Dar Es Salaam, Oktoba 11, 2022. Watanzania leo wanaungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike. Siku hii inaadhimishwa ifikapo Oktoba 11 kila mwaka kama wakati wa kukumbushana kuhusu nafasi ya mtoto wa kike katika nyanja mbalimbali, za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Hivyo basi kwa kuzingatia umuhimu wa siku hii, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kwa kushirikiana na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) tunaikumbusha jamii, wadau na serikali kuwa bado matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike yanaendelea kushika kasi nchini.
Kadhalika, kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo: Muda Wetu ni sasa, haki zetu, Mustakabali Wetu”. TAMWA na WFT tunalenga kuikumbusha jamii kuendelea kuibua na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia, hasa rushwa ya ngono, ubakaji, ulawiti, vipigo na ndoa za mapema kwa watoto wa kike.
TAMWA na WFT tumebaini kuwa licha ya vyombo vya dola kuchukua hatua na kupinga vikali vitendo hivyo dhidi ya watoto wa kike lakini bado matukio ya rushwa ya ngono, ubakaji, ulawiti, mimba za mapema na udhalilishaji yanazidi kushamiri huku watuhumiwa wengi wakiwamo wazazi, walezi, walimu pamoja na watu wao wa karibu ambao ndio wamepewa jukumu la kulinda watoto hao.
Imeshuhudiwa kuwepo kwa matukio kadhaa ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu jambo ambalo linatupa wasiwasi kuwa huenda elimu ya kulinda haki za mtoto wa kike bado haijawafikia wengi.
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na lile la mwanafunzi wa darasa la saba, Shule ya msingi Shahende, Geita, Helena Mashaka (13) anayedaiwa kuchomwa moto mikononi na mama yake hali iliyosababisha kushindwa kufanya mitihani yake ya darasa la saba.
Kadhalika, mtoto Farida Makuya (16) anadaiwa kuuwawa usiku wa Jumanne, Oktoba 4, 2022 nyumbani kwao Mtumba jijini Dodoma na watu wasiojulikana.
Wakati huo huo, Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka na kuwalawiti watoto zaidi ya 10 wa mafundisho ya kipaimara na kisha kuwapa fedha kiasi cha kati ya Sh 3,000 hadi 5, 000.
Tukio jingine ni la mwanafunzi wa darasa la sita, (12), wa Shule ya Msingi Mbagala Kuu, Dar es Salaam, anadaiwa kubakwa na Mwalimu wake, ambapo Mwalimu huyo amekuwa akimpatia binti huyo ufunguo wa makazi yake binafsi ili endapo akimuhitaji aweze kufika kwake kwa urahisi.
Hata hivyo, tunaipongeza serikali kupitia vyombo vya sheria kwa kutumia muda mfupi kusimamia na kutoa hukumu dhidi ya mwalimu wa shule ya msingi ya Global, Dar es Salaam, aliyehukumiwa kifungo cha maisha kwa kubaka na kulawiti mwanafunzi wa miaka minane.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) umebaini kuwa wasichana milioni 120, duniani wamewahi kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao.
Pamoja na ukatili huo kwa watoto wa kike, WFT na TAMWA bado wanasisitiza jamii kuepuka rushwa ya ngono hasa kwa watoto wa kike.
Mwaka 2020, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilichapisha ripoti ya utafiti na kuibua kuwepo kwa rushwa ya ngono katika Vyuo Vikuu viwili vya umma nchini, ambavyo ni Chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
Kadhalika, mwaka 2021, TAMWA kwa kushirikiana na (WFT) ilitekeleza mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari. TAMWA ilifanya utafiti na kubaini wanahabari wanakabiliwa kwa kiasi kikubwa na rushwa ya ngono na ukatili mwingine ndani ya vyombo vyao vya habari.
TAMWA tumebaini kuwa wasichana wanahabari vyuoni hukumbana na vitendo vya rushwa ya ngono na kusababisha wengi kuikimbia taaluma hiyo wakihofia vitendo vya rushwa ya ngono ambayo hukumbana navyo kuanzia wakiwa vyuoni Mkurugenzi wa TAMWA, Dk Rose Reuben.
TAMWA na WFT bado tunaendelea kuipongeza TAKUKURU kwa kufanya mabadiliko ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007. Hii ni dhamira chanya kwa serikali katika kushughulikia uovu huu katika nchi yetu. Kwa njia hii, inabakia kuwa sheria ya msingi katika kujenga msingi wa maadili ya taifa katika ngazi na taasisi zote.
“Hata hivyo katika kifungu kidogo cha 2,cha sheria hii, tumeona kuwa uchambuzi wa sheria unachanganya neno ukahaba na ngono: Pale ambapo kuna makubaliano ya pande zote, ya kubadilishana ngono kwa ajili ya huduma, au pesa, (katika kesi hii hakuna unyang'anyi wa mamlaka). Hivyo tunaomba kuondolewa kwa kifungu kinacholeta utata kati ya rushwa ya ngono na ukahaba Rose Marandu, Mkurugenzi Mtendaji, WFT
Hivyo basi tunapoadhimisha siku hii ya mtoto wa kike, tunatamani dunia itambue thamani yao katika maendeleo, afya yao, elimu yao, uchumi wao na ushiriki wao katika siasa, jamii ikiutambua mchango wao, itasimamia katika ulinzi wao na hivyo kupunguza matukio haya ya rushwa ya ngono.
Tunaomba serikali kupitia Takukuru, kuendelea kujikita katika mapambano haya wakishirikiana na wadau, ili jamii iwe na taarifa za kutosha kuhusu usalama wa watoto wa kike Rose Marandu,WFT
Hatutaacha, hatutanyamaza, hadi uwepo usalama wa watoto wa kike Tanzania!
Dkt. Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)
Rose Marandu
Mkurugenzi Mtendaji
Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT)
Mwisho