Machi 8, 2023, Dar Es Salaam. Leo dunia inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Kwa mwaka huu, Siku hii inaadhimishwa ikipambwa na kauli mbiu isemayo, “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu Katika Kuleta Usawa wa Kijinsia”
Kauli mbiu hii inatukumbusha pengo lililopo katika teknolojia, kwa upande wa wanawake na watoto wa kike hasa nafasi ya teknolojia katika kuhakikisha usalama, amani, na usawa kwa kundi hilo.
Tunaadhimisha siku hii, huku bado kukiwa na mapengo kadhaa yanayoibua changamoto za usawa wa kijinsia.
Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuonyesha athari za kijinsia za mapinduzi ya kidijitali na kuangalia jitihada za pamoja zinazoweza kufanyika kupunguza mgawanyiko wa kijidijitali katika mlengo wa kijinsia.
Kadhalika, maadhimisho haya yanatumika kama jukwaa la majadiliano ya kisera, ili kujenga uwezo kwa wadau mbalimbali katika kuimarisha ujuzi wa ubunifu, na pia kubadili muundo wa teknolojia ya kidijitali unaokidhi mahitaji ya wanawake na watoto wa kike.
Pia, kuhakikisha kuna ubadilishanaji wa uzoefu katika matumizi anuwai ya teknolojia ili kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika zama za kidijitali.
Maadhimisho ya mwaka huu yanatupa nafasi ya kutafakari, hatua madhubuti za siku zijazo zitakazowezesha matumizi sahihi ya kidijitali kwa watoto wa kike.
“Hebu fikiria dunia yenye usawa wa kijinsia, isiyo na upendeleo wala unyanyasaji wa kijinsia, dunia jumuishi isiyokuwa na habari potofu. TAMWA tunaamini ni muhimu tuungane kwa pamoja kujenga usawa kwa kuongeza ubunifu na matumizi chanya kwa wanawake na watoto wa kike.” Mkurugenzi wa TAMWA, Dk Rose Reuben
TAMWA tunaamini tunaweza kuibua changamoto zinazowakabili wanawake na watoto wa kike, kuhamasisha kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, na kuwapongeza wanawake na watoto wa kike, waliofanya vyema katika jamii yetu.
“Teknolojia ikiwamo mitandao ya kijamii, itumiwe vyema kuibua madhara ya ukatili wa kijinsia na habari potofu mitandaoni, kuasa juu ya vitendo vya udhalilishaji na zaidi kuonyesha fursa zinazokuja na ukuaji wake kwa wanawake na wasichana katika jamii, hayo ndiyo mafanikio tunayoyatarajia,” Dk Rose Reuben
Utafiti uliofanywa na taasisi ya Women at Web kwa kushirikiana na TAMWA, umebaini kuwa, asilimia 79 ya wanawake wanasiasa na wanaharakati wa kisiasa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao wakati wa uchaguzi Mkuu wa 2020.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa, uchaguzi mkuu wa 2020, umeonekana kama moja ya nyakati ambapo idadi kubwa ya wanawake katika siasa walikabiliwa na unyanyasaji wa mtandaoni, hasa wale wa nafasi za viti maalum 19 vya upinzani ambao walipewa majina mbalimbali na kudhalilishwa mtandaoni kwa muda mrefu.
Hali hiyo inaonyesha wazi na kulingana na utafiti huo ni dhahiri kuwa teknolojia imeleta neema lakini wakati mwingine, inatumiwa vibaya na kusababisha madhara.
TAMWA tunaitaka jamii yetu kuzitambua na kuzitumia fursa mbalimbali zinazokuja na Teknolojia, kama vile biashara, ajira, mawasiliano rahisi na hivyo ichagize maendeleo na ubunifu , i pamoja na kuhamasisha usawa wa kijinsia.
Wakati tunaendelea na kumbukizi za Siku ya wanawake Duniani TAMWA tunawakumbusha Watoto wa kike na wanawake wanaotumia teknolojia, wazitumie kwa manufaa, wakawekeze, na endapo wanashambuliwa na kudhalilishwa kwa nanmna yoyote ile wakatoe taarifa ya matukio ya ukatili, ili serikali na wadau wengine wa usalana wayafanyie kazi na yakomeshwe kabla ya kuleta madhara makubwa.
“Kama wachapishaji wa jarida la Sauti ya Siti, tuliweza kuonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii na tukafanikiwa kwa kutumia fasihi andishi, tunaamini pia, fasihi hiyo hiyo ikitumika vyema kidijitali, itamuinua mwanamke na mtoto wa kike wa kitanzania” Dr Rose Reuben
TAMWA tunaamini katika nguvu chanya ya teknolojia, na tunatamani teknolojia hii imuinue mwanamke wa Kitanzania, kisiasa, kiuchumi na kijamii.
“ Ni wakati sasa wa kuongeza ubunifu na matumizi ya teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya kijinsia ili tuwe na taifa lenye usawa” Dr Reuben
Dk. Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA