Press Release

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Dar es Salaam, 8 Machi 2025. Machi 8, kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Wanawake Dunia. Siku hii huadhimishwa duniani kote ili kuukumbuka mchango, nafasi, ushiriki na changamoto zinazomkabili mwanamke na mtoto wa kike.

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) kinaungana na dunia kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kauli mbiu ya kimataifa isemayo: ‘Chochea Mabadiliko’ na kitaifa kauli mbiu kwa mwaka huu ni: "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”

Katika maadhimisho haya TAMWA inaithamini siku hii kwani ni fursa muhimu ya kujadili hatua zilizopigwa katika kusimamia usawa wa kijinsia na kuweka mikakati ya kuharakisha mabadiliko yenye tija kwa wanawake na wasichana nchini.

Vilevile, Tanzania inaelekea kufanya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani baadaye mwaka huu. Uchaguzi huu ni muhimu kwa taifa letu hasa tunapotimiza takwa hili la kidemokrasia.

Tunatoa pongezi za dhati kwa vyama vya CCM na ACT-Wazalendo ambavyo tayari vimempitisha Rais Samia Suluhu Hassan upande wa CCM na Dorothy Semu, kwa chama cha ACT-Wazalendo kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka huu.

Hii ni hatua kubwa demokrasia hapa nchini, na inaendelea kuweka hamasa kwa jamii ambayo awali ilidhaniwa wanawake hawawezi kuwa marais wala viongozi.

Hata hivyo Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, bado kuna udhalilishaji mkubwa kwa wagombea wanawake katika vipindi vya uchaguzi. Udhalilishaji huo hufanyika majukwaani wakati wa kampeni  na kwenye mitandao ya kijamii ambao unachagiza kupungua kwa idadi ya wanawake viongozi ama ushiriki wao katika siasa na uongozi.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wanawake, (UN-Women) zinaonyesha kuwa, mpaka kufikia Juni 2024, kulikuwa na nchi 27 tu duniani, ambako wanawake 28 ni wakuu wa nchi hizo. Takwimu hizo zinaeleza kuwa, mapengo ya kijinsia katika nafasi za juu za uongozi hayatazibwa katika miaka 130 ijayo.

Idadi ya wanawake ni 24 kati ya wabunge 264 ambayo ni sawa na asilimia 9.1 huku idadi ya wabunge wanawake wa viti maalumu ni 113 ambayo ni sawa na asilimia 29 ya wabunge wote na  jumla ya wabunge wanawake ni 141 sawa na asilimia 37 ya wabunge wote ambao ni 393.

Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya madiwani wanawake wa kuchaguliwa kutoka kwenye kata ni 204 ambayo ni sawa ana asilimia 3.8 ya madiwani wote huku madiwani wanawake wa viti maalumu ni 1,407 sawa na asilimia 26.2 ya madiwani wote

Hivyo basi tunapoadhimisha siku hii, na tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, TAMWA tunaomba yafuatayo:

i. Vyama vya siasa, wanasiasa na jamii, kutumia lugha ya staha wanapomzungumzia, kumuandika au kumuelezea mgombea mwanamke.

ii. Vyama vya siasa vijenge tabia ya kuwaamini na kuwapa nafasi wanawake katika majimbo ya uchaguzi ili kuongeza ushiriki wao.

iii. Wanasiasa kuacha kutumia kigezo cha talaka, sura yake, idadi ya watoto wake, umbile lake, aina ya ndoa yake, katika kampeni za uchaguzi huu na badala yake wagombea wapimwe kwa ufanisi.

iv. Jamii na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza maudhui ya utupu, udhalilishaji na lugha zisizo za staha kwa wagombea wanawake.

v. Jamii kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha sera kupinga kauli za chuki na maudhi kwa wanawake na wasichana wanaogombea nafasi za uongozi badala ya kumshambulia kwa kutumia maisha yake binafsi.

vi. Taasisi, asasi za kiraia, kukemea pale ambapo mgombea mwanamke anadhalilishwa au kutwezwa utu wake wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

vii. Wanawake wawape ushirikiano wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao na kuepuka kusambaza maudhui yanayowadhalilisha na kutweza utu wao.

vii. Vyombo vya habari, kuendelea kusimama maadili ya kihabari, ambayo yatatoa taarifa sawa kwa wagombea wote bila ubaguzi na kulenga katika sera badala ya kumshambulia mtu binafsi.

Tunapoadhimisha siku watanzania tuungane pamoja kuharakisha mabadiliko ya kuwa na jamii yenye mtazamo wa kijinsia iliyo tayari kwa maendeleo endelevu!

Dk Rose Reuben

Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA

Search