Press Release

SIKU YA MTOTO WA AFRIKA - 16 JUNE 2020

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Chama cha wanahabari wanawake Tanzania TAMWA, kinaungana na watanzania wote , wakiwemo watoto wa tanzania, kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika. Hii ni siku muhimu sana kwa sababu wadau, jamii na nchi kwa ujumla wake, tunapaswa kutafakari masuala mbalimbali yanayohusu watoto kupitia siku hii.

Kumekuwa na changamoto nyingi zinazomkabili mtoto wa afrika. lakini ningependa kugusia changamoto za mtoto wa Tanzania. Inawezekana changamoto kadhaa zikafanana kati ya nchi moja na nyingine, lakini kwa kiwango fulani changamoto za mtoto wa Tanzania haziwezi kuwa sawa na mtoto aliyeko nchini Libya kwa mfano, sababu nchi hii inapitia vipindi kadhaa vya machafuko.

Kwa takriban miaka zaidi ya 30 TAMWA imejikita katika lengo mama ambalo ni kutetea sauti ya mwanamke na mtoto kupitia vyombo vya habari, safari hii ndefu kwani sote tutakubaliana kwamba changamoto za mtoto wa Tanzania miaka 30 iliyopita zina tofautiana kwa kiwango fulani na changamoto za mtoto wa Tanzania ya leo. Kuna sababu kadhaa zinazopelekea utofauti huo, ikiwemo mabadiliko ya mtindo wa maisha, mabadiliko ya sayansi teknolojia na ukuaji wa miji na mwingiliano wa watu kutoka jamii mbali mbali.

Lakini leo naomba niwakumbushe wazazi, walezi, watunga sera, wasimamizi wa sheria na wadau wengine wa watoto na serikali ambayo mtekelezaji mkuu wa mipango ya msuala mbalimbali kuhusu mtoto wa Tazania.

Leo Tanzania ina jumla ya watoto milioni 23 hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la kuhudumia watoto la umoja wa mataifa UNICEF , hivyo utaona ni kwa namna gani nchi ya Tanzania ilivyo na idadi kubwa ya watoto , kundi ambalo ni lazima lipewe kipaombele katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

Mtoto wa Tanzania anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Udumavu, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 32 ya watoto nchini wanaudumavu, hiyo ikiwa ni sawa na watoto milioni tatu ambao wako chini ya umri wa miaka mitano.

Hili ni tatizo ambalo wadau kwa pamoja tunapaswa kulitazama sababu madhara ya udumavu ni makubwa sana ambayo athari zake zinaanzia ndani ya familia na baade taifa linaathirika pia.

Pia mtoto wa Tanzania anakabiliwa na tatizo la ukatili wa kingono, watoto wanabakwa, wanaingiliwa kinyume cha maumbile,wanakeketwa, wanapigwa na kuumizwa au kuuliwa, wanalazimishwa kuolewa, wanapata mimba , magonjwa na ulemavu utokanao na vitendo vya ukatili wa kingono, wanaumizwa kisaikolojia dhidi ya vitendo hivi na hakuna jitihada mahususi za kutibu saikolojia ya watoto hawa na hivyo wanaishi na tatizo hili maisha yao huku utumikishwaji wa watoto nao ukiendelea katika maeneo mbalimbali hasa mashambani, migodini na mijini wanaonekana katika biashara za barabarani na kuombaomba.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kwamba matukio mengi ya ukatili kwa watoto yanafanywa na watu wa karibu wa familia na hasa majumbani. Bahati mbaya sana wazazi na walezi wengi waumeacha wajibu wao wa msingi wa malezi ya watoto. Wasaidizi wa nyumbani ndio wameachiwa jukumu la malezi ya watoto.

Ukuaji na urahisi wa kutumia teknilojia umesababisha watoto kutumia mitandao kiholela, kwa muda mrefu na kujifunza vitu vingi visivyoendana na madili mema. Makazi yamekuwa sehemu hatari kwa makuzi ya watoto.

JANGA LA COVID 19
Tangu kuingia janga hili nchini mtindo wa maisha ya mtanzania yalibadilika ili kwenda sambamba na maelekezo ya wataalam wa afya katika kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwawa covid 19.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuepuka misongamano , shule zikafungwa hivyo watoto wapo nyumbani chini ya uangalizi wa wazazi na walezi ili wawe salama dhidi ya maambukizi ya corona.

Kupitia siku hii natoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wako salama na shule zitakapotangazwa kufunguliwa watoto wote warejee shuleni wenye afya njema ya mwili na akili.

Joyce Shebe.

Mwenyekiti - TAMWA

Search