Press Released

Rushwa ya ngono: Kichocheo cha kurudisha nyuma maendeleo

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
 
Ndugu mgeni rasmi,
Wawakilishi wa FES,
Mkuu wa Dawati la Jinsia,
Mwakilishi wa Takukuru,
Wanahabari,
Nawasalimu kwa jina la JMT!
 
Dar Es Salaam, 2nd December, 2021. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Friedrich-Ebert-Stiftung (FES) Tanzania, wanaungana na watanzania wote kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
 
Maadhimisho haya, hufanyika kila ifikapo Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka.  Kwa mwaka huu, maadhimisho haya yamepambwa na kauli mbiu isemayo: Pinga ukatili wa kijinsia Sasa 
 
Hata hivyo wakati maadhimisho haya yakiendelea, TAMWA pamoja na FES tumebaini kuwa tatizo la rushwa ya ngono mahala pa kazi linaendelea kushika mizizi katika jamii yetu. 
 
Hilo lilibainika hata wakati TAMWA ilipofanya mradi na Asasi ya Habari ya Internews mnamo mwaka 2019 na kuwashirikisha wanahabari kufanya habari za uchunguzi kuhusu rushwa ya ngono mahala pa kazi.
Makala za wanahabari hao, zilibainisha wazi, rushwa hiyo ipo lakini imegubikwa na ukimya hasa kutoka kwa waathirika. 
Kadhalika, mwaka 2021, TAMWA kwa kushirikiana na Women Fund Tanzania, (WFT) ilitekeleza mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari. TAMWA ilifanya utafiti na kubaini wanahabari wanakabiliwa kwa kiasi kikubwa na rushwa ya ngono na ukatili mwingine ndani ya vyumba vyao vya habari.
Utafiti  uliofanywa na asasi ya EBA nchini Tanzania mwaka 2020 ulibaini kuwa, suala la rushwa ya ngono linafahamika na limetanuka kuanzia katika sekta ya elimu na katika sekta ya ajira. 
 
Tatizo la rushwa ya ngono ni kubwa lakini limegubikwa na ukimya, wahanga wengi hawatoi taarifa wakiogopa kudhalilishwa zaidi, Dr Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA.
 
TAMWA tunasema, rushwa ya ngono vyuoni ndicho chanzo cha kuwa na wanafunzi wasio na tija katika sekta ya ajira, lakini pia ndicho chanzo cha kuzalisha wanaataluma wasio na sifa za kuajiriwa. 
 
Rushwa hii ya ngono mahala pa kazi na vyuoni, ndicho chanzo pia cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa, Dr Rose Reuben. 
Katika tafiti zetu, TAMWA tumegundua kuwa rushwa ya ngono hufanyika sio tu mahala pa kazi, bali wakati mwingine, hata katika kambi za wakimbizi, katika shule za sekondari.
Rushwa ya ngono hurudisha nyuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja na nchi kwa sababu matokeo ya ukatili wa aina hii ni kurudisha nyuma ari ya utendaji kazi wa wanafunzi, wafanyakazi au waumini, Dr Rose Reuben
 TAMWA tumeona pia zipo changamoto katika kukabiliana na aina hii ya ukatili, kwanza ni ukimya. Wahanga wengi kushindwa au kuhofia kutoa ushahidi na kuzungumzia suala hili. Lakini pili, ukosefu wa takwimu zitakazowezesha wadau kufanyia kazi aina hii ya ukatili.
Ipo sheria ya makosa ya rushwa, inayogusa rushwa ya ngono, nayo ni sheria namba 11 ya mwaka 2007, kifungu cha 25. Dr Rose Reuben
 
Ukatili kwa njia ya mtandao
Wakati huo huo, tunakemea vikali ukatili kwa njia ya mtandao unaoendelea. Tumeona, tumesikia na wakati mwingine sisi ndiyo tumekuwa waanzilishi wa ukatili huu. Kutumia picha za wanawake vibaya, kutumia lugha dhalili kwa kundi Fulani mitandaoni, kutumia picha za watoto na kuweka maudhui yanayomdhalilisha. Haya ni baadhi tu ya matendo yanayochagiza ukatili wa kijinsia mitandaoni.
 
TAMWA ni wanahabari na wanahabari ni TAMWA, hivyo tunawaomba wadau wetu wa habari, mkatumie kalamu zenu kukemea rushwa ya ngono  ndani ya vyumba vyenu vya habari  na kuvaa joho la kupinga aina zote za ukatili wa kijinsia ikiwamo ule wa kwa  njia ya mtandao. 
 
Kadhalika, tunaipongeza serikali kwa kupitia wadau wake wakiwamo Takukuru, wamefanyia kazi suala la rushwa ya ngono kwa kufanya tafiti kadhaa lakini pia kwa kufanyia kazi makosa ya aina hii. Hongereni! lakini tunatamani  matokeo zaidi, kesi zaidi zipelekwe mahakamani, hukumu itolewe  ili kufanya mahala pa kazi pawe sehemu salama na penye tija. 
Pia tunampongeza  Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuzindua mwongozo wa madawati ya rushwa ya ngono vyuoni. Tunaomba yakatumike kwa tija. 
Ewe Mwananchi, pinga ukatili wa kijinsia sasa,
 
#KaziIendelee
#ZuiaUkatiliMtandaoni
#ZuiaUkatili
 
Dr Rose Reuben
 
 
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA

Search