Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewataka wazazi, walezi, jamii hasa wanahabari kuchukua hatua na kulinda haki za wahanga wa ukatili wa jinsia na usalama wao katika mitandao ya jamii ili kuepusha udhalilishaji zaidi unaoweza kujitokeza.
TAMWA inachukua hatua hii baada ya kuendelea kusambaa kwa video fupi na maudhui, ya binti wa kidato cha tano wa shule ya Panda Hill mkoani Mbeya, aliyetoroka shule na kisha kudaiwa kukimbilia kwa mwanaume aitwaye Baba Jose.
Baada ya kusambaa kwa maudhui hayo, kumeendelea kusambaa video fupi na taarifa mbalimbali zikimuonyesha binti huyo akijieleza na kwenda mbali zaidi kuwa alifanyiwa ukatili wa kijinsia yaani kubakwa na mwalimu wake wa nidhamu, jambo lililovuta maoni mengi dhalili.
Hofu ya TAMWA inajikita zaidi katika utu, usalama, na hatma ya baadaye ya binti huyu ambaye mahojiano yake yanaendelea kusambaa huku wasambazaji na waandaji wa maudhui hayo wakiacha sura yake ionekane wazi wazi, jambo ambalo linavuta hisia na maneno dhalili yanayoweza kuweka usalama wake na afya yake ya akili hatarini.
TAMWA tunaamini kuwa binti huyu bado anayo nafasi ya kujenga hatma yake, hata kuendelea na masomo na baade kuwa mwanajamii mwenye mchango mkubwa kwa taifa.
Pia vyombo vya dola vilivyochukua maelezo yake ya awali vinauwezo wa kuhakikisha haki yake inapatikana vizuri zaidi kuliko mijadala inayozuka baada ya mahojiano yake na waandishi wasiofuata maadili na kusambaza mitandaoni.
Binti huyu bado ana haki ya kulindwa na wazazi, walezi, jamii, serikali na waandishi wa habari na ndio maana TAMWA tunapata wasiwasi anavyoendelea kuhojiwa na kusambazwa mitandaoni ambako kunazua hisia na mijadala dhalili, kutukanwa na kutuhumiwa.
Lakini pia, mpaka sasa inatushangaza kwani hatujaona wazazi au walezi wake wakisimama moja kwa moja kuzungumzia suala hilo na badala yake binti huyo ameachwa kujieleza peke yake kwa wanahabari ambao nao wameshindwa kulinda utu wa muathirika kwa mujibu wa maadili ya uandishi. Maadili ya uanahabari yanasisitiza kuficha sura ya waathrika wa ukatili hata ikiwezekana wazazi wa mtu/mtoto aliyefanyiwa udhalilishaji, ili kumlinda na kulinda utu wake na kumpunguzia maumivu ya ukatili aliopitia na katika hili binti huyu anastahili kulindwa.
Kwa mujibu wa kanuni zilizotengenezwa Baraza la Habari Tanzania (MCT,2020) ni kinyume cha maadili kuwabainisha watoto walionyanyaswa, kutumika vibaya au walioshtakiwa na kupatikana na hatia ya jinai. Kanuni hizo zinawataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari katika kutumia picha na majina na waepuke kuchapisha taarifa kunapokuwa na uwezekano wa kuwaathiri wahusika.
Inaelezwa kuwa baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa amri ya kutafutwa kwa binti huyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera naye alitoa amri ya kusakwa. Alipopatikana taarifa zinaeleza kuwa, mwanamke aliyejitambulisha kama mama Abdul, ambaye naye alisema, binti huyo alipelekwa kwake na mwanaume mmoja aitwaye baba Jose, ambaye naye alisema: “Ni mke wake ...” Na baada ya hapo vyombo vya dola vilikusanya maelezo.
Katika hali hiyo TAMWA, kama wadau wa habari na watetezi haki za wanawake, wasichana na watoto, tunawataka wazazi, walezi , jamii na wanahabari kuwajibika na kulinda haki za wanawake na watoto, waliopitia ukatili wa kijinsia, ili kuepusha madhara ya kudumu na makubwa zaidi, ya kimwili na kisaikolojia kwa muathirika.
Imetolewa na
Dkt Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji.