Dar es Salaam, Oktoba 1, 2020. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kina furaha kubwa kuutambulisha umma wa Watanzania, kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa ‘Wanawake Wanaweza’, unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wanawake (UN-Women).
Hii ni fursa adhimu kwa TAMWA ambayo baadhi ya malengo yake makuu ni utetezi wa haki za wanawake na watoto, kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, kuondoa mifumo kandamizi inayochochoea ukatili kwa makundi hayo maalum, kwa kutumia vyombo vya habari.
Hivyo basi jukumu la TAMWA katika mradi huu ni kuongeza uelewa kwa umma kuhusu umuhimu wa ushiriki wa Wanawake katika siasa na katika uongozi na madhara ya magonjwa ya mlipuko kama Covid-19 kwa wanawake na wasichana.
“Katika kufanikisha lengo kuu la mradi huu, TAMWA itawajengea uwezo wanahabari katika kuripoti habari za jinsia na ufuatiliaji wa ushiriki wa wanawake katika uongozi na siasa,Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji, TAMWA.
Kadhalika ili kufanikisha hayo, TAMWA itaendesha midahalo ya kihabari kwa ajili ya kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
Mikoa 16 ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara, Wilaya 112 za mikoa hiyo na kata 458, ndiyo maeneo yatakayotumika kama sampuli ya utekelezaji wa malengo ya mradi huu.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, kuwa malengo ya mradi huu yatatimizwa kwa kutumia vyombo vya habari, hivyo basi TAMWA itashirikiana na wadau wake wakuu ambao ni vyombo vya habari, zikiwamo runinga 10, redio za kijamii 50, radio za masafa marefu 10 , magazeti 20 na mitandao ya kijamii, ili kuifikia jamii.
TAMWA inatambua kuwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi (hasa ya kisiasa) bado ni mdogo, hali ambayo inakinzana na azma ya kujenga jamii isiyokuwa na ubaguzi kama ilivyobainishwa kwenye dira ya Taifa 2025, Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, pamoja na sheria mbalimbali za nchi.
Kwa mfano, ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC: 2016) inaonyesha kuwa, asilimia 17 ya mawaziri ni wanawake, makatibu wakuu wanawake ni asilimia 11, wakuu wa mikoa ni asilimia 23, wakuu wa wilaya ni asilimia 28 na hii inaonyesha kuwa bado nafasi ya mwanamke katika ngazi za uongozi ni mdogo.
“Hata hivyo, bado tunaupongeza uongozi wa awamu ya tano, kwa mara ya kwanza alichaguliwa Makamu wa Rais mwanamke nchini, Mama Samia Suluhu Hassan Reuben
Hivyo basi katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi huu, TAMWA, inatarajia kutumia nyenzo zake muhimu kuongeza uelewa kwa jamii na kuhakikisha wanawake wanaonekana kuwa viongozi halali na madhubuti katika jamii yetu Reuben
Kama tulivyoainisha awali, kuwa wadau ni muhimu katika utekelezaji wa mradi huu, hivyo wadau wengine tutakaowashirikisha ni Chuo Kikuu cha Dar es Salam, kitivo cha Sayansi ya Jamii, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Shirika la Wanasheria Wanawake na Maendeleo Afrika, (WILDAF), Viongozi wa dini na Mtandao wa radio za kijamii nchini (TADIO), Wizara ya Habari na Wizara ya Afya.
Wengine ni Mtandao wa Wanawake Viongozi Afrika (AWLN) na machampioni wa GEWE, Viongozi wa kimila, Kituo cha Demokrasia nchini(TCD).
Hawa wote ni wadau ambao TAMWA itafanya nao kazi wakati wa utekelezaji wa mradi huu, na kwa nafasi yao watakuwa na mengi ya kuishirikisha TAMWA na umoja huu ndicho chanzo cha mafanikio ya utekelezaji wa mradi huu, Rose Reuben
TAMWA ambayo kiini chake ni wanahabari, inatarajia kushirikiana na vyombo vya habari ili kufikisha hii ajenda ya ushiriki wa wanawake katika siasa na katika uongozi kwa jamii, tukiamini kwamba, wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii.
Viongozi wa dini, taasisi za habari, taasisi za jinsia, ambazo TAMWA inakwenda kushirikiana nazo, ni nguzo muhimu katika kufanikisha adhma kuu ya mradi huu,Reuben.
Bila kuwasahau viongozi wa kimila na viongozi wa mikoa, wilaya na kata mbalimbali ambazo tutazifikia, TAMWA inatarajia ushirikiano mkubwa kutoka kwao.
Mkurugenzi Mtendaji
Rose Reuben
TAMWA.