News/Stories

WAZAZI WAWALAZIMISHA WATOTO KUANDIKA ‘MADUDU’ ILI WAFELI DARASA LA SABA

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Florence Majani, TAMWA.

Ruangwa. Licha ya serikali kujenga shule za kata kwa wingi ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari, wazazi wilayani Ruangwa, wamelalamikiwa kuwajengea watoto wao mazingira ya kufeli mitihani ya darasa la saba ili wasiendelee na shule na waolewe.

Hayo yalibainika wakati wa mdahalo kwa wanafunzi kuhusu mila na desturi zinazochochea mimba za utotoni ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA) wilayani Ruangwa.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi hao walisema baadhi ya  wazazi huwalazimisha watoto wao kukataa shule au kuwashauri wajifelishe mitihani ya darasa la saba ili waolewe.

“Kuna mwenzetu mmoja, alikuwa na akili sana lakini matokeo yalipotoka hakufaulu kujiunga na sekondari, tulipomuuliza kulikoni alisema mama yake alimwambia aandike 0000 ili afeli na aolewe,” alisema Zahara Chigope, Mwanafunzi wa Kidato cha nne, Sekondari ya Nambilanje.

Mwanafunzi mwingine, Nasma Kumkana, alisema suala la wazazi kuwashawishi wanafunzi wafeli kwa makusudi ni kubwa na wanalisikia kutoka kwa wanafunzi wenzao.

“Sio hivyo tu, hata baadhi ya wazazi tunawasikia wanasema bora mtoto afeli kwa sababu hawana hela za kumhudumia atakapoingia sekondari, hata wakiambiwa elimu ni bure watasema hawana fedha za sare za shule,” alisema

Nasma alisema mila hizo zinaambatana na ile ya baadhi ya wazazi kumshauri mtoto atafute mboga kwa jasho lake.

“Hii ina maana kwamba, mama anamwambia mtoto leo zamu yako kutafuta mboga, kwa maana nyingine,  mtoto wa kike anapewa ruhusa ya kuwa na mwanaume ili apate fedha ya kusaidia familia,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nambilanje, Charles Chitawala alisema tatizo hilo ni kubwa kwa kata ya Nambilanje na maeneo mengine ya Ruangwa.

“Sisi kama viongozi suala hilo linatuudhi, inabidi tutoe elimu, ili tabia hizo waziache. Ilifikia mahali ikabidi tuitishe vikao vya wazazi na wazazi wajaze mikataba,” alisema.

Alisema mwaka 2018, wazazi walijaza mikataba na kukubaliana kuwa iwapo mzazi atabainika kuwa alimshauri au kumlazimisha mwanafunzi kufeli kwa namna yoyote ile, basi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwalimu Chitawala alisema mikataba hiyo ilitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na kusainiwa na wazazi wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana.

Mratibu wa Elimu kata ya Nambilanje, Lista Mziwanda alisema suala la wazazi kuwalazimisha wanafunzi kuandika  ‘utumbo’ kwenye mitihani ya taifa lipo kwa kiasi kikubwa eneo hilo ingawa hakuna takwimu rasmi.

“Tulizibaini kesi hizo baada ya kuwabana wanafunzi ambao tuliwategemea kufaulu lakini hawakufaulu. Ukikaa na mtoto vizuri anakuambia ukweli kuwa alilazimishwa na mama,” alisema

Alisema kesi hizo ni za wanafunzi ambao walifaulu vizuri kwenye mitihani ya ndani na ile ya kujipima ‘Mock’ lakini mitihani ya taifa walifeli.

“Kinachofanyika sasa ni kutoa elimu lakini na hizo sheria ndogondogo kama kuwasainisha wazazi mikataba kuwa wakibainika kuwalazimisha watoto wafeli, watachukuliwa hatua. Tumeanza suala la mikataba mwaka jana, tutaangalia mwaka huu,”alisema.

Mwalimu Mziwanda alisema kati ya wanafunzi 76 waliomaliza darasa la saba mwaka 2018, 66 walifaulu kwenda Sekondari na wanne wamekwenda Chuo cha ufundi Nkoye.

Mmoja wa wazazi, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama ya kata, Esha Chigope, alisema kesi hizo zipo nyingi.

Esha alisema kuna mkazi mwenzao aliyefahamika kama Tendele, alikiri kumshauri mtoto wake aandike 1111, ili afeli mtihani wa darasa la saba.

“Tendele mwenyewe anasema wazi, alitaka mtoto wake afeli kwa sababu hakuna umuhimu kwa mtoto wa kike kusoma, kwa hiyo kweli mtoto akafeli,” alisema Esha.

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilu alisema watawachukulia hatua wazazi wanaorubuni wanafunzi wafeli na kusema kuwa hiyo  jamii ya wazazi inayohujumu watoto.

“Ndiyo maana tuliingia mikataba kati ya serikali na mzazi, kwamba hata mtoto akifeli, mzazi awajibike kwa kutoa maelezo kwa nini kijana amefeli,” alisema.

Alisema hali ya mwamko wa elimu kwa ukanda wa kusini hasa vijiji vya Nambilanje, Namichiga, Nachienjele na Nanjaro bado ni ndogo  na inahitajika elimu ya kutosha.

Alisema hata katika ziara zake alizofanya katika vijiji 81 vya Wilaya ya Ruangwa, alibaini suala la unyago ndilo linachochea kufifia kwa elimu wilayani humo.

“Watoto wanatolewa kupelekwa unyago kipindi cha masomo. Nilikamata wazazi waliokaidi agizo langu pamoja na watoto 22 waliokuwa wanachezwa huo unyago,”alisema Mgandilu.

Latest News and Stories

Search