Press Release

UWEPO WA RUSHWA YA NGONO VYUONI

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive
 
Dar Es Salaam, Oktoba 29, 2021.
 
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA) kinalaani  tukio la Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, kudaiwa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wa kike chuoni hapo.
 
Taarifa iliyotolewa na Chuo hicho baada ya kusambaa kwa jumbe za uwepo wa tukio hilo chuoni hapo katika mitandao ya jamii,  imeeleza kuwa Mhadhiri huyo, Petrol Mswahili, amefanya vitendo hivyo kwa wanafunzi wa kike, jambo linalodhihirisha uwepo wa rushwa ya ngono. 
 
TAMWA ikiwa ni taasisi inayopinga unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake ikiwamo rushwa ya ngono, tunalaani  tukio hilo linalovunja maadili ya utumishi wa umma na zaidi hasa kudhalilisha watoto wa kike katika taasisi hii ya elimu ya juu.
 
Kadhalika, TAMWA tunasikitishwa na  vitendo hivyo ambavyo sio tu vimekuwa chanzo cha kuharibu mustakabali wa kitaaluma wa watoto wa kike, lakini pia ndicho chanzo cha magonjwa ya kuambukiza, sonona na kurudisha nyuma kundi hilo. 
 
Mwaka 2019 TAMWA ilifanya tathmini ya kuangazia ukubwa wa rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari, maeneo ya kazini na taasisi za elimu ya juu, na kubaini kuwa tatizo hilo lipo kwa ukubwa wake.
 
Kadhalika TAMWA ilibaini kuwa ukimya umetawala kwa wale waathirika wa rushwa ya ngono kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo woga wa kukosa vibarua, kufukuzwa shule au kufeli mitihani yao. 
 
Hivyo tunalaani vikali vitendo hivi huku tukiupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuchukua hatua za haraka dhidi ya mhadhiri huyo lakini pia tunaushauri uongozi wa chuo hicho kuweka mikakati itakayokomesha vitendo hivyo.
 
TAMWA inaomba pindi uchunguzi utakapokamilika basi sheria ichukue mkondo wake ili iwe funzo kwa wahadhiri wengine wanaoharibu watoto wa kike. Pia tunaiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) iendelee kushirikiana na wadau kutoa elimu kuhusu rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine wa kijinsia. 
 
"Digrii bila rushwa ya ngono, ni digrii yenye tija"
 
Imetolewa na;
 
Mkurugenzi Mtendaji waTAMWA,
 
Dk Rose Reuben.
 

Search