Ndugu Wanahabari,
Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia uzima, afya njema na kuniwezesha kukutana nanyi ili niweze kuongea na watoto, wazazi/walezi na jamii kupitia kwenu wanahabari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2020.
Ndugu Wanahabari,
Tarehe 16 Juni, ya kila mwaka, Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ikiwemo Tanzania huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika. Chimbuko la maadhimisho haya ni mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa na Utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto, nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni, 1976. Mauaji hayo yalitokea wakati wa maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakipinga mfumo wa elimu ya kibaguzi nchini humo. Mwaka 1991 viongozi wa Umoja wa Nchi za Afrika walifanya uamuzi wa kuienzi siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto hao. Maadhimisho haya yanatumiwa na wadau wote katika nchi za Afrika kutathmini ya hali ya upatikanaji wa haki na ulinzi kwa watoto kwa lengo la kuboresha ustawi na Maendeleo ya watoto.
Ndugu Wanahabari,
Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2020 ni “Mifumo Rafiki ya Upatikanaji Haki ya Mtoto: Ni Msingi Imara wa Kulinda Haki Zao” Kaulimbiu hii inasisitiza kuweka mifumo madhubuti na rafiki ya kushughulikia mashauri ya watoto na changamoto nyingine zinazochangia watoto kukosa haki zao za msingi. Mifumo hiyo ni pamoja na uendeshwaji wa mashauri ya watoto waliokinzana na sheria, uendeshwaji wa makao ya marekebisho ya tabia za watoto waliopata hukumu, taratibu za kuasili mtoto, utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, utoaji wa ushahidi mahakamani na utekelezaji na usimamizi wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza nchi za Afrika kuweka mifumo madhubuti na rafiki ya kushughulikia haki za watoto, Tanzania inatumia nafasi hii kujitathmini kuhusu mifumo ya utoaji haki za watoto kama ilivyoelekezwa kwenye Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1990 ambao nchi yetu iliridhia mwaka 2003.
Serikali imeendelea kutoa huduma za ustawi wa jamii katika mahabusu 5 za watoto za Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Dar es Salaam. Mahabusu hizi zinatoa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na malazi, chakula na unasihi wakati watoto hao wakiendelea kuhudhuria mashauri yao mahakamani. Katika mwaka 2019/20, watoto 138 waliwezeshwa kupata huduma hizi ikilinganishwa na watoto 354 mwaka 2018/19
Katika usikilizwaji wa mashauri ya watoto, Serikali imeanzisha mahakama maalumu za kusikiliza mashauri ya watoto ambazo zimeongezeka kutoka Mahakama 3 mwaka 2015/2016 hadi kufikia Mahakama 141 mwezi Machi, 2020 nchi nzima. Kadhalika, Serikali inafanya mapitio katika baadhi ya vipengele vya sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake ili viweze kukidhi mahitaji ya sasa katika utoaji wa haki na ulinzi kwa ajili ya ustawi wa mtoto nchini.
Aidha katika kuimarisha huduma ya marekebisho ya tabia kwa watoto, Serikali kwa kushirikiana na Wadau inatekeleza programu ya marekebisho ya tabia kwa watoto waliopatikana na makosa katika Halmashauri mbalimbali Nchini. Programu hii imewezesha watoto waliopata huduma ya marekebisho ya tabia kuongezeka kutoka watoto 91 mwaka 2015/16 hadi watoto 501 Machi, 2020
Katika kuimarisha Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika ngazi za Mikoa na Halmashauri, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika vituo 427 nchi nzima kwa lengo la kuwezesha matukio ya ukatili wa kijinsia na watoto kuripotiwa katika vituo hivyo na kuwezesha watuhumiwa kuchukuliwa hatua za kisheria. Aidha, Mafunzo yametolewa kwa askari 490 wanaohudumu katika madawati hayo.
Sambamba na hilo, Serikali imeendelea kusimamia mfumo wa utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto; ambapo kuanzia mwezi Juni 2017 hadi kufikia Machi, 2020 jumla ya watoto 167 walipata huduma katika nyumba salama 9. Nyumba hizo zipo katika mikoa ya Arusha (2), Iringa (1), Kigoma (1), Mara (2), Manyara (1), Morogoro (1) na Mwanza (1). Vile vile kuna fursa kwa watoto katika utoaji wa ushahidi mahakamani pamoja na utekelezaji na usimamizi wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.
Ndugu Wanahabari,
Serikali imeendelea kutoa huduma za malezi ya kambo na kuasili watoto walio katika mazingira hatarishi hususan watoto wasio na wazazi, walezi au ndugu. Huduma hii inalenga kuhakikisha watoto wanalelewa katika malezi ya familia ya kudumu. Watoto waliopata huduma ya kuasili wameongezeka kutoka watoto 28 mwaka 2015/16 hadi kufikia watoto 95 Machi, 2020 na watoto waliopata huduma ya malezi ya kambo wameongezeka kutoka watoto 57 mwaka 2015/16 hadi kufikia watoto 217 Machi, 2020
Ndugu Wanahabari,
Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2016 inayoelekeza elimu kutolewa bila malipo kwa watoto wote na Sera ya Mtoto ya mwaka 2008 inayohimiza utoaji wa haki za msingi za watoto ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa. Mifumo mingine iliyoanzishwa ni Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo kamati zimeongezeka kutoka Kamati 7,316 mwaka 2017/18 hadi kufikia Kamati 16,343 Machi, 2020. Kamati hizi zina jukumu la kuratibu utekelezaji wa afua za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi husika. Aidha, Vituo vya mkono kwa mkono (one stop centres) vimeongezeka kutoka vituo 6 mwaka 2017 hadi kufikia vituo 13 mwezi Machi, 2020 katika mikoa 10 nchini ambayo ni Dar es Salaam (2), Pwani (1), Mwanza (1), Mbeya (1), Arusha (1), Iringa (1), Tabora (1), shinyanga (3), kilimanjaro (1) na Simiyu (1)
Ndugu Wanahabari,
Pamoja na mifumo mizuri ambayo serikali imeweka ili kusimamia na kulinda haki za watoto, bado watoto wanaendelea kufanyiwa vitendo vya ukatili vikiwemo ubakaji, ulawiti, utumikishwaji na mimba za utotoni. Kwa mujibu wa Takwimu za Jeshi la Polisi kwa miaka miwili mfululizo zinaonesha kuwa vitendo vya ukatili vinaendelea kuongezeka, ambapo kwa mwaka 2018 jumla ya matukio 14,491 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa, ikilinganishwa na matukio 15,680 yaliyoripotiwa mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la matukio 1,189. Aidha, kwa mwaka 2018 aina ya matukio yaliyoongoza ni ubakaji (matukio 5,557), mimba za mwanafunzi (matukio 2,692) na ulawiti (matukio 1,159), ambapo mwaka 2019, matukio yaliyoongoza ni ubakaji (matukio 6,506), mimba za wanafunzi (2,830) na ulawiti (1,405). Mikoa ya kipolisi iliyoongoza kuwa na matukio mengi zaidi ya ukatili dhidi ya watoto kwa mwaka 2018 ni Mkoa wa Tanga (1,039), Mbeya (1,001), Mwanza (809) na Arusha (792) na kwa mwaka 2019 ni Mkoa wa Tanga (matukio 1,156), Mkoa wa Kipolisi-Temeke (844), Mbeya (791) na Mwanza (758).
Ndugu Wanahabari,
Katika kukabiliana na changamoto zilizoainishwa dhidi ya Watoto wetu, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 ambapo imeweka kipengele kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kusababisha mimba kwa mtoto wa shule na pia kumuoza na hatimaye kukatisha masomo atashtakiwa na akipatikana na hatia atatumikia kifungo kisichopungua miaka 30 jela. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la C-SEMA imeendelea kupokea taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kupitia simu ya bure namba 116; taarifa hizo hupokelewa na kufanyiwa kazi bila kumuathiri mtoa taarifa. Kwa kutumia namba hii, watoto waliofanyiwa ukatili na kupata huduma wameongezeka kutoka watoto 493 mwaka 2016; Watoto 1072 mwaka 2017; Watoto 1854 mwaka 2018; Watoto 2139 mwaka 2019; na watoto 813 katika kipindi cha Januari mpaka Machi 2020, na hivyo kufanya jumla ya watoto 6,371 waliofikiwa. Huduma walizopatiwa ni pamoja na chakula, vifaa vya shule, unasihi, malazi, afya na huduma za sheria.
Ndugu Wanahabari
Katika eneo la malezi ya watoto wetu bado kuna changamoto kubwa ya matumizi ya mitandao, katika kipindi hiki tumeshuhudia watoto wanatumia vifaa ya kielektroniki ikiwa pamoja na simu na komputa kujifunzia, ni vyema watoto wazingatie matumizi sahihi ya vifaa hivyo; Wazazi au Walezi hakikisheni watoto wanasimamiwa katika matumizi ya vifaa hivyo ili kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vya ngono na ukatili mwingine mitandaoni. Usalama wa watoto ni muhimu wakati wote na hivyo, watoto wakiwa nyumbani katika kipindi hiki wajiepushe kwenda kwenye maeneo yatakayo hatarisha usalama wao, ikiwa pamoja na kubakwa, kulawitiwa, kushawishiwa kufanya ngono na hata kupata maambukizi ya Corona.
Ndugu Wanahabari,
Maadhimisho ya mwaka huu, 2020 yanafanyika bila mikusanyiko ya watu kama tulivyozoea kutokana na ugonjwa wa Corona. Hivyo Wizara ilielekeza Mikoa na Halmashauri kubuni mbinu mbadala za kufanya maadhimisho hayo, ikiwa ni pamoja na:-
- kuandaa na kurusha vipindi maalumu kwenye vyombo vya habari vya kitaifa, radio za jamii, mitandaoni na jumbe fupi za simu ili kutoa elimu kwa watoto, Wazazi na jamii kuhusu umuhimu wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na ugonjwa wa Corona.
- kutumia gari la matangazo ili kutoa ujumbe maalumu wa kuelimisha watoto na jamii kwa ujumla kuhusu haki na ulinzi wa watoto na kujikinga na ugonjwa wa Corona katika Halmashauri zetu.
- Utoaji wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa watoto hususani waliopo kwenye makao na shule za sekondari zilizofunguliwa katika Mkoa.
Ndugu Wanahabari,
Serikali inaendelea kusisitiza kufuatwa kwa maelekezo ya wataalam wa afya kuhusu kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa kutoruhusu mikusanyiko isiyo ya lazima. Nitoe rai kwa Wazazi/ walezi na jamii kwa ujumla kuimarisha ulinzi na tahadhari kwa watoto dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona. Wazazi/walezi wanashauriwa Kupunguza mizunguko isiyo ya lazima badala yake watulie katika familia zao ili wasimamie utekelezaji wa ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya katika kukinga familia zao dhidi ya maambukizi ya virusi vya CORONA.
Na kwa kuwa shule bado zimefungwa na watoto wanakaa nyumbani kwa muda mrefu ni muhimu kuendelea kuimarisha huduma za uchangamshi wa watoto ili watoto wapate haki yao ya kucheza na kuchangamsha akili. Ninawahimiza Wazazi kubuni michezo mbalimbali ya watoto, hasa kwa kutumia zana rahisi zinazopatikana katika mazingira yao ili mradi mtoto aweze kuburudika sambamba na kuendelea kujifunza kutokana na vipindi vya masomo kwa njia ya redio, televisheni na Mitandao ya Kijamii iliyoandaliwa kwa ajili yao.
Mwisho:
Napenda kutoa rai kwa Wadau wote wanaotekeleza shughuli za ulinzi na haki za mtoto kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kuhusu Sheria, Sera na Miongozo mbalimbali inayolinda haki za watoto nchini. Aidha, Serikali inatamani kuona mtoto wa kitanzania yupo salama wakati wote. Nawakumbusha wadau wote wa watoto kuona kwamba ulinzi wa watoto wetu ni jukumu letu sote.
Wanahabari, niwaombe muendelee kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hasa vitendo vya ubakaji, ulawiti na mimba za utotoni kwani ndio vitendo vinavyoongaza kufanyiwa watoto wetu katika jamii kwa sasa.
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza