Press Release

TUWALINDE WATOTO WA KIKE NA UKATILI WA KIJINSIA KWA NJIA YA MTANDAO

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active
 
Dar Es Salaam, October 11, 2021. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinawakumbusha, wazazi, walezi, wadau, serikali na waandishi wa habari kuchukua hatua ili kuondoa aina mpya ya ukatili kwa njia ya mitandao ya kijamii.
 
Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Oktoba 11, ambapo kwa mwaka huu, kauli mbiu ya kitaifa na kimataifa ni: Kizazi cha Kidijitali, Kizazi Chetu!.
 
Kauli mbiu hii inalenga kuikumbusha jamii kutoa haki sawa kwa watoto wote kwenye teknolojia ya kidijitali ili waitumie  kwa Maendeleo na kwa usahihi.  
 
Zipo faida lukuki za matumizi ya mitandao ya kijamii, kama vile elimu kwa njia ya mitandao, taarifa muhimu za kitaifa na kimataifa lakini  bado watoto wa kike wameonekana kuachwa nyuma katika ulimwengu wa kidijitali kwa kukosa  fursa sawa hasa katika matumzi ya intanenti, kumiliki simu janja, na uhuru wa  kutumia mitandao ya kijamii kama ilivyo kwa watoto wa kiume. 
 
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya wanawake, (UN-Women) Julai mwaka huu, ilionyesha kuwa kuna ongezeko la ukatili wa kijinsia kupitia mitandao ya kijamii. 
 
Ripoti hiyo imeeleza: Upatikanaji  wa intaneti kwa watoto wa kike na wanawake, umesababisha kundi hilo kukumbana na udhalilishaji wa kingono zaidi, ukilinganisha na wanaume,
 
Kadhalika ripoti hiyo imeonyesha zaidi kuwa, watoto wa kike wamekuwa wakitishiwa kimwili, kutumiwa picha za ngono, na kupewa lugha dhalili katika mitandao ya kijamii.
 
Kwa hapa Tanzania, matukio kadhaa ya udhalilishaji wa kingono kwa njia ya mtandao yamewahi kuripotiwa ikiwamo kusambazwa kwa video za ngono zikiwaonyesha watoto wa kike, huku mwanaume akifichwa uso.
 
Aina nyingine ya ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao ni kashfa na matamshi ya chuki, jina la akaunti kuibwa na  na kisha kutumiwa na watu kwa njia za utapeli au kurushwa kwa video za ngono. Hili limewakuta zaidi watoto wa kike wenye majina makubwa au maarufu katika jamii. 
 
Lakini pia, imekuwa ni tamaduni kwa watoto wa kike kurushiwa lugha dhalilishi kwa njia ya mtandao, ikiwamo zile zinazohusisha baadhi ya maungo yao ya mwili.
 
Picha za watoto wa kike zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii na kugeuzwa mjadala jambo ambalo limeonekana kuchangia kuongezeka kwa lugha dhalili dhidi yao.
 
Kutokana na kuongezeka kwa matukio haya yanayoendana na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii, hatuna budi kupunguza udhalilishaji huu na kuendelea kuhimiza matumizi sahihi, salama na yenye faida, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben.
 
Reuben ameomba  wazazi, walezi, serikali, asasi za kijinsia, asasi za kiraia, wapatanishi na wanahabari, kusimamia usalama wa watoto kike mitandaoni. 
 
Inawezekana tabia hizi zinaonekana kuwa ni za kawaida au kugeuzwa utamaduni lakini zimeleta madhara kwa watoto wa kike ikiwamo kukatisha masomo, kujiua, kutengwa na jamii na baadhi kuathirika kisaikolojia, Dkt, Reuben
 
TAMWA inaamini katika usawa wa kijinsia, haki za watoto na wanawake, hivyo katika kuadhimisha siku hii, tunaikumbusha serikali kutunga sheria zinazoendana na kasi ya teknolojia ili kuwabana wale watakaofanya ukatili wa kingono kwa njia ya mtandao.
 
Sheria isifumbe macho katika masuala haya, lakini si hayo tu, bado tunasisitiza hata ile sheria ya ndoa  ibadilishwe ili kumpa mtoto wa kike haki ya kusoma na kuolewa katika umri wa utu uzima Dkt. Reuben
 
TAMWA inapenda kutoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa matumizi ya dijitali katika jamii yetu ili kuendana na uhalisia wa dunia, pia  kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kutoa na kuwezesha watoto wote kupata elimu ya masuala ya dijitali pia kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya kidijitali  kwa kuzingatia jinsi zote bila ubaguzi.
 
TAMWA inaamini kuwa, maadhimisho ya mwaka huu, yataangazia  changamoto na fursa za kidijitali  kwa mtoto wa kike lakini bila kusahau, kuwa kumbe; malezi bora, elimu kwa mtoto wa kike ndicho chanzo cha leo kuwa na Rais wa kwanza mwanamke, ambaye ni Mama Samia Suluhu.
 
Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni siku ya kimataifa iliyotangazwa na Umoja wa Mataifa; pia inaitwa Siku ya Wasichana na Siku ya Kimataifa ya Wasichana. Siku hii huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 11.
 
Umoja wa Mataifa ulianza kuadhimisha siku hii baada ya kuonekana kuna changamoto nyingi zinazomuandama mtoto wa kike ikiwamo kunyimwa fursa ya kupata elimu, ubakaji, ulawiti,  ndoa za mapema, mimba za mapema na kukosa haki nyingine ikiwamo ya kucheza na kushauri katika ngazi ya familia. 
 
Maadhimisho hayo pia yanaangalia  mafanikio ya watoto kike kidunia, ikiwamo Tanzania kama vile  kuongezeka kwa idadi ya watoto wa kike wanaopata elimu ya juu, watoto wa kike kuendelea kupata elimu ya afya ya uzazi na kufikiwa na taasisi mbalimbali zinazogusa maisha ya mtoto wa kike.
 
Kizazi cha Kidijitali, Kizazi Chetu!
 
Dkt Rose Reuben.
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA

Search