News/Stories

CRDB , TAMWA yawataka wajasiriamali mbogamboga kuepuka mikopo ‘hatarishi’

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Dar es Salaam. Wajasiriamali wadogo wa mbogamboga, wamepewa elimu ya ujasiriamali na kukumbushwa kuepuka mikopo ‘hatarishi’ badala yake wakope kwa malengo.
Akizungumza na katika warsha ya wajasiriamali wanawake wa mbogamboga jijini Dar es Salaam, Meneja wa Elimu na Usimamizi, wa CRDB Foundation Joshua Mwakalobo amesema, wajasiriamali wengi wanakopa bila malengo na kuishi kwenye mikopo inayowasababishia madhara lukuki.
“Leo tunamzungumzia mama mboga mboga, ambaye akienda kukopa anakosa, sababu zinazochagiza kukosa mkopo ni kukosa dhamana. CRDB Foundation, iliamua kumsaidia mjasiriamali mdogo bila kujali vigezo vya msingi. Kwa hiyo wewe mjasiriamali, hauna TIN namba, hauna leseni unaweza kushikwa mkono na kupata mkopo” amesema Mwakalobo,
Mwakalobo ameyasema hayo wakati wa warsha ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) kwa kushirikiana na Benkiy a CRDB Foundation, ikilenga kumtambau mjasiriamali mwanamke wa mbogamboga.
Mwakalobo amesema, kabla ya kuchukua mkopo kuna mambo makubwa muhimu ya kujiuliza kabla ya kuchukua mkopo. Kwanza,Kwa nini ninakopa.
“Cha muhimu tunakopa kwa sababu ya kuongeza mtaji kwenye biashara na si kukopa kwa sababu mkopo una riba ndogo. Tunazungumzia uhitaji wa wewe kukopa,” amesema Mwakalobo
Kwa mujibu wa Mwakalobo kwa asilimia kubwa wanaume ndio wanaomiliki ardhi na hivyo asilimia kubwa ya wanawake wanakosa dhamana ya mikopo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAMWA, Dr Rose Reuben alisemaTAMWA kwa kushirikiana CRDB Bank Foundation inatambua na kuthamini mchango wa mwanamke mjasiriamali mdogo wa mboga mboga ambaye amekuwa akifanya juhudi za kujikwamua kiuchumi kwa biashara hiyo.
TAMWA na CRDB tunatambua kuwa wajasiriamali wadogo wapo wa aina nyingi, lakini leo katika kuadhimisha mwezi huu wa wanawake, tunafuraha kuwatambua wajasiriamali wanawake wa mboga na matunda kwa kuonesha uthubutu katika kujikwamua kiuchumi.
TAMWA katika tamko imeeleza kuwa kumtambua mwanamke mjasiriamali wa mboga, kunalenga kuibua fursa, changamoto na kuleta suluhisho zitakazowezesha kuwainua wanawake kiuchumi, huku tukiendelea kupigania haki zao na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Search