBU

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Dar es Salaam, Machi 29, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mwanahabari wa IPP Media, Blandina Sembu.
 
Taarifa ya Jeshi la Polisi inasema kuwa, mwili wa Sembu, aliyekuwa mtangazaji wa kipindi cha Wanawake, kinachorushwa na ITV, uliokotwa katika maeneo ya Bamaga usiku wa kuamkia Machi 28, hali ambayo inaonyesha utata wa mazingira ya kifo chake. 
 
TAMWA kimesikitishwa na tukio hilo lililompoteza mwanaharakati wa masuala ya wanawake, masuala ya watu wenye ulemavu na mwanahabari aliyeipenda kazi yake. 
 
"TAMWA ikiwa ni mdau mkuu wa wanahabari wanawake nchini , kimeguswa na tukio hilo na tunaziomba mamlaka husika kuchukua hatua za uchunguzi ili kujua undani wa kifo cha Sembu ikiwa kimesababishwa na watu basi hatua kali zichukuliwe kwa watekelezaji wa tukio hilo" Rose Reuben, Mkurugenzi wa TAMWA
 
TAMWA  itamkumbuka Sembu kwa mchango wake mkubwa katika masuala ya Ushiriki wa Wanawake katika Siasa na Uongozi kwani alikuwa ni mjumbe wa kamati ya  Muungano wa Ushiriki Tanzania iliyoangazia Ushiriki wa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana katika siasa na uongozi. 
 
 Kuondoka kwa Sembu ni pengo kubwa kwa tasnia ya habari, jumuiya za watu wenye ulemavu na pia katika jumuiya zinazotetea haki za wanawake nchini kwani alijitoa kwa dhati na alihakikisha anasemea haki za makundi hayo, pale inapobidi.
 
TAMWA inatoa salamu za pole kwa wanafamilia wote wa Blandina Sembu, Watendaji na Wanahabari wa IPP Media, wanaharakati wa masuala ya jinsia, watu wenye ulemavu na wanahabari  wote  nchini.
 
Rose Reuben,
Mkurugenzi Mtendaji- TAMWA.

Search