Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimesikitishwa na uteuzi usiozingatia usawa wa jinsia, wa Kamati ya Kuratibu Mdundo wenye asili ya Tanzania, uliofanywa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa .
Katika taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, John Mapepele, juzi, Julai 20, 2022, imeelezwa kuwa, Waziri Mchengerwa ameteua kamati hiyo itakayoratibu upatikanaji wa mdundo wenye asili ya kitanzania.
Mdundo wenye asili ya kitanzania, ni eneo nyeti kwa taifa, litakalobeba taswira ya utamaduni wetu na kielelezo halisi cha muziki wa Kitanzania ambao unalitambulisha taifa kwa mapana.
Hata hivyo, TAMWA inasikitika kwamba, miongoni mwa wajumbe wa 9 wa kamati hiyo, kuna uwakilishi wa mwanamke mmoja tu, Fatuma Hassan,maarufu kama DJ Fetty.Si hivyo tu, hata Mwenyekiti na Katibu wake, wote ni wanaume.
Kadhalika, hivi karibuni Waziri ameteua kamati maalum ya kuratibu vazi la taifa, ambayo ina Mwenyekiti na Katibu, wote wanaume na wajumbe watano, kati yao, mwanamke ni mmoja tu, mwanamitindo, Khadija Mwanamboka
Si kwamba tunakosoa ubora na weledi wa wajumbe na viongozi wa kamati hiyo, la hasha, lakini TAMWA ambacho kina wajibu wa kutetea ushiriki wa wanawake katika uongozi na maamuzi, kimesikitishwa na uteuzi huu ambao haukuangalia usawa wa kijinsia.
Miongoni mwa wajumbe 9, yupo mwanamke mmoja tu, je ni kweli kwamba katika tasnia ya burudani, vyuoni, sekta ya filamu, sekta ya habari, sekta ya sanaa na utamaduni, hakuna wanawake zaidi wenye uwezo wa kufanya majukumu hayo? Dk Rose Reuben, Mkurugenzi wa TAMWA.
TAMWA inaamini kuwa kuna wanawake lukuki wenye ujuzi, uwezo, ujasiri na wenye kazi za kupigiwa mfano katika sekta ya sanaa na utamaduni ambao wangeweza kutimiza majukumu yaliyoanishwa na wizara katika kamati hizi.
Chama hiki ambacho kwa miaka zaidi ya 30 sasa kimesimamia upatikanaji wa haki za wanawake na watoto, ikiwamo nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi, hatuwezi kunyamaza kimya, tukifurahia uteuzi huu usio na uwiano wa hamsini kwa hamsini.
Tunamuomba Waziri Mchengerwa, ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri katika wizara hiyo, afanyie uhariri orodha ya wanakamati hawa, ili kuwe na uwiano wa kijinsia katika kamati hizi zinazokwenda kufanya kazi kubwa yenye manufaa kwa taifa zima katika sekta ya utamaduni. Dk Rose Reuben
TAMWA inaendelea kuipongeza Wizara kwa kazi njema, ya kuboresha lugha ya Kiswahili na kusimamia maadili ya wasanii.
Dk Rose Reuben (PhD)
Mkurugenzi Mtendaji