Florence Majani, TAMWA.
Ruangwa, Lindi. Ni Januari 17 mwaka 2018, saa sita mchana. Kundi la wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za Nambilanje, wameketi mbele ya walimu wao, wakijadiliana kuhusu mila na desturi zinazokwamisha maendeleo na kuchochea mimba za utotoni katika kata hiyo.
Walimu walikuwa kimya wakifuatilia kwa umakini majadiliano hayo. Wanafunzi nao hawakuwa na hofu bali walitoa ya moyoni na kueleza kinagaubaga kinachoendelea majumbani.
Majadiliano hayo yaliandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) ili kuangalia mila na desturi zinazochochea mimba za utotoni na ukatili kwa wanawake na watoto.
Wanafunzi hao waliweka bayana kuwa, baadhi ya wazazi ndicho chanzo cha wao kufeli kwani huwalazimisha kufeli na kuwataka kuandika ‘madudu’ ili wasiendelee na masomo ya sekondari.
Mwanafunzi wa kidato cha nne, shule ya Sekondari Nambilanje, Zahara Chigope anaweka bayana kuwa wapo wanafunzi wenzake ambao wanashurutishwa na wazazi waandike ‘madudu’ kwenye mitihani ya taifa ili wasiendelee na masomo ya sekondari.
“Mzazi wake alimwambia aandike 11111 kila swali, ili afeli na asiendelee na sekondari,” alisema.
Alisema hata kwa wale wanaofaulu darasa la saba, wapo wazazi wanaokataa kwa makusudi kuwapeleka shule wakidai hawajalipwa fedha za korosho lakini kimsingi, ni ujanja tu ili wasiendelee na masomo.
Zahara alisema mwenzao mmoja aliyekuwa anafaulu vizuri kwenye masomo wakati wakiwa shule ya msingi, alifeli na alipomdodosa imekuwaje, ndipo alipomtobolea siri hiyo kuwa aliambiwa na mama yake aaandike ‘madudu.’
“Kweli alifeli kwa sababu aliniambia aliandika 11111 katika kila swali na sasa hivi yupo mitaani amezaa na wala hajaolewa,” alisema
Mwanafunzi mwingine wa kidato cha tatu wa shule hiyo, Zena Mitawa anasema mwenzao aliyetakiwa kuwa nao kidato cha tatu, alifeli darasa la saba kutokana na ushauri wa mama yake.
“Alikuwa anatuambia hata kabla hatujafanya mtihani wa taifa kuwa, mama yake hataki aendelee na shule kwani tayari yupo mwanaume wa kumuoa. Kweli matokeo yalipotoka, hakufaulu na sasa ameolewa huko Lindi mjini,” anasema.
Mwanafunzi mwingine, Nasma Kumkana, alisema suala la wazazi kuwashawishi wanafunzi wafeli kwa makusudi ni kubwa na wanalisikia kutoka kwa wanafunzi wenzao.
“Sio hivyo tu, hata baadhi ya wazazi tunawasikia wanasema bora mtoto afeli kwa sababu hawana hela za kumhudumia atakapoingia sekondari, hata wakiambiwa elimu ni bure watasema hawana fedha za sare za shule,” anasema
Nasma anasema mila hizo zinaambatana na ile ya baadhi ya wazazi kumshauri mtoto atafute mboga kwa jasho lake.
“Hii ina maana kwamba, mama anamwambia mtoto leo zamu yako kutafuta mboga, kwa maana nyingine, mtoto wa kike anapewa ruhusa ya kuwa na mwanaume ili apate fedha ya kusaidia familia,” anasema.
Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nambilanje, Charles Chitawala anasema tatizo hilo ni kubwa kwa kata ya Nambilanje na maeneo mengine ya Ruangwa.
“Sisi kama viongozi suala hilo linatuudhi, inabidi tutoe elimu, ili tabia hizo waziache. Ilifikia mahali ikabidi tuitishe vikao vya wazazi na wazazi wajaze mikataba,” anasema.
Anasema mwaka 2018, wazazi walijaza mikataba na kukubaliana kuwa iwapo mzazi atabainika kuwa alimshauri au kumlazimisha mwanafunzi kufeli kwa namna yoyote ile, basi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mwalimu Chitawala anasema mikataba hiyo ilitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na kusainiwa na wazazi wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana.
Mratibu wa Elimu kata ya Nambilanje, Lista Mziwanda anasema suala la wazazi kuwalazimisha wanafunzi kuandika ‘utumbo’ kwenye mitihani ya taifa lipo kwa kiasi kikubwa eneo hilo ingawa hakuna takwimu rasmi.
“Tulizibaini kesi hizo baada ya kuwabana wanafunzi ambao tuliwategemea kufaulu lakini hawakufaulu. Ukikaa na mtoto vizuri anakuambia ukweli kuwa alilazimishwa na mama,” anasema
Anasema kesi hizo ni za wanafunzi ambao walifaulu vizuri kwenye mitihani ya ndani na ile ya kujipima ‘Mock’ lakini mitihani ya taifa walifeli.
“Kinachofanyika sasa ni kutoa elimu lakini na hizo sheria ndogondogo kama kuwasainisha wazazi mikataba kuwa wakibainika kuwalazimisha watoto wafeli, watachukuliwa hatua. Tumeanza suala la mikataba mwaka jana, tutaangalia mwaka huu,”anasema.
Mwalimu Mziwanda anasema kati ya wanafunzi 76 waliomaliza darasa la saba mwaka 2018, 66 walifaulu kwenda Sekondari na wanne wamekwenda Chuo cha ufundi Nkoye. Mwananchi ilibaini kuwa, mazingira ya kielimu wilayani humo ni magumu kwa baadhi ya wanafunzi ambao hulazimika kubaki peke yao kwa muda mrefu baada ya wazazi wao kuondoka nyumbani na kwenda kukaa shambani msimu wa kilimo.
Mwanafunzi wa shule ya msingi Nambilanje Swaumu Ibadi anasema mazingira ya kielimu kwake ni magumu kwa sababu mama yake yupo shambani kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
“Jana usiku sijala, mpaka mchana huu kwa sababu nakaa peke yangu, mama amehamia mashambani na dada yangu niliyeachwa naye, ameondoka,” anasema
Anasema akibahatika kula, basi ni milo miwili tu kwa siku na wakati huo akitembea umbali wa karibu kilometa10 kutoka nyumbani hadi shuleni.
Saumu ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba, anasema hana mahitaji muhimu ya shule kama sare, madaftari na chakula kwa sababu mama yake hajamnunulia.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kijiji cha Nambilanje, Constatine Odilo, desturi za wazazi kuhamia shambani kipindi cha kilimo zinachangia kushuka kwa kiwango cha elimu na hata mmomonyoko wa maadili.
“Tunapokea kesi nyingi hapa kijijini za watoto wadogo wa kike kuachwa peke yao nyumbani wakati wazazi wakiwa wamehamia shambani, hili linachangia watoto hawa kuwa huru na hata wasipoenda shule, nani atawajibika?” anasema.
Familia zachangia kushuka kwa elimu, kuvunjika kwa maadili
Pamoja na wazazi kuhujumu elimu ya watoto wao, mambo mengine yanayotajwa kusababisha mimba za utotoni na kushuka kwa kiwango cha elimu eneo hilo ni wazazi kutengana.
Kwa mfano, Mtendaji wa Kata ya Nambilanje, Abdallah Tamba anasema kesi nyingi za wazazi kutengana ni nyingi na hali hiyo husababisha watoto kubaki bila malezi.
“Kwa mila za huku, kuachana ni kitu rahisi tu, kama ilivyo kuoa. Kwa hiyo mara nyingi wazazi wanapotengana, watoto ndiyo hupata tabu, wanakosa malezi kabisa,” anasema
Anasema mara nyingi baba anapobaki na watoto, huoa mke mwingine na kama mama huyo hatajali suala la elimu, basi watoto huacha shule.
Lakini watoto wa eneo hilo wanasema wazi kuwa mfumo wa matrilineal (mama kuwa kichwa cha familia) wa kabila za kusini, ndiyo huchangia changamoto hizo.
Kwa mfano, Nasra Juma, Mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Nambilanje anasema baadhi ya kinamama ndiyo wanaowaambiwa watoto wao wa kike wasiende shule bali washiriki kuleta mboga nyumbani.
“Sasa mama anamwambia binti yake kuwa leo zamu yako kuleta mboga, hiyo ina maana kuwa anamruhusu kwenda kufanya chochote ili alete mboga nyumbani,” anasema
Mila nyingine zinazotajwa kuchangia kushuka kwa elimu ni unyago ambao hufanyika kipindi cha masomo.
Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa TAMWA, John Ambrose anasema zipo mila na desturi zenye manufaa kwa jamii lakini endapo mila hizo zinachochea mimba, kushuka kwa elimu, zinamzuia mtoto kupata haki yake basi hazina budi kupingwa.
“Ndiyo maana tumeandaa midahalo hii, kwa kushirikiana na Taasisi ya Foundation for Civila Society, ili wanafunzi waeleze wazi yanayowasibu nyumbani, shuleni na katika mazingira yao mengine, tumeshuhudia mengi yanayofanyika kwa watoto na yanachangia ukatili kwao,” anasema Ambrose