News/Stories

COVID-19 NA USALAMA WA WANAWAKE, WATOTO NCHINI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Aprili 7, 2020. Wakati dunia nzima ikigubikwa na mshtuko kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinapenda kuihadharisha jamii juu ya ongezeko la ukatili wa wanawake na watoto unaoweza kukithiri wakati wa janga la ugonjwa huu.

“Watoto wapo nyumbani wakati huu ambapo serikali imezifunga shule, lakini iwapo wazazi na walezi hawatakuwa makini basi huenda wakaathirika na ubakaji na mimba za utotoni katika kipindi hiki ambacho macho na masikio yapo katika kudhibiti virusi vya Corona,”

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto(UNICEF) linasema, ukatili wa watoto aghalabu hufanyika nyumbani, mtoto akielekea au akitoka shule wakati anapokuwa peke yake bila msaada.

TAMWA inaipongeza serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kufunga shule ili kupunguza msongamano unaoweza kusababisha maambukizi, hata hivyo ni muhimu kuihadharisha jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na ule wa watoto unaoweza kuongezeka wakati huu.

Endapo wazazi/walezi hawatawasimamia vizuri watoto katika kipindi hiki cha siku 30 zilizotolewa na serikali kupitia Waziri Mkuu, basi tunaweza kutengeneza kizazi kingine kilichoathirika na ukatili wa aina mbalimbali ikiwamo ubakaji, ulawiti na mimba zisizotarajiwa.

Kwa mfano, Ripoti ya UNICEF 2016 inaonyesha kuwa, wakati wa mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi 2014 hadi 2016, ulisababisha ongezeko la ajira kwa watoto, ukatili kwa wanawake na watoto na mimba za utotoni. Kwa mfano, mimba za utotoni nchini Sierra Leone ziliongezeka kufikia 14,000 kutoka 7,000.

“Ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto na virusi vya Corona lakini wakati huo huo tuangalie madhara wanayoweza kuyapata watoto wa kike na wa kiume wanapokuwa nyumbani au mitaani”

Tunapaswa kujiuliza iwapo watoto wetu wapo salama wawapo nyumbani au mitaani wanapotembea wakati huu wa likizo ndefu. Je, Mafataki hawawanyemelei? Je ndugu na jamaa wanaobaki na watoto hawa wanawalinda au wanawaharibu? Je watoto hawa hawatakuwa katika hatari ya kuozwa mapema?

Si hivyo tu, janga hili la Corona linaathiri zaidi wanawake kwani shule zinapofungwa, mzigo mkubwa wa malezi unawaangukia kinamama nyumbani ambao ndiyo walezi wakuu wa familia.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) zinaonyesha kuwa, dunia nzima, asilimia 70 ya watoa huduma za jamii na za afya ni wanawake. Majukumu haya huwaweka mstari wa mbele katika utoaji wa huduma, Je katika janga hili la Covid-19, wanawake wanalindwa ipasavyo wasidhurike?

TAMWA inaiomba serikali, wadau na watunga sera kwanza, kutosahau hatari nyingine zinazoweza kuwapata wanawake na watoto katika kipindi cha janga la Covid-19.

Pili, wadau wa afya, elimu na watoto kutoa mafunzo kuhusu namna ya kujilinda na ya kuripoti kuhusu ukatili kwa watoto wakati huu wa mlipuko.

Tatu, kuongeza upatikanaji wa taarifa na misaada mingine kwa watoto.

Nne, kubuni mfumo wa kuwapa watoto elimu wawapo nyumbani.

Tano, wahudumu wa afya wanawake wawekewe mazingira salama ya kutoa huduma ili wasiathirike.

Sita, wazazi na walezi kuimarisha ulinzi na kuzuia matembezi yasiyo ya lazima kwa watoto.

Rose Reuben

Mkurugenzi Mtendaji,

TAMWA.

Latest News and Stories

Search