Press Release

Rushwa ya Ngono na Unyanyasaji wa Kingono Mahala pa Kazi, Shuleni ,Taasisi za Elimu, Ijadiliwe kwa Upana na Uwazi

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Novemba 29, 2022, Dar es Salaam. Miaka minne iliyopita, Chama cha  Wanahabari Tanzania(TAMWA) ilitekeleza mradi wake wa kuchapisha habari za uchunguzi juu ya unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na vyuo vikuu.
 
Mwaka mmoja uliopita, TAMWA ilitekeleza mradi mwingine uliofanana na huu, kwa kufanya utafiti kuangalia hali halisi ya rushwa ya ngono katika vyumba vya habari. 
Yote haya, yaliiwezesha TAMWA kubaini kuwa kuna tatizo  kubwa la rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika elimu ya vyuo vikuu. Matokeo ya tafiti na uchapishaji wa habari kuhusu rushwa ya ngono, yalichagiza wadau na waathirika kuweka wazi hali halisi ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono katika mazingira ya kazi na elimu.  
 
Hivyo basi, leo wakati dunia inafanya maadhimisho ya Siku 16 kupinga ukatili wa jinsia,  yanayokwenda na kauli mbiu isemayo: Kila uhai una thamani, tokomeza mauaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
 
TAMWA  kwa kushirikiana na wanamtandao wa kupinga ukatili wa jinsia hapa nchini pamoja na  wadau wetu wa maendeleo  kwanza tunajisikia fahari kuibua mengi kuhusu athari ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika taasisi za elimu na kwa kuendeleza mjadala huu katika jamii kupitia vyombo vya habari.
 
TAMWA kupitia miradi yake inayohimiza kuzuia ukatili katika jamii, tumeweza kufanya yafuatayo;
Kwanza, kuvunja ukimya uliotawala miongoni mwa wanahabari katika kusema kinagaubaga au kundika kuhusu madhila wanayopitia wanapodhalilishwa kingono.
 
TAMWA imebaini asilimia 48 tu ya wanahabari ndio wanaoweza kusema wazi kuhusu madhila ya rushwa ya ngono wanayopitia katika vyumba vya habari. Asilimia 52 inayobaki, hawawezi kusema wazi kuhusu changamoto hiyo.
Kadhalika TAMWA kwa kushirikiana na wadau wakiwamo Internews na WFT na Tasisi ya kuzuia Rushwa (TAKUKURU)wamebaini kuwa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu ni janga kubwa linalochagiza kushuka kwa kiwango cha taaluma, kuzalisha wahitimu wasio na sifa na kuharibu talanta kwa wale wanaokataa rushwa hiyo. 
 
Tumebaini kuwa wanahabari wengi wanawake wameacha kazi kwa kuhofia udhalilishaji wa kijinsia katika tasnia hiyo, wapo wanafunzi waliohama vyuo na kuacha shule kwa kuombwa rushwa ya ngono.  
Kadhalika, imebainika kuwa wapo viongozi katika maeneo ya kazi, wanaotoa kazi kwa upendeleo kwa kuomba rushwa ya ngono badala ya kuangalia uwezo na vipaji. 
Juzi akifungua kongamano la wadau wa rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wakufunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, jijini Dodoma, Naibu Waziri Utumishi, Deogratius Ndejembi, amesema rushwa ya ngono inasababisha kuzalishwa wasomi wasio na tija na kuwanyima haki wanafunzi.  
Kauli ya Ndejembi inachochea mjadala unaoonyesha  zaidi ukubwa wa tatizo hili na kutukumbusha watanzania  kuchukua hatua za ziada  kupambana na rushwa ya ngono mashuleni, vyuoni na katika sekta ya ajira na utumishi wa umma, tatizo ambalo linatishia kuharibu vipaji. 
“Hivyo basi, huu ni wakati kwa wadau wanaopinga ukatili wa  jinsia, watetezi wa haki za binadamu, wahanga wa ukatili na serikali   kukumbushana kuwa rushwa hii inavunja haki za binadamu, ni kosa la jinai kisheria, inaharibu utu, na inaua vipaji hapa nchini amesema Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dk Rose Reuben. 
 
TAMWA na WFT Tunaiomba serikali kama ambavyo tayari imeshaanza kulichukulia kwa uzito suala hili, iendelee kuwawajibisha wale wanaomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi na kwa wafanyakazi.Kadhalika, , tunaomba wanafamilia, wanawake  na wanaume, vijana wa kike na wakiume na jamii kwa ujumla,  wadau wa kuzuia ukatili wa jinsia, wahanga wa rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono kushiriki katika mijadala inayoweza kuleta suluhisho la janga hili tupinge ukatili wa kijinsia na kuhamasisha uwazi zaidi. 
 
“Sote tunaweza kuwa watetezi na sauti zetu kwa pamoja zinaweza kuleta  mabadiliko tunayotafutaDr Rose Reuben.
 
Tunapoadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, TAMWA tunatamani  kuwa asiwepo yeyote, popote pale, atakayefanyiwa  ukatili wa kijinsia hapa nchini. Lakini zaidi hasa tunasema; Rushwa ya ngono mahala pa kazi, vyuoni na mashuleni ni janga na inarudisha nyuma maendeleo ya jamii yetu.
Dr Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA.

Search