Press Release

TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB),WAZIRI WA AFYA KATIKA WARSHA YA UZINDUZI WA UTAFITI WA HAKI YA AFYA YA UZAZI KWA WANAWAKE WA MIJINI NA VIJIJINI KUPITIA VYOMBO VYA HABARI, JULY 22, 2023, Seashell Hotel, Dar es Salaam

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
 
  • Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa, Bi.AgnessMgaya
  • Mwenyekiti wa Chama cha Waandishiwa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi Joyce Shebe
  • Mkurugenziwa Chama wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA, Dr. Rose Reuben.
  • Wanachama wa TAMWA, wakiwamo pia na baadhi ya waanzilishi.
  • Wahariri kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari
  • Viongozi wa Asasi za Habari Tanzania,
  • Wanasayansi na watafiti
  • Wadau wa masuala ya jinsia na Afya
  • Waandishiwa Habari,
  • Wageniwaalikwa,
  • Mabibi na Mabwana

 

Nawasilimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Awali ya yote, napenda kutumiafursa hii kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutukutanisha katika mkutano huu muhimu wa uzinduzi wa utafiti wa haki ya afya ya uzazi kwa wanawake wa mijini na vijijini kupitia vyombo vya habari.

Aidha, nami nichukue nafasi hii kuwapa pole kwa kuondokewa na mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Bi. Leyla Sheikh mwezi uliopita “Bwana alitoa Bwana ametwaa, jina lake lihimidiweAmen”

Ni furaha yangu kuungana nanyi katika warsha hii ambayo nimeambiwa ni mwendelezo wa kutekeleza mradi wenu wa Uchechemuzi wa Masuala ya Haki ya Afya ya Uzazi kwa wanawake wa mijini na vijijini kupitia Vyombo vya Habari uliofadhiliwa na Wakfu wa wahisani wa Wellspring.

Ndugu wana warsha, mabibi na mabwana

Nimeambiwa kuwa, baadhi yenu mmekuwa hapa kwa siku mbili zilizopita mkijifunza na kujadili mchango wa vyombo vya Habari kwa namna ambavyo vyombo hivyo vinaweza kuongeza uelewa wa Haki za Afya ya Uzazi. Niwapongeze sana TAMWA kwa hatua hii ambayo moja kwa moja inalenga ustawi wa jamii yetu kwani uelewa unajengwa kwa taarifa sahihi na waandishi wa Habari mnaweza kufikia watu wengi kwa wakati mmoja.

Ndugu wanawarsha, mabibi na mabwana

Nchi yetu imesaini mikataba mbali mbali ya Kimataifa na Kikanda ambayo ina lengo la kuboresha afya ya uzazi, mama na mtoto. Lengo namba 3 la Maendeleo Endelevu (SDG 3), kipengele cha 7 linazungumzia upatikanaji wa huduma za afya uzazi kwa wote, ikiwemo uzazi wa mpango, kupata habari zinazohusiana na afya ya uzazi na kuweka afya ya uzazi katika mipango ya Serikali, ifikapo mwaka 2030.Aidha, Kifungu namba 14 (g) cha Itifaki ya Maputo (Maputo Protocol) kinazungumzia haki za afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake.

Ndugu wana warsha, mabibi na mabwana

Ikumbukwe kuwa, nchi yetu inatekeleza mikataba hiyo ya kimataifa kwa kuingiza masuala ya afya ya uzazi mama na mtoto katika mipango yake yote kuanzia Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2024/2025), Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya (2021/2022 – 2024/2025). Mipango hii yote inatekelezwa na Wizara kupitia Mpango mmoja wa Taifa wa afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Lishe (One Plan III). Pamoja na mpango huu kuna Mpango Maalum wa uwekezaji katika afya ya Uzazi kwa Vijana na Kupambabana na Unyanyasaji wa Kijinsia na Unyayasaji dhidi ya Watoto (National Accelerated Action And Investment Agenda For Adolescent Health And Wellbeing - NAIA-AHW) 2021/22 – 2024/25).

Hivyo, sote tunashuhudia kwa namna ambavyo nchi yetu inatilia maanani afya ya Uzazi, mama na Mtoto kupitia miongozo hiyo. Sambamba na hayo, Wizara inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa tunatekeleza haki za Afya ya Uzazi katika shughuli zetu za kila siku na tunafanya kazi na wadau mbalimbali wakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali na ndiyo maana nami nimekuja hapa kuungana nanyi kwani tunaelewa kuwa afya ya uzazi sio tu kuwa ni huduma bali pia ni haki ya msingi katika ustawi wa jamii.

Ndugu wana warsha, mabibi na mabwana

Wizara imeendelea huhakikisha kuwa haki za afya ya uzazi zinapatikana nchini kote ikiwemo kununua na kusambaza bidhaa za uzazi wa mpango.  Mathalani, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 Serikali ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango 2,538,247 sawa na asilimia 89 ya lengo, sindano za uzazi wa mpango aina ya Depo-provera dozi2,564,691 sawa na asilimia 94 ya lengo na vipandikizi 552,494 sawa na asilimia 81 ya lengo. Aidha, Serikali imeendelea kuwapelekea wananchi huduma hizi kwa kufanya huduma za mkoba (outreach services) ambapo asilimia 18 ya wateja wa njia za uzazi wa mpango walipata huduma kupitia njia hii katika kipindi nilichokitaja. Kuongezeka kwa matumizi ya njia za kisasa za uzazi kunadhihirishwa na takwimu za mwaka 2021/2022 (DHS / MIS) ambapo matumizi hayo yameongezeka kutoka asilima 32 (TDHS 2015/16) hadi 38(DHS/MIS 2022/23).

Ndugu wana warsha, mabibi na mabwana

Pamoja na kutoa huduma za uzazi wa Mpango, Wizara imeendelea kuandaa miongozo, kanuni, sera na sheria mbalimbali zinazowezesha utoaji wa haki za afya ya uzazi kwa wanawake na vijana nchini. Vilevile, huduma za matibabu kwa wanawake ambao wamepata changamoto za kuharibikiwa na mimba au baada ya mimba kutoka (cPAC: comprehensive postabortion care) zinapatikana kuanzia ngazi ya chini ya utoaji wa huduma za afya yaani zahanati na pia mafunzo kwa watoa huduma pamoja na vifaa vinatolewa kwa ajili ya huduma hii.

Jitihada hizi za Serikali katika afya ya uzazi kwa vijana zinaonesha mafanikio kwani Takwimu za mwaka 2021/2022 (DHS/MIS 2021/22) zinaonesha kuwa kiwango cha mimba za utotoni kimeshuka kidogo kutoka asilimia 27 ya mwaka 2015/16 hadi asilimia 22. Ni mategemeo yangu kuwa kwa jitihada za Serikali pamoja na wadau kama TAMWA kiwango hiki kitashuka zaidi.

Ndugu wana warsha, mabibi na mabwana

Pamoja na mafanikio tunayoyapata katika Sekta ya Afya, ikiwemo katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto bado tuna changamoto ya upungufu wa wataalamu wa kutosha katika kutoa elimu kwa vijana wa uelimishaji rika, muda wa watoa huduma kuwa mdogo na wataalamu kuwa na muda finyu wa kutekeleza majukumu yao kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine na uhitaji wa wale wanaowahudumia. Na ili kupambana na hili, Wizara ina mpango wa kurudisha kada ya watumishi wa afya katika ngazi ya Jamii (Community Health Workers) kuanzia mwaka huu wa fedha. Hii itasaidia kuwafikia wananchi walio wengi zaidi kuliko kuwasubiri waje vituoni.

Mtakubaliana na mimi kuwa, ili kuboresha huduma za afya ya uzazi, tunahitaji kupata taarifa sahihi na njia salama, zenye ufanisi, nafuu na zinazokubalika katika upangaji waujauzito kwa kuchagua hivyo basi ni lazima Wananchi wapewe taarifa sahihi ili waweze kujikinga na mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa.

 

Ndugu wana warsha, mabibi na mabwana

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania -TAMWA kimefanya Utafiti unaoonyesha jinsi vyombo vya habari vinavyoandika habari kuhusu wanawake na wasichana wa vijijini na mijini katika haki za afya ya uzazi nchini Tanzania.Utafiti huo ulifanyika kwa kukusanya, kuchambua, na kutoa taarifa za kina zinazotolewa katikavyombo vya habari.

Utafiti huo ulikuwa na madhumuni ya kurutubisha nakuwezesha ustadi wa watendaji wa vyombo vya habari katika kukuza matokeo ya haki za afya ya uzazi na jinsia hapa nchini. Pamoja na hayo,utafiti huo ulilenga kutoa takwimu za msingi zinazohitajika kwa mradi wenye mada isemayo: "Uchechemuzi kupitia vyombo vya habari Vijijini na Mijini kwa Wanawake na Wasichana katika Haki za Afya ya Uzazi wa Kijinsia”nchini Tanzania.

Ndugu wanawarsha, mabibi na mabwana

Katika utafiti huu, tumeambiwa kuwa taarifa kutoka kwa wanawake na wasichana zilikusanywa, kuchambuliwa ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na wanahabari, wahariri, watafiti  wa vyombo vya habari vya mkoa wa Dar es Salaam na walibaini yafuatayo:

  • Miongoni mwa vyombo 20 vilivyotumika katika utafiti huu, ilibainika kuwa, nusu hutoa zaidi habari za kisiasa, kijamii na uchumi lakini masuala ya Afya ya Uzazi hayapewi kipa umbele.
  • Wanahabari 125 walithibitisha ukosefu wa maarifa juu ya masuala ya Haki za Afya ya Uzazi (Sexual and Reproductive Health Rights - SRHR)ikiwa ni pamoja na upungufu wa maarifa husika ya kuripoti au kushughulikiamaudhui yanayoleta utata katika utafutaji wa data kutoka kwa watafiti.
  • vyombo vya habari 17 (85%) vinashughulikia programu za Afya ya Uzaziza ndani zinazojumuisha masuala ya Usafi wa Hedhi au UWAKI, nahivyo hawana nafasi au programu maalum za masuala ya afya ya Uzazi isipokuwa kama kuna ufadhili ambao haudumu kwa muda mrefu. Pia, ilielezwa kuwa, ni vyombo 3 (15%) tu vya habari vyenye  programu maalum za Afya ya Uzazi zinazozalishwa na vyombo vya habari maalum vya masuala hayo.
  • Kutokuwepo kwa mitandao maalumu ya wanahabari wa Afya ya Uzazi nchini hususan upande wa Bara ikilinganishwa na masuala mengine ya kijamii, kisiasa au kibiashara kunapunguza ukuzaji wa ajenda hiyo kwa jamii.
  • Uelewa mdogo miongoni mwa wanawake na wasichana wa mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na nafasi ndogo ya kutafuta huduma za Afya ya Uzazi.
  • Afya ya Uzazi imebinafsishwa na inahusishwa na kanuni na miiko ya mila na tamaduni, hivyo ni vigumu kupata vyanzo vya habari na kuna utayari mdogo wawatu kujadili jambo hilo kupitia vyombo vya habari.
  • Ushiriki duni kutoka kwa watafiti na taasisi za kitaaluma katika utoaji wa taarifa na takwimu kuhusuHaki za Afya ya Uzazi kwa vyombo vya habari, kwa sababu tu watafitina wasomi wanapendelea jarida, vitabu na mijadala ya kitaaluma.
  • Sera za vyombo vya habari, hazitoi kipaumbele masuala ya Haki za Afya ya Uzazi, kwa sababu hazichangii mapato.
  • Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa, wanahabari wengi hawajapata mafunzo ya Haki za Afya ya Uzazi, ambapo asilimia 76 ya wanahabari waliohojiwa, walisema kuwa, hawajapata mafunzo hayo, na asilimia 22 tu ndiyo waliopata mafunzo.
  • Watafiti 7 waliohojiwa walibaini kuwa kuna haja ya uchechemuzi wa masuala ya Haki ya Afya ya Uzazi na kushauri kuwa, kuna haja ya kuwajengea uwezo wanahabari ili waweze kuripoti masuala ya afya ya uzazi
  • Kwa ujumla afya ya uzazi imekuwa ikitangazwa na kueleweka kama huduma na sio haki kwa wananchi wetu kwani matokeo yanaonyesha kuna uchapishwaji mdogo wa maudhui ya Haki za Afya ya Uzazi.  Pia, hakuna uchapishwaji wa habari za kina za utendaji, kampeni za kiafya, na za uchunguzi kuhusu Haki za Afya ya Uzazi.

 

 

 

Ndugu wanawarsha, mabibi na mabwana

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina nia ya kuboresha huduma za afya ya uzazi na kuwalinda wasichana, wanawake na watoto kutokana na unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto. Vilevile, kuimarisha afya na kuepusha magonjwa yanayosababishwa na ngono, ikiwemo VVU, pamoja na mimba za utotoni. Jitihada hizi zitafanikiwa sana endapo wanahabari watapata taarifa sahihi na za kutosha na za kina kuhusu masuala ya Afya ya Uzazi na kuyafikisha kwa wanachi kwa usahihi wake.

Mwisho,

Kabla sijamaliza hotuba yangu, nitumie fursa hii kwa mara nyingine kuwashukuru Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa utafiti mzuri ambao umeleta matokeo yatakayosaidia Serikali katika kuboresha utoaji wa huduma za afya hapa nchini ikiwemo huduma za afya ya uzazi mama na mtoto.  Wizara inathamini, mchango wa wanahabari kama injini ya kuwafikia wadau na jamii nzima katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa haki za afya ya uzazi. Vilevile, nawashukuru wadau wa sekta ya afya wanaoshirikiana na Serikali katika kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma za afya hapa nchini.

Baada ya kusema haya machache, naushukuru sana uongozi wa TAMWA kwa kunialika katika Warsha ya Uzinduzi wa Utafiti wa Haki ya Afya ya Uzazi kwa Wanawake wa Mijini na Vijijini kupitia vyombo vya Habari

 

 

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza

Search