News/Stories

TAANnet - KUADHUAMISHA SIKU YA KUTOKUNYWA POMBE DUNIANI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Mtandao wa Wadau unaopambana na unywaji pombe kupita kiasi  – TAAnet, leo tarehe 3Machi, 2018 unaungana na watanzania wote kuadhimisha siku ya kutokunywa pombe duniani ambayo kwa mara ya kwanza yanafanyika kitaifa mkoani  Dodoma.

Maadhimisho hayo yatakayoongozwa na kauli mbiu ya mwaka huu ya “Maendeleo ya Viwanda yataletwa na Udhibiti wa Unywaji Pombe kupita kiasi”  yataanza kwa maandamano yatakayopokelewa na Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa mkoa huo Dr. Bilinith Mahenge saa mbili asubuhi kwenye viwanja vya Chuo cha Biblia Dodoma

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Watu zaidi ya milioni 3 walifariki kutokana na matumizi mabaya ya pombe mwaka 2016. Zaidi ya robo tatu ya vifo hivi vilikuwa ni vya wanaume. Kwa ujumla, matumizi mabaya ya pombe husababisha zaidi ya asilimia 5 ya mzigo wa magonjwa duniani.

Matumizi ya pombe na athari zake ni tatizo linalozidi kukua nchini Tanzania, na linapaswa kudhibitiwa haraka iwezekanavyo. Ongezeko hili la unywaji pombe katika jamii ya watanzania TAAnet inazikumbusha  taasisi husika pamoja na Serikali kuangalia kwa hakara namna ya kudhibiti tabia hiyo ili kunusuru maisha ya vijana yanayoendelea kuharibika kila siku.

Kama wadau wa kupambana na madhara ya unywaji pombe , tungependa kuona watunga sera wanalitafutia tatizo hili ufumbuzi kwa  kuwa ufumbuzi wa ubunifu ambao utaokoa maisha, kama vile kutokomeza unywaji pombe kupindukia.

Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambazo bado haina sera/muongozo  wa pombe ukilingalinisha na Nchi jirani kama Kenya, Malawi huku Uganda wakiwa njiani kumalizia mkakati wa sera yao ya pombe.

TAAnet inapendekeza kupitiwa kwa sheria na kuweka masharti kuhusiana na matangazo, uuzaji na udhamini wa pombe pamoja na kuonyeshwa kwa onyo la athari za pombe   kwenye matangazo ya vilevi ili kupunguza matumizi yake kwa jamii.

TAAnet inaamini kwamba, endapo kutakuwa na sera ya kudhibiti matumizi mabaya ya pombe, wanaume watawajibika zaidi na kuacha matumizi yaliyopitiza ya vileo, yanayochangia unyanyasaji wa kijinsia, na badala yake kuchangia ustawi wa familia na kukuza maendeleo kwenye jamii na katika Taifa kwa ujumla.

Kupunguza matumizi mabaya ya pombe kutasaidia kufikia malengo kadhaa yanayohusiana na afya ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), ikiwa ni pamoja na  afya ya uzazi na watoto, magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukizwa na magonjwa ya akili, majeraha na sumu. 

Edda sanga

Mkurugenzi Mtendaji

Latest News and Stories

Search