Press Release

MAADHIMISHO YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA DUNIANI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Mheshimiwa, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani Dk. Willow Williamson, Mwakilishi kutoka Dawati la jinsia Mkoa wa Kinondoni Mathias Mulumba, Mwakilishi kutoka Muungano wa ‘Men engage Tanzania’ Marcela Lungu na Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali nchini, Habari za asubuhi.
UKATILI WA JINSIA: “MABADILIKO YANAANZA NA MIMI”
Wakati dunia ikiadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na CRC kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani Tanzania, (UsEmbassyTz) tunawasisitiza wanajamii kuibua na kufichua matukio yote ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea kuanzia katika ngazi ya familia na katika taasisi kama vile mashuleni, vyuoni na sehemu kazi.
Siku hii inaadhimishwa duniani kote wakati Tanzania ikiwa bado na matukio ya ubakaji, vipigo, rushwa ya ngono, udhalilishaji, ndoa na mimba za mapema.  
Kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa inasema: Pinga ukatili wa kijinsia, mabadiliko yanaanza na wewe” 
Kauli mbiu hii inatupa nguvu TAMWA na CRC kuitaka jamii ibadilike kwa kuvunja ukimya kwani bila kutoa taarifa za matukio haya, vyombo vya dola havitaweza kufanya kazi yake ipasavyo.
TAMWA imebaini kuwa licha ya  vyombo vya dola kuchukua hatua lakini bado kuna matukio ya ubakaji, ulawiti, mimba za mapema na udhalilishaji.
Hivyo basi, TAMWA tunasisitiza jamii ifichue, kwani mabadiliko haya yanaanza na wewe ambaye utafanya maamuzi ya kuripoti vitendo hivyo.
Tukiyakalia kimya matukio haya, hatuwezi kupata suluhisho, ni muhimu kuripoti bila kuona haya ili vyombo vya dola vichukue hatua,
TAMWA imeshuhudia matukio kadhaa ya ubakaji wa watoto katika kipindi cha Oktoba na Novemba mwaka huu jambo ambalo linatupa wasiwasi kuwa huenda elimu bado haijawafikia wengi, wengi hawaripoti na pengine matukio kama haya yanaendelea huko majumbani kwa kificho. 
Kwa mfano, Novemba 11, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ijinga, Wilaya ya Magu, Badri  Masengo (40) alidaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita,Shule ya Msingi Ijinga mwenye umri wa miaka 15 . 
Kadhalika tukio jingine kama hilo ni lile la kubakwa kwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Montfort, (10)  na mwalimu wake, (27) Anderson Eneza, mnamo Novemba 11, 2020.
Tukio jingine ni lile la Medadi Chitezi (60) mkazi wa kijiji cha Ulumi, Rukwa, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 10. Chitezi alifanya kosa hilo Agosti, 12, 2020. 
Huko visiwani Zanzibar, limeripotiwa tukio la Mzee wa miaka 60, Haroub Abdallah Hamad, anayedaiwa kumbaka mtoto wa miaka mitano. Tukio hilo limetokea Oktoba 10, 2020, wilayani Wete, Pemba. 
Kadhalika, utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (PCCB) umebaini kuwa kuna tatizo kubwa la rushwa ya ngono katika vyuo vikuu nchini. 
Utafiti huo uliochapishwa hivi karibuni, uliofanywa katika vyuo vikuu vya Mlimani na Dodoma, ni angalizo tosha kuwa ukatili wa kijinsia upo wa aina nyingi, katika mazingira tofauti, kwa jinsia zote na katika sekta mbalimbali binafsi na za umma, Reuben, TAMWA
Kadhalika, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani mwaka 2013 unaonesha kuwa takriban asilimia 35 ya wanawake Duniani wamefanyiwa ukatili wa kijinsia wa kupigwa au kubakwa katika maisha yao.
 
Wakati huohuo, utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) umebaini kuwa wasichana milioni 120, duniani wamewahi kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao. 
Hiyo inamaanisha kuwa,  wanawake na wasichana milioni 200 walifanyiwa vitendo vya ukeketaji katika nchi 30 duniani huku wasichana na wavulana  milioni 246 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia wakiwa shuleni.
TAMWA imefanya jitihada kadhaa  kupunguza ukatili wa kijinsia  chini ya miradi yake mbalimbali ikiwamo ule wa Ushiriki wa Wanawake katika siasa na uongozi unaofadhiliwa na African Women Developmen Fund(AWDF)  na Ushiriki wa Wanawake katika Siasa na Uongozi unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wanawake(UN-Women). 
Mradi mwingine unaogusa eneo hilo ni ule wa Rushwa ya Ngono katika vyombo vya habari,  unaofadhiliwa na mfuko wa Wanawake Tanzania(WFT) ambapo TAMWA inafanya tafiti kujua ukubwa wa tatizo hilo na kufanya uchechemuzi ili kupunguza aina hiyo ya ukatili.
TAMWA inaibua matukio ya ukatili huo yanayoweza kutokea katika nyanja za siasa na uongozi au kazini, kisha kukaa na wadau wa siasa, serikali na wanahabari kuwapa mrejesho na madhara ya ukatili wa kijinsia katika muktadha huo. 
Mafanikio ni makubwa lakini bado jamii inatakiwa ishike hatamu kwa kuvunja ukimya na wakati huo huo wanaharakati na serikali nao watimize wajibu wao, kwa kufanya hivyo tutapunguza tatizo hili, mabadiliko yanaanza na wewe, Reuben, TAMWA
Hata hivyo TAMWA inamuomba Rais John Magufuli, kuendelea kuteua mawaziri wanawake, ambao tunaamini wataibeba ajenda ya masuala ya ukatili wa kijinsia na kuipeleka bungeni ili ifanyiwe kazi.
Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, huadhimishwa kila mwaka na huanza Novemba 25, ambayo ni Siku ya Kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na kuendelea hadi Desemba 10, Siku ya Haki za binadamu Duniani.
Kwa mawasiliano zaidi;
Tanzania Media Women Association (TAMWA)
P.O.BOX 8981, Dar es Salaam
Find us @Facebook, twitter, instagram
Mobile: +255 22 2772681

Search