Dar es Salaam, Novemba 14, 2025. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani(GIZ) leo wanazindua mradi wa ‘Sauti Zetu’ wenye lengo la kupaza sauti ili kuzuia, kupunguza ukatili wa kijinsia na kutoa elimu kwa kutumia vyombo vya habari .
Sambamba na uzinduzi huu, TAMWA na GIZ kwa pamoja tunapaza sauti zetu ili kuwasaidia wanawake na watoto dhidi ya ukatili wa kidijitali.
Haya yote yanafanyika wakati dunia inaelekea katika kuadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 1.
Hivyo basi, TAMWA tunaamini kuwa, uzinduzi wa mradi huu unafanyika huku kukiwa na haja kubwa ya kuwasaidia wanawake na watoto dhidi ya madhila ya ukatili unaofanyika mtandaoni.
Ukatili wa mtandaoni unawaathiri wanawake na watoto sambamba na makundi mengine kwa kiasi kikubwa kwani kundi hili bado halina uelewa wa kutosha wa kujilinda na kulinda taarifa zao.
TAMWA kwa uzoefu na kwa tafiti tulizowahi kufanya tumebaini kuwa faida na hasara za matumizi ya dijitali ni sawa na shilingi yenye pande mbili kwani wanawake na watoto wanatumia vifaa vya kidijitali na kupata faida lukuki lakini kwa upande mwingine mitandao ya kidijitali inawaathiri.
Na leo tunayo furaha kubwa kuzindua mradi huu adhimu wa ‘Sauti Zetu’ wakati ambapo tumebakiza siku chache tu kabla ya kuadhimisha Siku hizi 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia.
Tukirejea kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ambayo mwaka huu inasema: ‘Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia 2025: Maliza ukatili wa kijinsia kupitia majukwaa ya kidijitali kwa wanawake na wasichana wote’.
TAMWA tunasisitiza kuwa wanawake na watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili huu wa kidijitali.
Kwani tumeshuhudia madhara ya afya ya akili na ya kimwili yanayosababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii.
Kumekuwa na juhudi za dhati za serikali, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na wanaharakati wa masuala ya jinsia.
Kwa mfano, Mkataba wa Kidijitali wa Kimataifa wa 2024 (Global Digital Compact)uliweka viwango vya kwanza vya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa kidijitali na utawala wa akili bandia (AI governance).
Mwezi Desemba 2024, nchi Wanachamazilipitisha Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Uhalifu wa Mtandaoni (UN Cybercrime Convention), chombo cha kwanza cha kisheria cha kimataifa chenye athari katika kukabiliana na ukatili wa kidijitali.
Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN General Assembly)pia ulipitishaazimio kuhusu Ukatili Dhidi ya Wanawake katika Mazingira ya Kidijitali mwaka 2024, likizitaka nchi kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kuzuia na kutokomeza ukatili wa kidijitali, pamoja na kuimarisha udhibiti na uwajibikaji wa majukwaa ya mtandaoni.
Lakini bado TAMWA imeona kuna uelewa mdogo juu ya matumizi sahihi ya majukwaa ya kidijitali hali inayochagiza madhara kwa kundi hili la wanawake na watoto.
Kwa mfano, kusambaza picha au video za faragha bila ridhaa, mara nyingi hutumika kuwaaibisha, kuwabambikizia makossa, au kuwatala wanawake na wasichana.
Mengine ni kufichua taarifa binafsi kwa kuweka namba ya simu, mahala pa kazi au sura ya mwanamke mitandaoni kwa lengo la kumtisha.
Lakini pia kuna ukatili wa mitandaoni ambapo watu huunda akaunti bandi kwa kutumia jina au picha ya mwanamke ili kuharibu sifa yake au kudanganya watu wengine.
Ukatili mwingine ambao kimsingi unafanyika sana hapa nchini ni kauli za chuki au maudhui ya chuki ambapo watu huandika au kutamka maneno ya matusi yanayochochea ubaguzi au ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Mengine ni wadhalilishaji kutumia vitisho kwa kusambaza picha au video za faragha na kisha kudai pesa au upendeleo wa kingono.
Wasichana wadogo wanaotumia mitandao kama Whatsap, Tiktok na Snapchat wapo katika hatari kubwa zaidi.
Madhara ya ukatili huu ni makubwa kwani vifo, kukosa haki, kutengwa na athari kubwa za kisaikolojia zimewakumba wanawake na wasichana.
Hivyo basi TAMWA tunapozindua mradi huu na tunapoelekea katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, tunapaza sauti zetu kwa kufundisha na kukemea vitendo vyovyote vya ukatili wa kijinsia kwa njia ya kidijitali.
Katika kuanza utekelezaji wetu, tumeandaa ‘ Mwongozo wa Kanuni 10 za Kujilinda na Ukatili wa Kidijitali’.
Uzinduzi wa Mwongozo huu unakwenda sambamba na safari yetu ya ‘Kupaza sauti’ ili kupunguza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari.
KUHUSU MRADI WA SAUTI ZETU
Mradi huu unalenga kutumia vyombo vya habari kama nyenzo ya kuelimisha jamiikuhusu masuala ya Ukatili wa Kijinsia (GBV),ikiwemo kueleza maana ya GBV, chanzo chake katika jamii, na kutoaelimu kuhusu huduma zilizopo kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.
Kupitia utoaji wa ujumbe muhimu kuhusu masuala ya GBV, mifumo ya kisheria, haki za waathirika na njia za kupata haki, mradi huu utawawezesha waathirika kupataufahamu wa haki zao na huduma za msaada zilizopo.
Aidha, mradi huu utalenga kuongeza uelewa wa umma, kupinga mila na desturi kandamizi, na kuhamasisha wadau mbalimbali kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mradi huu unatekelezwa katika mikoa minne ya Tanzania Bara, ambayo ni Dar es Salaam (Kinondoni, Temeke), Dodoma (Chamwino, Bahi) na Tanga (Lushoto na Tanga Mjini).
Vyombo vya habari vitakuwa ndicho chombo kikuu cha kufikisha taarifa, kuongeza uelewa na kutumika kama daraja kati ya jamii, asasi, waathirika na jamii nzima.


