News/Stories

TAMWA YAKEMEA MAUAJI YA WANAWAKE NA WATOTO NCHINI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinaungana na taasisi nyingine nchini kulaani vikali matukio ya mauaji ya wanawake na watoto yaliyotokea hivi karibuni hapa nchini.

Kwa kadri siku zinavyoendelea mauaji ya wanawake na watoto yanayotokana na sababu mbalimbali yameripotiwa kutokea sehemu mbalimbali hasa katika maeneo ya Njombe, Rombo, Mto wa Mbu na Simiyu. 

Pamoja na matukio ya mauaji ya watoto Njombe na Simiyu, hivi karibuni  kumetokea mauaji ya wanawake Arusha na mikoa mingine.

TAMWA tunasikitishwa na mauaji hayo na tunaikumbusha jamii kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi kulingana na sheria na taratibu za nchi yetu. 

Hivyo tukiwa wadau wanaosimamia haki za wanawake na watoto tunakemea haya na kuwataka wadau wengine kuanzia ngazi ya familia hadi serikalini kuwalinda watoto na kuhakikisha kuwa migogoro ya kifamilia inamalizwa kwa mazungumzo ya amani. 

Tumeona na tunapongeza juhudi kubwa zilizofanywa na vyombo vya usalama nchini lakini pamoja na juhudi hizo cha kujiuliza ni kuwa kwanini bado matukio haya ya mauaji yameendelea kuripotiwasiku baada ya siku? 

Tunachelea kwamba, matukio haya yasipoundiwa mifumo ya muda mrefu ili kuyakomesha kabisa, basi tutaendelea kupoteza kinamama na watoto ambao kimsingi ni nguvu kazi ya Taifa.

TAMWA tunapendekeza uwepo wa mfumo endelevu utakaohusisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi, vyombo vya usalama na kampuni za simu kuwezesha waathirika kutoa taarifa za dalili zozote za ukatili kabla haujatokea. 

TAMWA tunaungana na familia za waathirika wa matukio haya tukiwatakia faraja katika kipindi hiki kigumu. 

 

Rose Reuben

Mkurugenzi Mtendaji

TAMWA

 

Latest News and Stories

Search