Godwin Assenga, Tamwa.
Dar es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) kinatoa pongezi za dhati kwa mwanaharakati wa masuala ya haki za binadamu na Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebecca Gyumi kwa kushinda tuzo ya Umoja wa Mataifa katika kipengele cha utetezi wa haki za binadamu kwa mwaka 2018.
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda alimtangaza Gyumi pamoja na washindi wengine, Octoba 25 mwaka huu.
Washindi wengine ni marehemu Asma Jahangir , mwanasheria wa Haki za Binadamu wa Pakistan, Joenia Wapichana, mwanaharakati wa haki za watu wa jamii za pembezoni wa Brazil na taasisi ya Front Line Defenders, inayojihusisha na ulinzi wa haki za binadamu, Ireland.
“TAMWA inaamini kuwa, ushindi wa Gyumi ni ushindi kwa watoto na wanawake wote nchini ambao haki zao zimekuwa zikikandamizwa,” anasema Edda Sanga, Mkurugenzi, TAMWA.
Wengine waliowahi kushinda tuzo hii miaka ya nyuma ni pamoja na aliyewahi kuwa mke wa Rais wa Marekani, Franklin Roosevelt, Eleanor Roosevelt, mwanaharakati wa haki za binadamu na kiongozi wa dini wa Marekani, Martin Luther King.
Wengine ni aliyewahi kuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu(ICRC)
Sherehe za utoaji wa tuzo hizi zitafanyika Desemba huko New York, Marekani.