Mwandishi Wetu, TAMWA Dar es Salaam. Viongozi wapya wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) wamefanya ziara katika vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha.
Viongozi hao, Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben na Mwenyekiti wa chama hicho, Joyce Shebe walitembelea vyombo vya habari kumi ikiwa ni awamu ya kwanza ya ziara hiyo.
Miongoni mwa vyombo vya habari vilivyotembelewa na viongozi hao wa TAMWA ni pamoja na Tumaini Media, Upendo Media, Radio Maria ,Star TV, Channel Ten, EFM Radio, Times FM Radio, Azam Media na kampuni ya magazeti ya Mwananchi Communication na The Citizen na New Habari Co-operation.
Shebe alisema lengo la ziara hiyo ni viongozi hao wapya wa TAMWA kujitambulisha kwa vyombo vya Habari ili kuimarisha uhusiano, kuhamasisha waandishi wanawake kujiunga na chama hicho cha kitaaluma.
“Ongezeko la wanachama wapya ndani ya TAMWA litawasaidia kunufaika na nafasi za kitaaluma kupata mikopo ya kujiendeleza na masomo ya elimu ya juu kama Shahada na kuhudhuria makongamano ya kitaaluma, fursa za mafunzo ya kitaalum,”alisema Shebe
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben alipongeza jitihada za baadhi ya vyombo vya habari katika kutunga sera za kuimarisha usawa wa kijinsia na kutoa nafasi za uongozi kwenye vyombo vyao.
Kadhalika viongozi hao walipongeza jitihada za baadhi ya vyombo vya habari katika kutunga sera za kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyumba vya habari.
TAMWA ni shirikisho lisilo la kiserikali lililoanzishwa miaka 31 iliyopita kwa lengo la kutetea haki na ustawi wa wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari.
Vigezo vya kujiunga na TAMWA ni pamoja na kuwa mwanamke mwanahabari, shahada ya mawasiliano ya umma au ya habari na uzoefu wa kazi ya uandishi wa miaka mitatu.
Katika ziara hiyo TAMWA imekutana na kuzungumza na viongozi wa vyombo vya habari kama wakurugenzi na wahariri wakuu, na kujifunza mambo mengi yanayoendelea ndani ya vyumba vya habari nchini.