Press Release

UDHALILISHAJI WA KINGONO, MUUAJI WA KIMYA WA TASNIA YA HABARI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Machi 8th 2022, Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, kinalazimika kutupia jicho lake kwenye usalama wa wanahabari wanawake katika vyumba vya habari nchini Tanzania.
 
Ulazima huu umekuja baada ya kuwepo kwa mwendelezo wa matukio, ushahidi, na ripoti za kitafiti zinazoonyesha kuwa wanahabari wanawake siyo tu Tanzania bado wanapitia unyanyasaji wa kingono katika vyumba vya habari. 
 
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa mwaka huu, yamebebwa na Kauli mbiu isemayo; Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu. Kauli hii inatupeleka zaidi kutaka kuweka usawa katika vyumba vya habari baada ya kubaini kuna mdudu anayetafuna tasnia ya habari kimya kimya. 
 
 Utafiti uliofanywa na Asasi ya Wanawake katika Habari Africa (WIN) mwaka 2022 ulibaini kuwa, asilimia 41 ya wanawake wanahabari waliwahi kufanyiwa unyanyasaji wa kingono wakiwa katika maeneo ya kazi. 
 
Hivyo basi wakati tukiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, TAMWA inahimiza Wamiliki wa vyombo vya habari, watunga sera, serikali na wanahabari wote kwa ujumla kutupia jicho unyanyasaji na ukatili wa kingono unaofanywa ndani ya vyumba vya habari.
 
Unyanyasaji wa kingono kwa wanahabari iwe ndani au nje ya vyumba vya habari, una madhara makubwa katika chombo cha habari, taaluma ya habari, aina ya habari zitakazoandikwa na hata katika maendeleo ya nchi yenyewe. Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk  Rose Reuben.
 
Udhalilishaji wa kingono kwa wanahabari wanawake, unachagiza wanahabari wengi wa kike kuikimbia tasnia  na hilo limesababisha kupoteza vipaji lukuki ambavyo vingekuzwa iwapo kusingekuwa na bughudha hiyo.
 
 
Kadhalika udhalilishaji wa kingono kwa wanahabari unashusha hadhi ya chombo cha habari, kwani pindi mwanahabari anapotoa shutuma kuwa mhariri au kiongozi wa chombo cha habari kamdhalilisha kingono, basi ni dhahiri chombo hicho hutazamwa vibaya. Kadhalika vivyo hivyo anapotoa taarifa kuwa amedhalilishwa na chanzo cha habari.
 
Kaika utafiti uliofanywa na TAMWA kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) mwaka 2021, kuhusu hali ya rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari, ilibainika kuwa wanahabari wanawake wamewahi kukutana na udhalilishaji huu, kimwili, kimaneno na hata baadhi walifukuzwa kazi. 
 
Hata hivyo changamoto kubwa tuliyoiona TAMWA katika tafiti hizo ni ukimya. Wanahabari wengi wanawake hawataki kusema pindi wanapodhalilishwa, hivyo wanaishi katika msongo, maumivu, fedheha na wengine kuacha kabisa tasnia, kwa sababu ya udhalilishaji wa aina hii.  Dk Rose Reuben.
 
Utafiti wa TAMWA ulibaini kuwa wanafunzi wengi wa tasnia ya habari wa vyuo vikuu wanaokwenda kujifunza kwa vitendo  katika vyumba vya habari wamekutana na udhalilishaji huo na kujikuta wakiikimbia tasnia hiyo mara tu wanapomaliza masomo yao. 
 
Hata utafiti wa WIN uliofanyika Afrika nzima kuangalia ukubwa  wa tatizo hilo, ulibaini kuwa ni asilimia 4 tu ya wanahabari wanawake wanaopaza sauti zao pindi wanapofanyiwa ukatili huu.
 
Katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, kwanza tunawaasa wanahabari kupaza sauti zao na kueleza bayana madhila wanayopitia katika kazi zao ikiwamo udhalilishaji wa kingono.
 
Imetosha sasa wanahabari kuwa kipaza sauti cha kusemea matatizo ya wengine  katika jamii, ilhali tatizo lao wamelinyamazia kimya, Dk Rose Reuben.
 
Kadhalika tunaviomba vyombo vya habari kuhakikisha vinaweka na ketekeleza sera ya jinsia ndani ya vyumba vya habari, na sera ya kupinga unyanyasaji na rushwa ya ngono na sera hizi zijulikane na wote ndani ya vyumba vya habari. 
 
Katika utafiti wa TAMWA tulibaini kuwa vyumba vingi vya habari havina sera ya jinsia wala sera za kupinga rushwa na unyanyasaji wa kingono, na vile vyenye sera hizi hazitumiki au hazijulikani na wanahabari/ wafanyakazi wengine, Dk Rose Reuben.
 
Lakini zaidi tunaiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuendelea kushirikiana na wadau kutoa elimu kuhusu sheria ya mwaka 2017 inayoangalia rushwa ya ngono mahala pa kazi. Hii itasaidia wanawake na wasichana kuifahamu  kujua kuwa uwepo wa sheria hii na namna ya kukusanya ushahidi wa madhila hayo. 
 
Lakini wakati huo huo serikali ione umuhimu wa kupeleka ajenda ya rushwa ya ngono katika vyuo vya elimu ya juu na hata mashuleni, ili kuwajengea uelewa watoto wa Tanzania uelewa na athari ya rushwa hii. 
 
Kwa mfano, hivi karibuni yamekuwapo matukio kadhaa ya wahadhiri kwa vyuo vikuu kuwadhalilisha kingono wanafunzi na huku video zao za utupu zikivuja. Haya na mengine mengi yapo pia katika vyombo vya habari na mahala pa kazi ikiwamo serikalini. 
 
Kwetu sisi TAMWA hili ni janga na ni muuaji wa kimya kimya wa utu wa wanawake,  endapo lisipochukuliwa hatua basi mabinti zetu vyuoni na wanataaluma katika uandishi watapoteza mwelekeo na hivyo tutapoteza vipaji na nguvu kazi, Dk Rose Reuben.
 
 
Kama kauli mbiu ya mwaka huu isemavyo, Haki Sawa kwa maendeleo Endelevu ndivyo tunavyotaka wanahabari wanawake waheshimiwe na wathaminiwe, watimize wajibu wao bila kulazimishwa au kurubuniwa kutoa rushwa ya ngono. 
 
Tunachoweza kusema TAMWA ni; Mwanahabari mwanamke anaweza kuripoti habari za uchunguzi kama mwanaume, anaweza kuripoti michezo kama mwanaume, anaweza kuripoti katika vita kama ilivyo kwa wanaume. Uanamke wake, hauondoi ujasiri, utimamu na umakini katika taaluma  yake. 
 
Kadhalika, Mwanahabari mwanamke hapimwi kwa sura wala sauti yake, bali ujuzi na kipaji katika taaluma yake ya uanahabari. 
 
TAMWA tunasisitiza kuwa hiki ni; Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu kama kauli mbiu  ya mwaka huu isemavyo. 
 
 
Mkurugenzi Mtendaji
 
Dk Rose Reuben
TAMWA
 

Search