News/Stories

TAMKO LA ASASI ZA WANAWAKE KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

TAMKO LA ASASI ZA WANAWAKE KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Dar –Es- Salaam, Oktoba 23, 2025.
Wakati Watanzania wakielekea katika tukio la kikatiba la kupiga kura mnamo Oktoba 29, muunganiko wa asasi za kiraia zinazotetea makundi maalum ikiwamo wanawake, watoto na vijana wanawake, tumeungana kwa pamoja kuhimiza umma kuhusu ajenda muhimu ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi sambamba na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika upigaji kura siku ya Oktoba 29 mwaka huu.

Ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ni miongoni mwa vipaumbele vya asasi za kiraia zenye mrengo wa jinsia. Kwa sababu tunaamini wakiwapo viongozi wanawake, kutakuwa na hatua mahsusi katika kuongeza kipato na maendeleo ya mwanamke.

Hivyo basi sisi muunganiko wa asasi za kiraia, tunawahakikishia kuwa tunakwenda kutimiza wajibu wetu wa kikatiba wa kupiga kura na kadhalika tunahimiza wanawake kwenda kushiriki katika mchakato wa kikatiba wa kupiga kura, ili tunapokwenda kuwachagua viongozi wetu, basi tuwatwike mzigo wa mambo ya msingi yanayowahusu wanawake .

Viongozi hawa tutakaowachagua, tunaamini kuwa baada ya mchakato huo, tutawatwika madai yetu ya kimaendeleo yanayowahusu wanawake, watoto, wanawake vijana na watu wenye ulemavu na ajenda nyinginezo za mrengo wa jinsia.

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika ambazo zimepiga hatua katika ajenda ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi. Kwa mara ya kwanza Tanzania imepata kiongozi mkuu wa nchi mwanamke, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye pia anawania kiti hicho cha urais kwa tiketi ya CCM.

Kadhalika, mwaka huu kumekuwa na wagombea wengine wanawake wa urais, akiwemo Saumu Rashid kutoka UDP na Mwajuma Mirambo –UMD.

Kwa upande wa wagombea wenza wa urais kutoka vyama vingine ni pamoja na Eveline Wilbard Munis (NCCR), Husna Mohamed Abdallah (CUF), Aziza Haji Selemani (D. MAKINI), Amani Selemani Mzee (TLP), Chausiku Khatibu Mohamed (NLD), Sakia Mussa Debwa (SAU), Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja (CHAUMA).

Hii ni hatua kubwa ya kidemokrasia kwa Tanzania na kwa ajenda ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.

Tunapokaribia uchaguzi mkuu, tunapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa mwanamke kiongozi anaposhika madaraka asihukumiwe kwa jinsia yake, bali kwa uwezo, uzoefu na dira yake ya maendeleo.

Ikumbukwe kuwa uongozi wa mwanamke si tishio bali ni nyenzo ya kuimarisha demokrasia jumuishi, yenye kusikiliza na kutenda kwa manufaa ya wote.

Tunapenda kuikumbusha jamii kuwa katika kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi, ni muhimu kuepuka lugha za kejeli, udhalilishaji na mashambulizi ya kibinafsi — hasa kwa misingi ya kijinsia. Badala yake, mjadala wa kisiasa ujikite katika sera, ilani, na hoja zenye kujenga taifa.

Wanawake wanaowania nafasi kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais, wasibezwe, wasitukanwe, na tunakemea vikali lugha dhalili zinazotweza utu kwa wanawake wanasiasa na viongozi wengine wanawake.

Bado tunaamini kuwa kwa kumpata Rais mwanamke Tanzania imepiga hatua kubwa kupitia yeye katika kutekeleza Dira ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5) inayosisitiza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika maamuzi.

Kupitia Rais huyu mwanamke tumeona sheria kadhaa zikibadilishwa ikiwamo ya vyama vya siasa na hata miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya afya.

Asasi za kiraia zinasimama imara katika kuhakikisha kuwa mafanikio haya yanaendelezwa, si kwa maneno tu bali kwa vitendo.

Ushiriki wa wanawake katika siasa unaongeza uwajibikaji, uwazi, na ustawi wa kijamii, kwa kuwa tafiti nyingi zinaonesha kwamba wanawake viongozi wanapendelea sera zinazogusa elimu, afya, haki za watoto, na usawa wa kiuchumi. Kama zipo changamoto kupitia uongozi wake basi si muda wa kumkashifu kwa kupitia jinsia yake.

Tunapenda pia kuikumbusha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa, na wadau wote kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanakuwa salama, jumuishi, na huru dhidi ya vitisho, udhalilishaji, na ukatili wa kijinsia, ambao mara nyingi huwakatisha tamaa wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa.

Tunatoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake kuratibu midahalo, makala, na mijadala inayojenga uelewa wa umma juu ya uwezo na mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.

Kwa muktadha huu, tunasema: “Uongozi bora hauna jinsia — una maadili, dira, na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi.”

Tunaamini kuwa taifa lenye usawa wa kijinsia katika uongozi ni taifa lenye amani, ustawi, na maendeleo endelevu.Tanzania ni yetu sote — wanawake na wanaume wanapaswa kushiriki kwa usawa katika kuijenga.

Imetolewa na:
Muunganiko wa Asasi za Wanawake na Watetezi wa Usawa wa Kijinsia – Tanzania

(Oktoba 23, 2025 – Dar es Salaam)

  1. Ulingo Wanawake

  2. Women Walfare Tanzania

  3. TAMWA

  4. Binti Makini-

  5. WAJIKI-

  6. WILDAF-

  7. WFT-

  8. Young and Alive

  9. Generation Act

  10. TAWIA

Latest News and Stories

Search