Dar es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA), kinajumuika na Waafrika wote kumpongeza Rais mpya wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde.
Sahle-work anakuwa Rais wa kwanza mwanamke kuiongoza Ethiopia baada ya kuteuliwa na bunge la nchi hiyo jana Octoba 25.
Taarifa iliyotumwa na TAMWA leo Oktoba 26, imesema Rais Sahle-Work, anaendelea kupeperusha bendera za wanawake waliowahi kuwa marais Afrika.
Marais wengine waliowahi kushika nyadhifa hizo ni pamoja na Ellen Johnson Sirleaf, (Liberia), Joyce Banda (Malawi) na Ameenah Gurib-Fakim, aliyewahi kuwa Rais wa Mauritius.
“Kuteuliwa kwake ni chachu ya mabadiliko zaidi kwa wanawake ambao awali hawakuaminika wanaweza kuongoza,”imesema taarifa hiyo ya TAMWA
“TAMWA, inaendelea kuhamasisha kuwepo kwa uwakilishi wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi hapa nchini,”imesema taarifa hiyo.
Katika moja ya hotuba zake Sahle-Work amesema; “Kukosekana kwa amani kwanza kunawaathiri wanawake, hivyo wakati wa uongozi wangu nahamasisha zaidi nafasi za wanawake katika kuleta amani.”