Press Release

TAMWA waukumbuka mchango wa Rais BWM katika usawa wa jinsia

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinaungana na Watanzania wote kuomboleza kifo cha Mwanadiplomasia Mkongwe, mwanahabri mahiri na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.

TAMWA inakumbuka mchango wa Rais Mstaafu Hayati BWM katika kuijenga nchi hii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni lakini hasa inaukumbuka mchango wake katika kujenga na kuhimiza usawa jinsia, kisheria, kisera na katika ngazi za maamuzi.

 

Mmoja wa waanzilishi wa TAMWA, Eda Sanga anaukumbuka mchango wa Hayati BWM katika kusimamia ubora wa habari, usawa wa kijinsia hasa sheria ya makosa ya kujamiiana ya Sospa ya mwaka 1998.

“Mimi binafsi nimefanya naye kazi kwa ukaribu kabisa, nikiwa nafanya kazi RTD, yeye alikuwa anasoma taarifa habari na mimi nikisimamia vipindi vya external services”

Mama Eda anasema, wakati wa mkutano wa  Beijing ulioangazia masuala ya usawa wa kijinsia Rais alikuwa Hayati Mkapa. Na hata tulipomaliza mkutano  na ripoti kuandikwa, yeye ndiye aliyepokea ripoti.

 “Wakati anaipokea tulimuona ana mtazamo chanya akionyesha kuyakubali masuala tuliyoyazungumza kule likiwamo suala la elimu, afya, ambavyo vinahusu zaidi wanawake,” anasema

Mama Eda anamkumbuka Hayati BWM kwa kusimamia sheria zenye mrengo wa jinsia ikiwamo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya  Sospa mwaka 1998.

“Huyu ndiye alikuwa waziri wetu wa habari, wakati tunaanzisha TAMWA. Mimi nikiwa na wenzangu  tulienda ofisini kwake tukiwa na nakala ya jarida la ‘Sauti ya siti’, tulimpa ili alione asije tu kuliona mtaani. Tukaongea naye, ili akubaliane na yale tuliyotaka, kwa sababu wakati huo tulikuwa ni waandishi wa vyombo vya habari vya serikali,”

 “Huyu baba alisaidia sana kuwaona wanawake katika sura hiyo mpya, sura ya kufanya taifa liwe na usawa wa kijinsia, kwa kuwa sote tunaamini kuwa taifa likiwa na wanaume peke yake, ni sawa na mtu anayekwenda na mguu mmoja.”

Mama Eda anasema alikuwa ni mtu mzuri kwa upande wa haki za wanawake na katika kuendeleza taaluma ya habari akisisitiza habari zizingatie ustaarabu, umoja na utamaduni wetu.

Mwanzilishi mwingine wa TAMWA Rose Haji Mwalimu, anamkumbuka Hayati BWM kwa kupambana na kumaliza mauaji ya vikongwe.

“Rais Mkapa tunamkumbuka kwa mengi, alikuwa mstari wa mbele, hasa katika kutetea haki za jinsia, ameongeza idadi ya wanawake katika uongozi, na kumaliza mauaji ya vikongwe”anasema

Anasema kati ya mambo aliyoyafanya ni kusimamia maadhimio ya mkutano wa Beijing  baada ya mwaka 1995.

“Maadhimio hayo yametupa hamasa nyingi TAMWA katika kutetea masuala mbalimbali ya jinsia. Alisaidia kupitisha sheria ya makosa ya kujamiiana 1998, katika miaka ambayo kulikuwa na ubakaji na unyanyasaji ulioshika kasi kubwa. Alitambua na kujua kwa nini TAMWA na wadau wengine  wanahimiza haki na usawa wa kijinsia,”anasema Rose Mwalimu

Mama Rose anasema Sera ya jinsia, imetoa dira, mwongozo na kuweka misingi ya taifa linalosimamia misingi ya jinsia.

“Kupitia sera ya jinsia aliyopitisha tunaona asasi kama TAMWA zikiwa na nguvu ya kupigania masuala ya usawa na hata kuanzishwa kwa  madawati ya jinsia katika vituo vya  polisi,” anasema na kuongeza:

“Kwa kweli ni pigo kubwa kwa TAMWA kupoteza nguli huyu wa habari, kutokana na mchango wake katika masuala ya jinsia, nashauri TAMWA tungefanya mkesha kumuenzi  jemedari huyu.”

Mwasisi mwingine wa TAMWA, Maria Shaba anasema:

Anasema anamkumbuka kwa mengi, lakini hatasahau mkono wake katika kupitisha Sheria ya Makosa ya Kujamiaana mwaka 1998.

“Mwaka 1998, lilipopelekwa  azimio huko bungeni la kuundwa kwa sheria ya kujamiiana, rais aliweka mkono, kukubali kupitisha sheria ya kujamiiana, ile ya Sospa, wakati wake, mambo mengi ya kijinsia yalipewa kipaumbele” anasema

Mwanzilishi mwingine wa TAMWA na mwanaharakati wa masuala ya jinsia, Leyla Sheikh anasema:

“Tumepoteza champion wa haki jinsia. Tutamkumbuka kwa mengi aliyofanya kuleta haki jinsia, kuondoa unyanyapaa, dhidi ya watu wanaoishi na VVU, kutokomea ukeketaji, mauaji ya vikongwe kwa tuhuma za uchawi, kuongeza idadi ya wanawake kwenye nafasi za uongozi,”

“Kwa ufupi wanaharakati  tunaombolea msiba huu mzito kwa maamuzi makuu aliyofanya mzee wetu BWM, kwanza aliruhusu kupitishwa kwa sheria ya makosa ya kujamiiana, SOSPA 1998, Kwa hili hatutamsahau Abadan, mzee wetu mpendwa”

Anasema katika uongozi wake, alipitisha sheria ya ardhi  na sheria ya vijijini 1999. Hizi sheria zimetupatia umiliki madhubuti wa ardhi yetu sisi wananchi na zimeweka bayana haki ya mwanamke kumiliki maeneo ya kilimo na majengo.

“Sera ya jinsia ya mwaka 2000, imetupa mwelekeo na miongozio na kuweka msingi wa kuwa na taifa lenye kusimamia haki jinsia na kuweka fidia kwa mwathirika wa ubakaji, unajisi nangono lazimishi.”anasema Sheikh

Mwanzilishi mwingine wa TAMWA, Ummy Mahfoudh anasema:

“Jambo moja linalogusa kwake ni unyenyekevu aliokuwa nao. Alikuwa na unyenyekevu, si kwa mkubwa wala mdogo, maskini wala tajiri. Alikuwa ni mtu mwenye busara.

Mahfoudh anasema kwenye usawa wa kijinsia, bunge na safu yake ya mawaziri ilikuwa na usawa wa kijinsia, si kwa sababu alichagua tu jinsia, bali alijali sana vigezo

 “Kwenye suala la muungano, alikuwa ni muumini wa muungano,” anasema Mahfoudh

MWISHO

Search