Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Reuben ametwaa tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ iliyotolewa na World Women Leaders Congress (WWLC) Juni 19 jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo zilitolewa kwa wanawake viongozi wa Afrika Mashariki walioleta mabadiliko katika jamii, walioibua vipaji, wanawake mifano ya kuigwa na wenye uthubutu kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ya binafsi na serikali kutoka katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Wanawake viongozi kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi walitunukiwa tuzo hizo kutokana na vigezo vya ushindi vilivyowekwa.
Akizungumzia tuzo hiyo, Reuben amesema tuzo hiyo inawatia moyo wanawake wengine kufanya bidii zaidi kwani kuna watu wanawakubali na wanaweza kuzitunuku kazi zao.
“Wanawake wanaweza kuwa viongozi wazuri, tuzo hii inaeleza kuwa uongozi wa wanawake unakubalika, hii ni tuzo ya dunia, kumbe ulimwengu umekubali kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi,” amesema
Ameongeza: “Jamii kwa ujumla ikubali kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi. Wanahabari wafanye kazi zao kwa kujiamini, kazi zao zikajulikana na wasikatisshwe tamaa na kitu chochote.”
Wengine waliotwaa tuzo hizo kutoka Tanzania ni Emma Kawawa, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Tanzania Women CEO’S Roundtable.
Tuzo hizo zinatolewa ili kuhamasisha wanawake viongozi katika sekta za umma na binafsi, kutambua mafanikio ya wanawake kikanda na kidunia pamoja na kuwatia moyo wanawake vijana kushika nafasi za mbalimbali za uongozi.