Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Abeda Rashid Abdallah.....
Ndugu wadau wa masuala ya jinsia.
Viongozi wa serikali,
Wanahabari,
Itifaki imezingatiwa!
Zanzibar, February 4, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kina furaha kubwa kupata fursa hii adhimu, leo Februari 4th, 2021, ya kukutana tena na wadau wake muhimu walioshiriki katika utekelezaji wa mradi wa Wanawake Sasa’ uliofadhiliwa na taasisi ya kimataifa ya African Women, Development Fund (AWDF).
Mradi wa ‘Wanawake Sasa’ umehitimishwa kwa mafanikio makubwa na kamwe mafanikio hayo yasingepatikana bila nyinyi wadau muhimu ambao mlishiriki katika kuhimiza Amani, ushirikiano katika chaguzi na ushiriki wa wanawake katika siasa, uongozi na maamuzi.
Kutokana na ushirikiano wenu, tumeona namna ambavyo Rais, John Maguuli ameendelea kuteua viongozi wanawake, na hilo limethibitishwa katika kauli yake aliyoitoa Novemba, 2020 mara baada ya uchaguzi kuwa; ataendelea kuwaamini wanawake.
Kwa msingi huo napenda nitumie fursa hii kuahidi kuwa, serikali ninayoiongoza itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi, alisema Rais JPM.
Ndugu Mgeni Rasmi,
Si hayo tu, tumeona kivitendo, ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi na tumeshuhudia idadi ya wanawake zaidi ya 230 katika bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwamo mawaziri wanawake.
Kwa upande wa Zanzibar, tuliona uthubutu wa kinamama wawili, waliojitokeza na kuchukua fomu za kuwania urais.
Ndugu mgeni rasmi,
TAMWA inaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na ile ya bara kwa kushiriki katika matukio ya utekelezaji wa mradi huu katika maeneo manne, ikiwamo Zanzibar, Arusha, Dar es Salaam na Dodoma.
Viongozi wa Serikali wameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kufungua, kutoa nasaha na kutoa ushauri kwa TAMWA katika ajenda hii ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, Amani na mshikamano. Tunawashukuru!
Ndugu Mgeni Rasmi
Kupitia midahalo ya wanawake wanasiasa iliyofanywa katika maeneo yetu manne ya mradi, wanawake wanasiasa zaidi ya 150 kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini, walipata fursa ya kujifunza umuhimu wa kutumia vyombo vya habari kueneza ajenda zao za kisiasa.
Pia kupitia midahalo hiyo, waliweza kujifuza changamoto za kila mmoja hasa katika mrengo wa ukatili wa kijinsia, ikiwamo rushwa ya ngono na kujua namna ya kukabiliana na changamoto za aina hiyo.
Wanawake wanasiasa waliopata mafunzo waliteuliwa kuanzia ngazi ya kanda hadi kitaifa.
Ndugu Mgeni Rasmi,
TAMWA iliwaleta pamoja viongozi wa dini 50 kutoka maeneo hayo manne ambao walishiriki kikamilifu kueneza Amani wakati wa uchaguzi na kusisitiza ushiriki wa wanawake katika siasa, uongozi na maamuzi. Haya kwetu ni mafanikio kwani, nafasi ya viongozi wa dini katika kuhubiri Amani na kuwaleta watu pamoja, vilisaidia katika kufanyika kwa uchaguzi wa Amani, huru na wa haki.
Ndugu mgeni rasmi,
Kama ujuavyo TAMWA inatumia silaha yake kuu, ambayo ni vyombo vya habari katika kufikisha ajenda kwa jamii, na hivyo iliwapa mafunzo wanahabari zaidi ya 70 kutoka katika maeneo hayo manne. Wanahabari hao walifundishwa na kupata ujuzi kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
Wanahabari hao baada ya mafunzo walifanikisha kuchapishwa kwa Makala za magazeti 40, vipindi vya redio na televisheni, talk show na kuongeza wigo wa idadi ya wanahabari tuliofanya nao kazi awali na kuwafikia wa wanahabri zaidi kutoka Zanzibar, Arusha hadi Dodoma ambao waliandaa Makala za kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
Ndugu mgeni rasmi,
TAMWA na wanahabari kupitia kazi zao, walishirikiana na kuwafikia wanawake ambao awali waliogopa kushiriki katika siasa na uongozi. Hii iliongeza idadi ya wanawake waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi kuanzia ngazi za chini hadi nafasi za ubunge.
Taarifa fupi ya mradi Wanawake Sasa
Wanawake Sasa ni mradi uliotekelezwa kwa ushirikiano wa asasi tatu, TAMWA, WiLDAF na GPF Tanzania, chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa Afrika (AWDF).
Mradi huu ulikuwa na malengo makuu matatu, kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi, kwa kuwahamasisha na kuwawezesha wanawake, wanawake wenye ulemavu na vijana kuwa viongozi.
Lengo la pili, ni kuwahamasisha na kuwawezesha wanawake katika vyama vya siasa kuwania nafasi za uongozi katika vyama vyao.
Lengo la tatu ni, kukuza wanawake kisiasa, kuhamasisha Amani katika chaguzi kupitia vyombo vya habari kwa kuishirikisha jamii. Mradi huu wa mwaka mmoja, ulianza kutekelezwa Januari Novemba 2020 na utekelezaji wake ulivihusisha vyama vitano vya siasa (CCM,ACT WAZALENDO,CUF,CHADEMA NA NCCR-MAGEUZI) katika kanda nne Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji,
Rose Reuben.
TAMWA.